Wakili Alex Mgongolwa
SHIRIKISHO
la Soka Tanzania (TFF), limesema kwamba Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa shirikisho
hilo utafanyika Februari 16 na 17 mwakani, badala ya Desemba mwaka huu kufuatia
Kamati ya Utendaji kuafiki mapendekezo ya marekebisho ya Katiba katika kikao
chake cha Novemba 3, mwaka huu 2012.
Taarifa iliyotumwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
ya TFF, Wakili Alex Mgongolwa imesema kwamba baada ya kutafakari mapendekezo
hayo, Kamati ya Utendaji ya TFF imeamua kuifanyia marekebisho Katiba ya shirikisho
hilo kama iliyopendekezwa.
“Kwa vile
mapendekezo mawili kati ya matatu ya ya marekebisho ya Katiba yana uhusiano na
Uchaguzi Mkuu wa TFF, ipo haja ya marekebisho hayo kufanyika kabla ya
kutangazwa kwa Mkutano Mkuu wa TFF na kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa
TFF,”imesema taarifa ya Mgongolwa.
Aidha, Mgongolwa
amesema kwa vile TFF haina uwezo wa kuitisha mikutano mikuu miwili – Mkutano
Mkuu Maalum kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ya TFF; na Mkutano Mkuu wa
Uchaguzi – katika kipindi kifupi kijacho, marekebisho ya Katiba yafanywe kwa
njia ya Waraka (“Circular Resolution”).
“Waraka huo
(“Circular Resolution”) uwe umeshatayarishwa na Sekretariati ikishirikiana na
Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ifikapo tarehe 15 Novemba 2012 na ukabidhiwe kwa
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanaowakilisha Kanda za TFF ambao watahakikisha
kuwa kila Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa
Kanda husika anapata fursa ya kutoa ridhaa yake,”imesema taarifra ya Mgongolwa.
Aidha,
wakili huyo ameagiza zoezi la kupata ridhaa ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu liwe
limemalizika katika kipindi cha siku 21 na kwamba kikao kinachofuata cha Kamati
ya Utendaji Desemba 15, mwaka huu kiwe kwa madhumuni ya kupokea taarifa ya
zoezi hili na kufanya matayarisho ya Mkutano Mkuu.
“Katiba ya
TFF inaelekeza kuwa taarifa ya Mkutano Mkuu itolewe kwa wanachama wake angalau siku
60 (“notice period”) kabla ya Mkutano. Hivyo Kamati ya utendaji inatarajia kuwa
Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utafanyika Jumamosi na Jumapili ya tarehe 16 na 17 na
Februari 2013,”.
Amesema Kamati
ya Utendaji ya TFF inasisitiza kuwa utaratibu huo umeamuliwa kutokana na TFF
kutokuwa na uwezo wa kifedha wa kutayarisha mikutano mikuu miwili katika
kipindi kifupi kijacho na kwamba kinyume chake ni kuchelewa zaidi kufanyika kwa
Mkutano Mkuu, jambo ambalo hawana budi kuliepuka.
Amesema Kamati
ya Utendaji ya TFF inatarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa Wajumbe
wa Mkutano Mkuu wa TFF na wadau wa soka kwa jumla ili kufanikisha zoezi hilo na
hatimaye kufanikisha Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa TFF.
Katika kikao
chake cha Novemba 3, mwaka huu, Kamati ya Utendaji ya TFF ilipokea taarifa ya
mapendekezo ya marekebisho ya Katiba ikitakiwa kuongeza kipengele kinachohusu
“Club Lincencing” kama ilivyoagizwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika
waraka wake unaowataka wanachama wote wa CAF, ikiwemo TFF, kuhakikisha kuwa
kipengele hicho kinaingizwa katika katiba zao.
Kutokana na
ushauri na maagizo ya FIFA, TFF inatakiwa kuunda wa Kamati ya Rufaa ya
Uchanguzi (“Elections Appeals Committee”) na kuondokana na utaratibu iliyonao
hivi sasa, ambao Kamati ya Rufaa (“Appeals Committee”) inajigeuza na kuwa
Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wakati wa mchakato wa uchaguzi wa TFF.
Pendekezo lingine
ni kuindoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF pamoja na kutamka kuwa
Wawakilishi wa klabu za Ligi Kuu katika Kamati ya Utendaji watachaguliwa moja
kwa moja na klabu zenyewe.
Hiyo
inatokana na azimio la Mkutano Mkuu uliopita la kuruhusu uundwaji wa chombo
huru cha kusimamia Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza pamoja na kupitishwa kwa
Kanuni zinazokiongoza chombo hicho kama zilivyopendekezwa na klabu za Ligi Kuu
na kupitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF.
Habari Na Mahmoud Zubeiry
Post a Comment