Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (kulia), akikabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa utendaji wa bandari ya Dar es Salaam kutoka kwa Mwenyekiti wa kamati aliyounda kufanya kazi hiyo, Bernard Mbakileki (kushoto) jijini Dar es Salaam jana.
...........................
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amekabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam na kuelezwa kuwa kuna watu muhimu waliihujumu kwa kukwepa kuhojiwa kwa visingizio mbalimbali.
Dk, Mwakyembe ameelezwa kuwa miongoni mwa visingizio hivyo ni kuuguliwa, kufiwa na wengine kuzima kabisa simu zao za mikononi ili wasipatikane.
Kauli kuhusu watu hao kukwepa kuhojiwa, ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Wakili Bernard Mbakileki, wakati akimkabidhi Waziri Mwakyembe ripoti hiyo jijini Dar es Salaam jana.
Mbakileki alisema kamati yake iliyokuwa na wajumbe saba, iliwahoji watu 116, wakiwamo wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wafanyakazi, menejimenti na uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari Tanzania (Dowuta).
Pia walitembelea Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambako walionana na Kamishna wake Mkuu, Wakala wa Vipimo (WMA), ambako walionana na Ofisa Mtendaji wake Mkuu na maofisa wengine wa Kitengo cha Kupakia na Kupakua Makontena (Ticts), ambako walionana na meneja wake mkuu na maofisa wengine.
Vile vile, kamati ilipitia nyaraka mbalimbali, ikiwamo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria mbalimbali, mikataba, nyaraka za zabuni na mihutasari ya vikao.
Alisema mahojiano yalichukua dakika zisizopungua 50 kwa kila aliyehojiwa. “Baadhi ya waliohitajika kuhojiwa walikwepa kwa visingizio mbalimbali ikiwamo kuuguliwa na kufiwa na wengine kuzima simu kabisa,” alisema Mbakileki na kuongeza kuwa suala hilo wanamuachia Waziri Mwakyembe.
Alisema pia kamati ilitumia mtandao kupata taarifa kutoka nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kutembelea pia eneo la Upakuaji na Upakiaji wa Mafuta (KOJ) na Polisi Chang’ombe.
Mbakileki alisema walitembelea Polisi Chang’ombe kupata taarifa kuhusiana na wezi waliovamia KOJ kwa lengo la kupoteza ushahidi.
Alisema wadau wengi walijitokeza na kwamba, licha ya baadhi ya magazeti kujaribu kuchapisha habari zilizolenga kuitisha na kuikatisha tamaa kamati, ilifanya kazi yake vizuri kwa kusimamia nguzo muhimu ya ukweli na haki, ambavyo alisema viliwaweka huru.
Akipokea ripoti hiyo, Waziri Mwakyembe, alisema kamati hiyo iliundwa kwa lengo la kuangalia chanzo cha kuzorota kwa huduma katika bandari hiyo kiasi cha kukimbiwa na wateja wa ndani na nje ya nchi.
Alisema hali hiyo imesababisha Watanzania wengi, ambao ni wafanyabiashara kutoitumia bandari hiyo, badala yake sasa wanatumia bandari ya Mombasa, nchini Kenya.
Aliihakikishia kamati hiyo kwamba, kazi iliyoifanya haitakwenda bure na kwamba, mapendekezo yote yaliyomo kwenye ripoti hiyo ya kuitaka serikali kuibadilisha bandari hiyo ili kiwe chombo cha kutegemewa ndani na nje ya nchi, yatatekelezwa.
“Mmetumia muda, mmejitoa kwa hali na mali. Ni suala zito lenye changamoto kubwa. Hatuwezi tukaachia taarifa (ripoti) hii ikakaa kwenye makabati,” alisema Waziri Mwakyembe.
Alisema mpaka kufikia Desemba, mwaka huu, watakuwa wametekeleza yote yaliyomo kwenye ripoti hiyo.
Waziri Mwakyembe alisema alisoma kwenye ripoti ya awali na kuona kwamba, kuna mambo mengi yanayotakiwa kutekelezwa.
Hivyo, alisema atakaa na wenzake na kuiperuzi ripoti hiyo ukurasa kwa ukurasa ili kuangalia kila kitu na kusema ana uhakika wataipa bandari hiyo sura mpya, kinyume cha ilivyo sasa.
Alisema jambo kubwa lililomshtua wakati anateua kamati hiyo, ni taarifa za asasi za kimataifa, ambazo alisema zinaielezea bandari ya Dar es Salaam kuwa kati ya bandari 36 kubwa barani Afrika, ndiyo inayoongoza kwa kukosa ufanisi, na kusema: “Hii inauma sana”.
Waziri Mwakyembe alisema tofauti na bandari nyingine, ambazo kupokea kontena huchukua siku moja au siku nne, bandari ya Dar es Salaam huchukua siku 10 mpaka 25, na kuhoji: “Kuna mdudu gani hapa?”
Alisema pia katika bandari ya Dar es Salaam ni gharama zaidi kupokelea mizigo yote, ambako wanaongeza dola za Marekani 400 kuliko bandari ya Mombasa, na kuhoji: “Kwanini?”
Pia alisema kumekuwa na vitendo vya udokozi wa mizigo inayoshushwa katika bandari ya Dar es Salaam, ambapo alisema imekuwa vigumu mzigo kupita bila kudokolewa au mwenye mzigo kutakiwa kutoa kitu cha juu.
“Hakuna chombo kinapita bila kudokoa. Tutakuja na maamuzi na wahakikishia hakutadokolewa kitu. Kikidolewa kitu, wale wote waliohusika watadokolewa vilevile,” alisema Waziri Mwakyembe.
Alisema Watanzania wameanza kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu vya historia katika utapeli wa kimataifa.
“Mimi nilidhani mwanzoni kwamba, tumeingia kwenye rekodi ya kimataifa kwa kumuingiza twiga kwenye ndege. Maana hata twiga alivyo mrefu na mkubwa unamuingizaje muingizaje ndani ya ndege? Nikadhani itaishia hapo. Lakini kuna matukio makubwa zaidi ya twiga,” alisema Dk. Mwakyembe na kuongeza:
“Kontena na ukubwa wake ule linayayuka tu kama kiberiti juu ya meza mtu anaingiza kwenye mfuko. Kontena unaliona hapa leo, baada ya dakika 15 halipo wala hamna mtu anajua limepitia wapi. Ndiyo bandari ya Dar es Salaam.
Halafu baadhi ya ndugu zangu wanategemea tukae chini. Tukae kimya. Tuliapa kufanya kazi na kuitumikia nchi tutafanya hivyo.”
Alisema katika matukio ya kupotea kwa makontena kwa wizi wa aina yake, mwaka juzi, yalipotea makontena 10, mwaka jana makontena 26 na mwaka huu kabla hajateuliwa kuongoza wizara hiyo makontena mawili katika bandari ya Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa watatekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyo kupitia ripoti yake.
Alisema katika kutekeleza hilo, watapitia kila kitu kwa makini na kwamba, hawatamuonea mtu yeyote, badala yake watatenda haki kwa kila mtu na vilevile wataitendea haki nchi pia.
Waziri Mwakyembe alisema katika jitihada, ambazo zimekwishafanywa na wizara yake, baadhi ya nchi jirani zimeanza kuamini kwamba, kuna mabadiliko yameanza kuonekana katika bandari ya Dar es Salaam.
Alisema tayari amekwishapokea mawaziri zaidi ya wanne na ujumbe, baadhi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ubalozi, pia amekuwa na mawaziri wa uchukuzi wa Burundi, Rwanda na Uganda, ambao alisema wameonyesha hamu ya kutumia tena bandari ya Dar es Salaam.
“Na nimewahakikishia kuwa patabadilika (katika bandari ya Dar es Salaam). Na lazima pabadilike. Patabadilika tu. Utake usitake patabadilika,” alisema Dk. Mwakyembe na kuongeza:
“Wale wote wale wanaona kwamba, mabadiliko haya yanawakera, kazi ziko nyingi sana nchi hii waondokea. Lakini bandari itabadilika.”
Alisema utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti hiyo hawataufanya kwa pamoja, bali watafanya kwa awamu, na kwamba, kabla ya wiki kuisha, wataueleza umma ni hatua gani za mwanzo watachukua.
Alisisitiza kuwa kufikia Desemba, mwaka huu, watakuwa wamehitimisha utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti hiyo ili kuweka misingi imara ya bandari inayoaminika katika ukanda wa Afrika.
Akijibu swali kuhusu hatima ya watu waliokwepa kuhojiwa kwa visingizio mbalimbali, Waziri Mwakyembe alisema kama walidhani kukwepa kwao huko kutawapunguzia maswali, basi watakwenda kuyajibu mbele ya waziri.
“Mimi nitakaa hapa na wenzangu kama ni mambo ni makubwa zaidi yanahusu polisi, basi atajikuta anaenda polisi. Hatutaamuacha mtu. Hili ni fagio la kusafisha, tusafishe. Kama sehemu ni safi tutaacha safi vilevile. Lakini tuna wajibu mkubwa hatuwezi kuacha chochote bila kufanyia kazi,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema kila baada ya wiki moja au mbili watakuwa wanatoa taarifa kwa umma za utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti hiyo.
Kamati hiyo iliteuliwa na Waziri Mwakyembe Agosti 27, ilipewa hoja 34 za kufanyia kazi na ilianza kazi yake rasmi Agosti 31, mwaka huu.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo, ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM), Mhandisi Ramo Makani (Makamu Mwenyekiti wa Kamati), John Wanga, Halima Mamuya, Said Sauko, Richard Kasesela na Bernardina Mwijarabu.
CHANZO: NIPASHEA
Post a Comment