Na Othman Khamis Ame OMPR
Wakati neema ya mvua za vuli ikiendelea kunawiri katika maeneo mbali
mbali nchini ikileta faraja zaidi kwa wakulima na wafugaji kwa kupata
malisho ya Mifugo yao lakini kwa upande mwengine mvua hiyo hiyo
imeonekana kuleta hasara.

Sehemu ya jengo la Makumbusho ya Taifa la
Beit Al Ajaib ikionekana kunyofuka kutokana na mvua za vuli
zinazoendelea kunyesha Zanzibar.
Hasara hiyo inaonekana kuikumba Wizara ya Habari,Utamaduni, Utalii na
Michezo kufuatia Jengo lake Maarufu la Makumbusho ya Taifa la Beit Al-
Ajaib liliopo Forodhani Mjini Zanzibar kubomoka upande wa nyuma wa Jengo
hilo.
Kifusi kilichodondoka kutoka kwenye Dari ya Jengo hilo robo yake
kimeishia kwenye gari moja ndogo yenye nambari za usajili Z 897 DF
inayomilikiwa na Bwana Said Saleh Saidi Mkaazi wa Forodhani ambae
alikuwa ameiegesha pembezoni mwa Jengo hilo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifika mapema asubuhi
katika eneo hilo kuangalia tukio hilo baada ya kupata taarifa hiyo na
kuonyesha masikitiko yake kutokana na hasara hiyo kubwa.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk
alimueleza Balozi Seif kwamba Wizara hiyo ilikuwa ikiendelea na juhudi
za kulifanyia matengenezo Jengo hilo kwa kipindi kirefu sasa.
Waziri Mbarouk alifahamisha kwamba jitihada hizo zilikuwa zikienda
sambamba na matayarisho ya kutaka kuliezeka jengo hilokwa upande wa
nyuma.
Alieleza kwamba kutokana na tatizo hilo Wizara ya Habari inakusudia
kuwatumia Wataalamu wa Wizara yake kwa kukaa pamoja na Wahandisi wa
Idara ya Ujenzi Zanzibar kuangalia hatua za kuchukuwa ili tatizo hilo
lisije leta maafa.

Gari ndogo yenye nambari za usajili Z 897
DF ikionekana kuvurugika kabisa baada ya kifusi cha dari ya jengo la
Makumbusho ya Taifa la Beit al ajaib kuidondokea kufuatia mvua za vuli
zinazoendelea kunyesha Zanzibar.
Naye Mmiliki wa gari ndogo iliyoegeshwa pembezoni mwa Jengo hilo ambayo
imeharibika kabisa kutokana na tukio hilo Bwana Said Saleh Said alisema
alishuhudia mporomoko huo ukitokea muda mfupi baada ya kuegesha gari
yake.
Bwana Said alimueleza Balozi Seif kwamba Tukio hilo liliweza kuleta
mtafaruk na kusababisha hofu miongoni mwa wakaazi wa eneo hilo pamoja na
wale wafanyakazi wa Jengo hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa ZanzibarBalozi Seif Ali Iddi akimpa pole Bwana
Said kutokana na hasara iliyomkumba alimtaka kuendelea kuwa na subra na
kuamini kwamba hiyo ni mitihani ambayo inaweza kutokea na kumpata
kuimbe ye yote na wakati wowote ule.
Hata hivyo Balozi Seif aliwanasihi watu wanaomiliki vyombo vya moto
kuhakikisha kwamba wanakata bima ya vyombo vyao kwa lengo la kujinginga
na hasara wakati vyombo vyao vinapopatwa na ajali.
Jengo la Beit Al- Ajaib lililojengwa na Utawala wa Kijerumani Mwaka 1870
likiwa na umri wa karibu miaka 142 hutegemewa sana katika Sekta ya
Utalii ndani ya mwambao wa Afrika Mashariki pamoja na wataalamu na
wanafunzi wa kigeni wanaokuja kufanya utafiti hapa Nchini.
Chanzo ZanziNews
Post a Comment