NYIMBO NAYE ADAI MANGULA ANASHINDANA NA KIVULI
SIKU chache
baada ya Makamu Mwenyekiti mpya wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa,
Philip Mangula, kujibu mapigo ya wapinzani wake akisema wanaombeza
wanasahau historia yake, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa,
amemtaka aweke mikakati hiyo katika vitendo.
Dk. Slaa
alidai kuwa kwa sasa Watanzania wamechoka kusikiliza historia, hivyo
kama Mangula ana uthubutu aanze kusafisha chama chake kwa kuwaondoa
watuhumiwa magwiji wa ufisadi kabla ya kuhangaika na wale waliotoa
rushwa kwenye uchaguzi wao.
Wakati Dk.
Slaa akitoa somo hilo kwa Mangula, naye mwanasiasa mkongwe nchini,
Thomas Nyimbo, amemvaa kigogo huyo wa CCM akisema kuwa ni kama
anashindana na kivuli chake kwa kujidanganya kuwa ataitokomeza rushwa
ndani ya chama hicho.
Kauli hizo
zinakuja siku chache baada ya Mangula kakaririwa na vyombo vya habari
akitamba kuwa wanaombeza kuwa hawezi kuitokomeza rushwa CCM wanasahau
rekodi yake akiwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Mangula bila
kumung’unya maneno aliwataja wafanyabiashara Yusuf Manji na Thomas
Nyimbo kuwa ni miongoni mwa watu aliowafutia ushindi wasigombee ubunge
baada ya kubainika kujihusisha na rushwa katika kura za maoni mwaka
2000.
Mwanasiasa
huyo pia alikumbushia jinsi chama kilivyofuta matokeo ya baadhi ya
washindi katika majibo 32 na kuamuru uchaguzi urudiwe baada ya kubaini
uwepo wa mizengwe ya rushwa, hivyo akaahidi kuwa wanaombeza wangoje
waone ndani ya miezi sita atakavyochukua hatua.
Hata hivyo,
katika mahojiano yake na gazeti hili jana, Dk. Slaa aliendelea kumbeza
Mangula akisema kama anajisifu kuwa anaweza kuondoa wala rushwa katika
CCM, basi aanze na watuhimiwa sugu walioshindikana kung’oka kwenye
falsafa ya kujivua gamba.
Alisisitiza
kuwa anamshangaa Mangula kwa kujisifu kwa jambo hilo, na kwamba kama
kweli anaweza basi atekeleze sera ya kujivua magamba iliyomshinda
mtangulizi wake Pius Msekwa na Wilson Mukama.
Alisema kuwa
watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho ambao wametajwa hadi na
wana-CCM wenyewe bado wapo na wanaendelea vema na kazi za kila siku.
“Hivyo kama
Mangula ana ubavu aanze na hawa aache kujisifia historia, mambo
anayoyataja kwanza Watanzania wengi hawayajui, wanataka kuona sasa,”
alisema.
Nyimbo ajibu mapigo
Akizungumza
na Tanzania Daima kwa simu jana, Nyimbo alisema kitendo cha Mangula
kumzungumzia mtu binafsi katika tatizo linalohitaji marekebisho ya mfumo
mzima ni suala la kushangaza na kuonyesha kushindwa mapema.
“Mangula
amepewa nafasi, sasa kama atasema hawezi kutokomeza rushwa japo suala
hilo ni la kihistoria unafikiri wanachama wake watamuelewa, si
watamshangaa?” alihoji.
Nyimbo
aliongeza kuwa historia ya rushwa ilikuwepo hata kwa manabii na kueleza
kwamba kinachoweza kufanyika ni kupunguza tatizo kwa kuhakikisha
wananchi hawaathiriwi kwa kiasi kikubwa.
Kuhusu
kuenguliwa kugombea ubunge ndani ya CCM kwa tuhuma za rushwa, kada huyo
ambaye aliwahi kuhamia CHADEMA na kujitoa hivi karibuni na kubakia
mwanasiasa huru, Mangula alimtaka Mangula kuwa mkweli juu ya hilo.
“Nyimbo ni
mwanasiasa mwenye historia yenye kutukuka katika Tanzania huwezi
ukanikuta katika kashfa yoyote; sasa huyo ndugu yangu anaposema
aliniengua wakati huo alikuwa kiongozi wa wapi?”
TANZANIA DAIMA
Post a Comment