Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

KRISIMAS INAPOSHEHEKEWA NA WATANZANIA MILIONI SABA TU




 
Na: Maggid Mjengwa,

Ndugu zangu,

Mwaka 1950 nchi yetu ilikuwa na idadi ya Watanzania wapatao milioni saba. Ni kwa mujibu wa takwimu za kisayansi. Takwimu hizo zinabainisha, ifikapo mwaka 2050, nchi yetu itakuwa na Watanzania wapatao milioni mia moja. Hii leo, idadi ya Watanzania inakadiriwa kuwa milioni arobaini na tano.

Tafsiri yake? Tukianza na hili la Krismas, tunaona, kuwa mwaka 1950 kulikuwa na idadi ya Watanzania milioni saba tu waliosheherekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Na hata sherehe nyingine za kidini zilisheherekewa na idadi hiyo ya Watanzania.

Maana kubwa ya taarifa hizo za kisayansi ni ukweli, kuwa, wakati huko nyuma ilisemwa, kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne; ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora, tunapaswa sasa kutafakari upya.

Kwamba tulidhani kuwa ardhi tunayo ya kutosha, hapana, huko tunakokwenda ardhi yetu itakuwa ndogo sana kwa idadi kubwa ya Watanzania watakaoongezeka. Hivyo basi, moja ya tishio la nchi kuendelea ni kukua kwa kasi kwa idadi ya watu bila kuwa na mipango thabiti ya kuhakikisha kuna udhibiti wa rasilimali za nchi na kuwaandaa watu wanaoongezeka kwenye misingi bora ya elimu na uhakika wa huduma muhimu kama vile afya.

Kwamba kikubwa kinachohitajika kukabiliana na changamoto za kuongezeka kwa idadi ya Watanzania miaka 50 ijayo ni kuwa na siasa safi na uongozi bora. Na hakika, siasa za ovyo ovyo huzaa uongozi wa ovyo ovyo, na uongozi wa ovyo ovyo ndio utakaopelekea Watanzania milioni mia moja watakaoishi miaka 50 ijayo waione nchi yao kuwa ni mahali pagumu zaidi pa kuishi.

Inahusu kuwa na siasa safi na uongozi bora utakaokuwa na uwezo wa kufanya maamuzi magumu ya kuhakikisha rasilimali za nchi hii ikiwamo ardhi zinalindwa. Kwamba zinalindwa kwa ari ya kizalendo ili Watanzania wa kesho na kesho kutwa wapate hakika ya uhai wao na maisha yenye staha kwenye nchi waliyozaliwa. Inahusu kuwa na mipango madhubuti ya baadae. Kuingalia Tanzania kwanza na si majina ya watu, na vyama vyao vya siasa ambavyo kimsingi ni vya kupita tu.

Na ili tuelewe hatari ya huko tunakokwenda, tuna lazima, na hasa kwa viongozi wetu, kuwa na uelewa wa hali halisi ya sasa kwa maisha ya Watanzania walio wengi.

Nitatoa mfano hai, majuzi hapa nikiwa njiani kwenda Iringa kutokea Bagamoyo nilisimama kwenye moja ya vitongoji vya Bagamoyo ili kununua embe dodo. Akina mama wale wakarimu walinipokea kama mwenzao. Bei ya dodo niliyotajiwa ilinifanya pia nitafakari sana, niingiwe na huzuni pia.

Maana, ni ukweli, kuwa mama yule anaanza kuzitafuta dodo zinakotoka, kisha anazipanga pale chini mchangani. Bei ya dodo kubwa kabisa ni shilingi mia sita!

Nilinunua dodo saba. Na hesabu ya dodo saba ikampa tabu sana mama yule. Akaniomba nimsaidie hesabu ya haraka. Nikamwambia ni shilingi 4,200. Kwenye noti ya elfu tano niliyompa alihitaji kunirudishia shilingi mia nane. Nikamwambia aitunze chenji hiyo.

Akashukuru , lakini, wakati akinifungia dodo zangu akaniongeza dodo mbili! Hivyo, kimsingi aliniongeza dodo za thamani ya shilingi 1, 200! Hivyo, ile mia nane niliyomwachia haikuwa na faida kwake. Unafanyaje?

Njiani niliwaza juu ya tunakokwenda kama nchi.Tujiulize; hivi rasilimali zetu za nchi ikiwamo madini, gesi na mafuta tunayoambiwa tunayo kwa wingi yatamsaidia vipi mama yule wa Bagamoyo mwuza embe dodo ambaye yumkini hajui kusoma, kuandika na kuhesabu?

Na idadi yao inazidi kuongezeka. Takwimu zinasema; asilimia 39 ya Watanzania milioni 45 hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Na hawa wanawaririthisha nini watoto wao?

Ukweli unabaki, kama Krismas ya mwaka 1950 ilisheherekewa na Watanzania milioni saba, na ya leo inasheherekewa na Watanzania milioni 45, basi, Krismasi ya mwaka 2050 itasheherekewa na Watanzania milioni mia moja. Na tujiulize le, je, Watanzania hawa wa mwaka 2050, ambao ni watoto na wajukuu zetu, watakuwa na cha kusheherekea?

Naam, kila kizazi na Jukumu Lake; Tafakari,Chukua Jukumu La Kizazi Chako. Heri ya Krismas!
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top