Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

CCM YABUNI MBINU MPYA

 
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuanzia sasa, kitawashughulikia watendaji wa Serikali wanaoitwa katika vikao mbalimbali vya chama hicho, kuelezea utekelezaji wa ilani ya chama hicho, lakini wanagoma kuhudhuria na wakati mwingine kuamua kutuma wasaidizi wao.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Taifa, Nape Nnauye, wakati akifungua semina ya Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Nyamagana, Mkoa wa Mwanza.


Alisema kwamba, baadhi ya watendaji hao wamegeuka kuwa miungu watu katika sehemu zao za kazi na wamekuwa wakikaidi kuitikia wito wanapoitwa na viongozi wa chama katika ngazi za utawala.

“Kama kuna mtendaji ambaye anakichukia chama kinachounda Serikali anayoitumikia kisa tu chama kinafuatilia utekelezaji wa ilani yake, anapaswa kutupisha.

“Kwa hili hatutanii, tutamtimua kazi mara moja na nyie viongozi wa CCM mnapaswa kumjadili katika vikao vyenu na pale mtakapotuletea kuwa kiongozi fulani ni mzigo kwa chama, hatutaweza kuchukua zaidi ya dakika tatu kubariki uamuzi wa vikao vyenu ili iwe fundisho kwa watendaji.

“Wakati wa uchaguzi tumekuwa tukikesha kusaka kura ili CCM iweze kuunda Serikali, lakini watendaji wabovu wamekuwa wakitukwamisha na wananchi kuichukia Serikali. Hivyo basi, tutawashughulikia viongozi ambao wamekuwa wakishindwa kufika katika vikao vya chama kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa utekelezaji wa ilani ya chama chetu,” alisema Nape.

Kauli hiyo ya Nape ilikuja baada ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, kuchukizwa na vitendo vya baadhi ya viongozi wa taasisi za Serikali zilizopo mkoani hapa, kushindwa kufika katika kikao hicho licha ya kupewa mwaliko maalumu.

Konisaga alisema kwamba, baadhi ya watendaji wanapaswa kuchukuliwa hatua kutokana na dharau walizonazo dhidi ya chama tawala na kwamba ndiyo wanaosababisha CCM kuchukiwa na wananchi.

“Katika hili lazima nichukue hatua kwa sababu hapa kuna baadhi ya watendaji, ambao hawakufika katika kikao na kufika kwao kungesaidia kutatua kero za wananchi.

“Kwa hiyo basi, naagiza wale ambao hawakufika, waripoti ofisini kwangu Jumanne (kesho) saa nne asubuhi na nyie viongozi wa juu wa chama tukiwaletea taarifa za uamuzi wa vikao vyetu, kwamba huyo hafai, tafadhali muondoeni kwa kuwa chama hakitaweza kushinda kama ataendelea kuwepo,” alisema Konisaga.

Chanzo:Mtanzania
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top