Waziri Mkuu wa Kenya na mgombea urais wa Muungano wa CORD, Raila Odinga
akimkaribisha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kushoto) kwenye
mkutano wa CORD uliofanyika juzi katika Viwanja vya Uhuru, jijini
Nairobi.
Na Mpiga Picha Wetu Hisani kubwa ya Mwananchi
,,,,,,,,,,,
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa
Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, alihudhuria mkutano wa kampeni wa Chama
cha Orange Democratic Movement (ODM) nchini Kenya kama chama rafiki kwa
mwaliko wa Raila Odinga.
CHADEMA ilifafanua kuwa Mbowe aliteuliwa na Kamati Kuu na wala hakutoa
kauli yoyote kwenye mkutano huo ya kuwashawishi Wakenya wamchague
Odinga kama alivyofanya Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, alipohudhuria
mkutano wa chama hicho Decemba 7 mwaka huu.
Magufuli akiwa amealikwa kibinafsi kama rafiki wa Odinga alitoa kauli
ya kumpigia debe kiongozi huyo akitaka Wakenya wamchague na kwamba
Watanzania wanamuunga mkono.
Hata hivyo kauli hiyo iliibua mtafaruku huku baadhi ya watu wakiwemo
CHADEMA wakihoji kama ilikuwa ya serikali na kumtaka Rais Jakaya Kikwete
atolee ufafanuzi, vinginevyo nchi ingekuwa na uhusiano mbaya na Kenya,
endapo Raila hatachaguliwa kuwa Rais.
Akizungumza na Tanzania Daima, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa
CHADEMA, John Mnyika, alisisitiza kuwa Mbowe alihudhuria kampeni za ODM
kwa niaba yao na kwamba alipewa baraka zote na Kamati Kuu.
Alisema hatua hiyo ni tofauti na ile ya Magufuli ambaye alialikwa
kibinafsi na Odinga halafu akatoa kauli tatanishi za kuhatarisha
uhusiano wa kidiplomasia bila kufafanua kama ni msimamo wake au
serikali.
“Kwetu ODM ni chama rafiki kama ilivyo kwa vyama kadhaa barani Afrika
na Ulaya. Mfano kwa Afrika vipo Democratic Turnhalle Aliance (DTA) cha
Namibia, RENAMO cha Msumbiji, New Patriotic Party cha Ghana na Forum for
Democratic Change cha Uganda.
“Kwa Ulaya vipo CDU kinachotawala nchini Ujerumani, KMT kinachotawala
China, DP kinachotawala Albania, Republican chama cha upinzani nchini
Marekani, Conservative cha Uingereza na Peoples Party cha Hispania,”
alisema.
Mnyika aliongeza kuwa hoja yao haikuwa Waziri Magufuli kuhudhuria
mkutano wa ODM ila kauli aliyoitoa ilikuwa ya kuweka shakani uhusiano wa
Kenya na Tanzania endapo kitashinda chama tofauti na ODM.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, aliongeza kuwa ndiyo maana
CHADEMA kupitia kwa Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, Ezekiel Wenje,
iliitaka serikali ifafanue kama ilimtuma-katumwa na chama chake cha CCM
au binafsi.
“Wenje alihoji kitendo cha Magufuli kupanda jukwaani kuanza kumnadi
kiongozi wa ODM kuwa ni ukiukwaji wa kanuni na taratibu za kimataifa
ambapo kwa mujibu wa kanuni hizo ni kosa kubwa taifa moja kuingilia
siasa za taifa jingine hata kama hayo mataifa yana ushirikiano,”
alisema.
Barua ya mwaliko wa Magufuli kutoka ODM ambayo Tanzania Daima imeiona
inaonyesha kuwa alialikwa kibinafsi, hivyo hakukuwa na sababu kuwasemea
Watanzania kama vile amebeba dhamana ya uwaziri katika mkutano ule.
NA TANZANIA DAIMA
NA TANZANIA DAIMA
Post a Comment