Na. Zawadi Msalla- MAELEZO 20/11/2012, Arusha.
Rais
Jakaya Kikwete ameiasa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi Kusini mwa Afrika
(SADC) kuimarisha ushirikiano kati yake na nchi wanachama wa Jumuiya
hiyo ili kufanikisha utekelezaji wa Mkakati wa pili wa kushughulikia
masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya hiyo.
Rais Kikwete ameeleza hayo wakati akizindua Mkakati wa kushughulikia
masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya hiyo (SIPO II) jijini
Arusha wakati wa mkutano uliowahusisha wawakilishi mbalimbali kutoka
katika Jumuiya wanachama wa SADC.
Amesema ili malengo ya Mkakati huo yaweze kufanikiwa ni lazima
ushirikiano wa ndani na nje wa nchi hizo wanachama uimarishwe na
kuongeza kuwa SADC haiwezi Kutegemea mikakati ya ndani ya ulinzi na
Usalama ya nchi fulani kutaka kutekeleza mkakati wake.
"SADC
haitakiwi kuiingilia kwa kutaka kuibadili mikakati ya ndani ya Nchi
wanachama ya ulinzi na usalama badala yake washirikiane kwa karibu
kuangalia nini cha kufanya" Amesema Rais.
Kuhusu
umuhimu wa mkakati huo Rais Kikwete amesema utakuwa muongozo wa
SADC katika masuala yote ya ulinzi, usalama na siasa, na umejikita
katika kutatua vikwazo mbalimbali vya kiulinzi vilivyopo.
Amefafanua
kuwa Utekelezaji wa SIPO na maazimio yake utapelekea hali ya amani na
utawala bora kwa Nchi nyingi za Afrika na kuongeza kuwa katika awamu ya
pili ya SIPO mabadiliko mengi yamefanyika yakiwemo uongezaji wa
vipaumbele katika mfumo wa utekelezaji na ufuatiliaji wa masuala ya
ulinzi na usalama.
Uzinduzi
wa SIPO II utaangalia ushirikiano kati ya Nchi wanachama, ushirikiano
katika masuala ya kibiashara, uhakika wa kushughulikia masuala ya
upatikanaji wa Amani na ushirikiano katika nyanja ya habari.
Akieleza
historia ya chombo cha Usalama cha SADC alisema kabla ya kuanzishwa
kwa chombo hicho kulikuwa na ushirikiano wa nchi katika masuala ya
ulinzi na usalama na kubainisha kuwa kuanzishwa kwa SIPO kunatokana na
nchi wanachama kuona umuhimu wa kuwa na chombo kinacho waongoza katika
masuala hayo yote.
Awali
akizungumza na wajumbe wa mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe amesema kuwa SIPO imekuwa ni
nyenzo muhimu nay a kutegemewa na nchi za SADC katika masuala yote ya
usalama.
Amesema
SIPO ilizinduliwa rasmi mwaka 2004 na baadae kufanyiwa marekebisho ya
kimsingi mwaka 2007 na kueleza kuwa kutokana na marekebisho hayo ya
Mwaka 2007 ilikubaliwa kuwa mikakati na vapaumbele vya SIPO iwe
inapitiwa kila baada ya miaka mitano.
Aidha uzinduzi huo utafuatiwa na mafunzo mbalimbali yatakayoendeshwa na wataalamu kwa muda wa siku nne.
Post a Comment