NDANI ya
miaka saba tu, Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), ameteua makatibu wakuu watatu - Yusuf Makamba, Wilson
Mukama, na Abdulrahman Kinana.
Mtangulizi
wake, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kwa miaka yote aliyokaa madarakani
(10), alifanya kazi na Katibu Mkuu mmoja, Philip Mangula.
Si hilo tu. Hata serikalini, ndani ya miaka minne, Rais Kikwete ameteua mawaziri wakuu wawili - Edward Lowassa na Mizengo Pinda.
Mtangulizi wake, Rais Mkapa, alifanya kazi na Waziri Mkuu mmoja tu, Frederick Sumaye - kwa miaka 10.
Maana yake nini? Baadhi yetu tunaona kwamba Rais Kikwete bado anafanya ‘mazoezi’ ya kuunda serikali.
Ni zaidi ya
hapo. Hata kwa kutazama tu utendaji wa viongozi anaowateua serikalini na
katika chama, ni dhahiri kwamba miongoni mwa vielelezo vya udhaifu wa
Rais Kikwete ni uteuzi wa wasaidizi wake.
Na wakati
mwingine baadhi yetu tunadhani kwamba inawezekana Rais Kikwete anateua
viongozi dhaifu kwa kuogopa ‘kufunikwa’ na viongozi mahiri.
Tunakumbuka,
kwa mfano, jinsi mzozo wa kimadaraka kati yake na swaiba wake wa
zamani, Edward Lowassa, ulianza kufukuta chini chini baada ya yeye na
‘watu wake’ kugundua kwamba Lowassa alikuwa ‘anamfunika’ bosi wake
katika utendaji wa masuala mazito.
Lakini hilo
lilikuwa tatizo la bosi, kwa kuwa utendaji mzuri wa mdogo wake ulikuwa
unajenga sifa ya serikali nzima, hasa mkuu wa serikali mwenyewe.
Na katika
mazingira ya utendaji yasiyomtegemea mtu mmoja pekee, kiongozi mkuu
anayejizungushia watendaji na wasaidizi dhaifu anakuwa anapalilia na
kustawisha udhaifu wake mwenyewe.
Kwa kutazama
na kulinganisha utendaji wa Mkapa na Kikwete, hasa katika suala la
uteuzi ndani ya chama na serikali, Watanzania wanajua nani mahiri, na
nani dhaifu, kati ya viongozi hawa wawili.
Kwa maana
hiyo, ‘ulegelege’ wa Serikali katika masuala mazito na unyonge wa sasa
wa CCM, ni matokeo ya uteuzi na usimamizi mbovu.
Na hili
limedhihirishwa na ukweli kwamba katika fursa zote alizopata za kuunda
serikali upya, au kukipanga chama upya, Rais Kikwete hawezi kujisifu
kwamba amezitumia vizuri.
Kwa upande
wa chama, tunapotazama hili la uchaguzi ndani ya chama uliomalizika -
ambao kwa mara ya kwanza umeingiza mke wa rais na mtoto wake katika
baadhi ya vikao vikubwa vya maamuzi - tunaona dhamira ya rais na familia
yake kujaribu ‘kuteka’ chama chao kwa masilahi wanayojua wao.
Lakini
hitimisho la uchaguzi wao, na jinsi rais alivyounda upya sekretarieti ya
CCM, umekuwa ushahidi mwingine wa kushindwa kwake kukibadilisha chama
kuelekea matamanio yao ya kung'ang'ania madaraka.
Katika
sekretarieti hii ya Kinana, Zakia Meghji, Nape Nnauye, Mohamed Seif
Khatib, Asha-Rose Migiro, Mwigulu Nchemba, na Vuai Vuai; CCM itakuwa
inajipa sifa za kijinga kuamini inapiga hatua kubwa kwenda mbele.
Na kwa jinsi
historia ya utawala wa Rais Kikwete ilivyo hadi sasa, baadhi yetu
hatuamini kama hii ndiyo sekretarieti yake ya mwisho kabla hajaondoka
madarakani.
Hata Philip
Mangula katika nafasi ya makamu mwenyekiti, hatarajiwi kuleta jipya
katika CCM ya sasa iliyomong'onyoka, na inayoathiriwa na magonjwa sugu
niliyotaja kwenye uchambuzi wangu wiki kama tatu zilizopita.
Kama ambavyo
JK alimwingiza Pius Msekwa ili kujipatanisha naye baada ya kumfanyia
faulo za kumnyang'anya uspika mwaka 2005, ndiyo alivyomwingiza Mangula
sasa kama njia ya kupoza machungu aliyomsababishia tangu wakati wa
mchakato wa kugombea urais mwaka 2005.
Na kama
ambavyo uteuzi wa Msekwa kuwa makamu mwenyekiti uliirudisha CCM nyuma
miaka 35, ndivyo uteuzi wa Mangula, Kinana, Meghji, Khatib na wengine
utakavyopunguza au kuondoa kasi ya chama hicho kukua.
Hata
wanaosifu historia binafsi za wateule wapya wa rais, kama ninavyoona
baadhi yao wakimsifia Kinana, ingekuwa vema wakajikumbusha mbwembwe
zilizomwingiza Wilson Mukama katika nafasi hiyo.
Ameacha urithi gani? Sasa hivi, ingawa ndio wameteuliwa, tunapaswa kuanza kujiuliza, “nani anakuja baada ya Kinana?”
Na licha ya
utendaji wa Mangula huko nyuma, nafasi aliyopewa sasa haimfanyi kuwa
mtendaji. Na katika mazingira ambamo bosi wake ni Kikwete, tusitarajie
lolote la maana kutoka kwake.
Zaidi ya
hayo, Kama CCM imekosa mbadala wa Mangula, Kinana, Meghji na Seif Khatib
katika zama na changamoto tulizomo, ni ushahidi mwingine kwamba chama
hicho kinaelekea makaburini.
Na
Watanzania watamshukuru Rais Kikwete kwa kuwasaidia kuharakisha kifo cha
chama alichodhamiria kukiua mwaka 2005 kama kisingemteua kuwa mgombea
urais. Na kwanini kisife?
Chanzo:CHADEMA Blog
Imeandikwa na Ansbert Ngurumo
Post a Comment