Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

KIGOGO NCCR-MAGEUZI AHAMIA CHADEMA

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Lawrence Tara, amejivua uanachama wa chama hicho na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Tara ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bashnet, wilayani Babati,  Mkoa wa Manyara tangu mwaka 2000, alitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari jana, baada ya kupokewa Chadema na Mjumbe wa Kamati Kuu wa chama hicho, Godbless Lema.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na kiongozi mwingine wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, Ally Bananga.
Tara alitoa sababu mbili zilizomfanya aihame NCCR-Mageuzi na kujiunga na Chadema; upendeleo na dhuluma kwa watumishi wa chama hicho.
Alidai kwamba baadhi ya viongozi wa NCCR-Mageuzi wanaonyesha upendeleo wa wazi kwa kigezo cha urafiki kama kifanyavyo chama tawala, CCM.
Alisema yeye ni mmoja wa waathirika wa mfumo huo mbovu ndani ya NCCR- Mageuzi, baada ya chama hicho kumtelekeza katika kudai haki yake ya ubunge aliyodai kwamba iliporwa na CCM.
“Tunahitaji chama cha siasa kilicho makini na ambacho Watanzania tunapaswa kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja bila kutengana na kwa maoni yangu NCCR-Mageuzi siyo chama cha aina hiyo,” alisema Tara.
Akifafanua madai ya kudhulumiwa na CCM, Tara alidai kwamba alishinda ubunge wa Jimbo la Babati Vijijini, lakini akadhulumiwa.
Alisema katika mazingira hayo amebakiwa na chaguo mojawapo kati ya kubaki ndani ya chama kisichokerwa na hali hiyo na ambacho baadhi ya viongozi wake wanaendeleza upendeleo wa urafiki na undugu.
“Nikaona bora kujitenga na kuachana na chama chenye viongozi wa aina hiyo na kutafuta chama imara ambacho hakina simile na mambo kama hayo. Pia chenye kupigania haki, ukweli na ambacho kimepania utawala bora na ustawi wa Watanzania,” alisema.
“Ninaamini Chadema ni chama makini kilichopania kutokomeza dhuluma, uovu na ufisadi wa kidola na kuleta ustawi wa Tanzania,” alisema na kuwaomba wakazi wa Bashnet, Manyara na
Watanzania kumuunga mkono.
Akizungumza katika mkutano huo, Lema alimpongeza Tara na kusema chama hicho sasa kimeongezewa nguvu.
“Huyu ni sawa na Leonel Messi (mchezaji soka mahiri wa klabu ya Barcelona na Argentina). Sasa huwezi kumleta achezee AFC ya Arusha na Babati Stars halafu mpate mafanikio kutokana na mfumo uliopo, huyu anatakiwa awe Manchester United au timu nyingine kubwa,” alisema Lema.
Alisema viongozi wa chama chake badala ya kumpa ushirikiano ili aweze kushinda ubunge, Mwenyekiti wake alikubali kupewa ubunge wa kuteuliwa na Rais na hivyo Tara kuachwa mwenyewe.
“Uso umeumbwa na haya kuna vitu ukishakula huwezi kupinga. Hivyo jambo bora ni kuondoka huko na kwa hili nampongeza Tara kwa kuacha vyeo vyote ikiwemo posho za vikao vya udiwani na posho ya kila mwezi,” alisema Lema.
Alisema Tara anatarajiwa kupewa kadi ya chama hicho na Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe au Katibu Mkuu wake, Dk Wilbroad Slaa kwa kuwa yeye hawezi kufanya hivyo kutokana na nafasi kubwa aliyokuwa nayo mwanachama huyo mpya.
Chanzo:CHADEMA BLOG
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top