Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Meja Jenerali Samuel Albert Ndomba
(pichani kushoto) kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ).
Aidha, Rais Kikwete amempandisha cheo Meja Jenerali Ndomba kuwa Luteni
Jenerali. Taarifa iliyotolewa leo, Ijumaa, Septemba 21, 2012, mjini Dar
Es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue kupitia
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais – Ikulu, imesema kuwa uteuzi huo
unaanza leo.
Taarifa hiyo ya Balozi Sefue imesema kuwa kabla ya uteuzi wake, Meja
Jenerali Ndomba alikuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Jenerali Ndomba anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Jenerali
Abdulrahman A. Shimbo ambaye amestaafu Jeshi kwa mujibu wa sheria baada
ya kufikisha umri wa miaka 60.
Taarifa ya Balozi Sefue pia imesema kuwa Rais Kikwete amemteua Brigedia
Jenerali Raphael Mugoya Muhuga (pichani kulia) kuwa Mkuu wa Jeshi la
Kujenga Taifa kuanzia leo, Ijumaa, Septemba 21, 2012.
Aidha, Rais Kikwete amempandisha cheo Brigedia Jenerali Muhuga kuwa Meja
Jenerali. Kabla ya uteuzi wake, Brigedia Jenerali Muhuga alikuwa Mkuu
wa Utawala na Mafunzo wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu. Dar es Salaam. 21 Septemba, 2012
Post a Comment