Viongozi
akiwemo Mhe. Majaliwa wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa
Tanzania na Mjumbe kutoka Chiyoda kuashiria Makubaliano kati ya Tanzania
na Shirika la Chiyoda ambalo litashirikiana na Tanzania katika kutoa
mafunzo kwa Wahandisi kwenye masuala ya gesi na mafuta. Waliosimama
kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof.
James Mdoe; Bw. Francis Mossongo, Afisa Mwandamizi wa Dawati la Japan,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mkurugenzi
wa Shirika la Chiyoda. ============================================
Tanzania
kushirikiana na Japan katika mafunzo kwa Wahandisi
Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameshiriki hafla
iliyoashiria kusainiwa kwa makubaliano kati ya baadhi ya nchi za Afrika na
Makampuni mbalimbali ya Japan iliyofanyika wakati wa Mkutano TICAD VI jijini
Nairobi.
Hafla hiyo ambayo
ilitanguliwa na Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan ilihusisha nchi
20 za Afrika ambazo zimeingia makubaliano ya kuimarisha uwekezaji na biashara
na Makampuni makubwa 22 ya Japan.
Kwa upande wa
Tanzania, Serikali imeingia Makubaliano na Shirika la CHIYODA kwa ajili ya kuwajengea
uwezo Wahandisi wa Tanzania kwa kuwapitia mafunzo kwenye masuala ya teknolojia
ya gesi na mafuta.
Akizungumza wakati wa
Kongamano hilo Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta alisema kuwa
Kongamano hilo ni jukwaa muafaka wakati Afrika ikiwa katika jitihada za mageuzi
ya kiuchumi. Hivyo aliziomba nchi za Afrika kutumia ujuzi na uzoefu mkubwa wa
Japan katika kuiimarisha Sekta Binafsi ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia
maendeleo.
Aidha, aliongeza kuwa
Kenya ikiwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea
kushirikiana na nchi wanachama wenzake kuhakikisha kunakuwepo mazingira mazuri
ya kuvutia wawekezaji kutoka nje hususan Japan. Pia aliishukuru Serikali ya
Japan kwa ushirikiano mkubwa inaotoa kwa Afrika na kukaribisha uwekazaji kutoka
sekta binafsi ya Japan kwenye maeneo ya uzalishaji wa nishati ya umeme na
maeneo mengine.
Kwa upande wake,
Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe alisema kuwa Japan itaendelea kushirkiana
na Afrika katika kuhakikisha inapiga hatua zaidi ya maendeleo. Aliongeza kuwa
kwa kutambua umuhimu wa ushirikiano kati ya Afrika na Japan Kampuni 22 na Vyuo Vikuu vya Japan zimefuatana
nae ili kukamilisha mikataba 73 na nchi za Afrika.
Aidha, alieleza kuwa Kampuni za Japan zimetumia fursa
ya Mkutano wa TICAD VI kutangaza Azimio
la Biashara ikiwa ni katika kuelezea nia na madhumuni yao katika kuchangia
maendeleo ya Afrika.
Mbali na Tanzania
nchi zingine za Afrika zilizoingia Makubaliano na Kampuni na Mashrika kutoka
Japan ni pamoja na Kenya, Angola, Cameroon, Congo, Cote d’ Ivoire, DRC,
Ethiopia, Misri, Ghana, Madagascar, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria,
Rwanda, Seychelles, Afrika Kusini, Uganda na Zambia.
Wakati huohuo,
Mkutano wa Sita wa Kilele wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya
Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD
VI) umemalizika Jijini Nairobi leo huku
Wakuu wa Nchi na Serikali wakipitisha kwa kauli moja Azimio la Nairobi na
Mpango Kazi wa utekelezaji wake.
Azimio la Nairobi pamoja
na mambo mengine linalenga katika kutekeleza mambo makuu matatu ambayo ni:
Kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchumi ili kuwa na vyanzo mbadala vya kuendesha
uchumi huku mkazo ukiwekwa kwenye uanzishwaji wa viwanda vitakavyozalisha ajira
kwa wingi kwa vijana wa Afria; Kujenga mifumo ya Huduma za Afya ambazo ni
endelevu kwa maisha bora ikiwemo kuboresha huduma za afya, kuweka mikakati ya
kukabiliana na magonjwa kama Ebola, kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto
na jamii nzima; na Kukuza na kuimarisha Utulivu na Ustawi wa Jamii.
Mbali na Mkutano wa
Kilele wa TICAD VI, shughuli zingine zilizoenda sambamba na mkutano huo ni
Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan; Maonesho ya Biashara ya Afrika
na Japan; na Mkutano wa Majadilino ya Kibiashara kati ya Viongozi Wakuu wa Serikali
na Wakurugenzi Wakuu wa Makampuni Binafsi.
Mkutano
wa TICAD VI
ambao ulihudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali zaidi ya 30 kutoka
Afrika, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda pia uliyashirikisha
Makampuni zaidi ya 100 kutoka Serikali ya Japan, Sekta Binafsi na
kuhudhuriwa na zaidi ya Wajumbe 10,000
kutoka sehemu mbalimbali duniani.
-Mwisho-
|
Post a Comment