Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

CCM YAWATOSA WALIOFUNGUA KESI KUPINGA MATOKEO


 na Josephat Isango

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewageuka wanachama wake waliotumwa kufungua kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo mbalimbali nchini, Tanzania Daima Jumapili limebaini.


Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa waliofungua kesi kupinga ubunge wa Godbless Lema mkoani Arusha, wametoswa na sasa wanakusudia kumwangukia mbunge huyo kumwomba radhi ili awasamehe deni la uendeshaji wa kesi tangu mwanzo hadi juzi Mahakama ya Rufaa ilipomrejeshea ubunge.


Baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, CCM kupitia Katibu Mkuu wake, kwa wakati huo, Yusuf Makamba, iliandika barua yenye kumbukumbu namba CCM/OND/636/VOL.11/122 ya Novemba 9, 2010 kwenda kwa makatibu wake wa mikoa na wilaya kuwaamuru wote walioshindwa katika uchaguzi wapinge matokeo, na kwamba chama kingewasaidia gharama za uendeshaji wa kesi hizo.


Katika barua hiyo, Makamba aliwataka wagombea wa ubunge kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, huku wagombea udiwani walioangushwa kufungua kesi katika mahakama za mahakimu wakazi ndani ya siku 30, tangu ulipofanyika uchaguzi huo.


Katika barua hiyo ambayo Tanzania Daima Jumapili ina nakala yake, Makamba aliwaagiza makatibu wa CCM wa mikoa kwa kushirikiana na makatibu wa wilaya na kata kuwasaidia wagombea walioshindwa kwenye uchaguzi kuandaa hoja za malalamiko na vielelezo kwa ajili ya kupeleka mahakamani, huku akisisitiza kuwa “Chama Cha Mapinduzi Makao Makuu kitachangia gharama za mawakili kwa wagombea ambao hawana uwezo kifedha.”


Baadhi ya wabunge wa upinzani walioshitakiwa na kesi zao kuhukumiwa na kuibuka kidedea, hawajalipwa gharama za uendeshaji wa kesi hizo.


Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (CHADEMA) kupitia kwa wakili wake, Benjamin Mwakagamba wa Kampuni ya uwakili ya BM ya jijini Dar es Salaam, alisema kuwa, mdaiwa katika kesi hiyo, Dk. Lucas Siame (CCM) tangu aamriwe na mahakama kulipa, amekuwa haonekani mahakamani au kuonesha dalili zozote za kulipa gharama za uendeshaji wa kesi.


Wakili huyo anasema kuwa, mdaiwa huyo ambaye alipinga matokeo, amekuwa akiishi kwa kujificha maeneno ya Sinza, jijini Dar es Salaam.


Tanzania Daima Jumapili lilimtafuta Dk. Siyame kupitia simu yake ya mkononi akapatikana, ila alisema hajui utaratibu kama alipaswa kulipa au la.


“Mwandishi hizo habari za kulipa ndio nazisikia kwako,” alisema lakini alikiri kuwa CCM haikumsaidia uendeshaji wa kesi aliyofungua dhidi ya Silinde.


Silinde, alishinda kesi katika Mahakama Kuu ya Rufaa Kanda ya Mbeya, baada ya kufuta shauri la kesi ya rufaa iliyopelekwa na Siame, aliyekuwa mgombea wa CCM, Mei 2, mwaka huu.


Siame aliyekuwa amekata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa Julai mosi, mwaka jana dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliompa ushindi mbunge huyo wa CHADEMA, alilazimika kuomba mahakama kuondoa shauri hilo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (CHADEMA) ambaye naye alishinda kesi ya pingamizi iliyofunguliwa na Benson Mpesya (CCM), alipoulizwa endapo amelipwa fidia kama ilivyoamriwa na mahakama, alisema kuwa amelipwa sehemu ya fedha, na nyingine bado.


Sugu alisema kuwa, hata hivyo Mpesya amekuwa akimtuma wakili wake kuonana na wa kwake ili angalau amwongezee muda wa kulipa.


“Nimekuwa mstaarabu sana, ningeweza kutafuta amri ya mahakama ili mali zake zikamatwe, lakini alimtuma wakili wake nimvumilie,” alisema Mbilinyi.


Wakati mzigo wa kulipa gharama ukiwaangukia wafungua kesi, waliomshtaki Mbunge wa Singida Mjini, Tundu Lissu (CHADEMA) wanatafuta suluhu.


Walalamikaji wawili waliokata rufaa dhidi ya Lissu, ambao kesi yao bado haijaanza kusikilizwa, tayari wameshaanza kumtafuta mbunge huyo ili wafanye utaratibu wa kuondoa kesi Mahakama ya Rufaa.



Akizungumza kwa simu kutoka Muyanji-Makiungu, Singida, mlalamikaji wa kwanza katika kesi hiyo, Shabani Selema alisema: “Natamani sana kuiondoa kesi hiyo mahakamani ambayo Chama chetu Cha Mapinduzi kilishinikiza tukate rufaa, lakini kwa sasa chama hakieleweki, sina haja tena na hiyo kesi, sitaki na ninataka kwenda Dodoma nionane na wakili wetu angalau nichukue hata kitambulisho changu cha mpiga kura kwani kilikuwa ni sehemu ya vielelezo, mimi nakuahidi kuwa nakuja Dar es Salaam wakati wowote na nitamtafuta Lissu tukafute hiyo kesi.”


Alipohojiwa inakuwaje ajitoe katika hatua hii ya rufaa, Selema alijibu: “Mwandishi kama kuandika andika tu, mimi hii kesi sina hamu nayo, nimekuwa naiendesha mwenyewe, hata familia yangu, rafiki zangu na wasomi mbalimbali sasa wananishangaa, chama kimeniacha, kwanza wamenivuruga sana.”


Kwa upande wake, Lissu alisema taarifa kwamba mlalamikaji wake anamtafuta ili wafute kesi, amezisikia kutoka kwa wanafamilia yake.


Tanzania Daima Jumapili iliwatafuta viongozi wa CCM Makao Makuu kuzungumzia suala hilo, lakini simu zao hazikuweza kupatikana hewani huku simu ya Naibu Katibu Mkuu bara, ikiita muda wote bila kupokelewa.


Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda alipopigiwa simu hakuweza kupokea, lakini baadaye alimpigia mwandishi na kumuuliza: “wewe nani?”


Mwandishi alipojitambulisha kwamba anatoka Tanzania Daima Jumapili, Chatanda alisema: “Kama wewe ni wa Tanzania Daima, nipigie sina haja ya kukupigia.”


Baada ya kusema hayo akakata simu, na alipopigiwa tena, simu ilikuwa tayari imefungwa - haikupatikana tena.

NA TANZANIA DAIMA
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top