Na Majid Ahmed, Mogadishu
African Airlines, shirika la ndege linalomilikiwa na wafanyabiashara wa
Somalia, limeanza safari za ndani katika maeneo yaliyokombolewa kutoka
kwa al-Shabaab, likiwa ni la kwanza kwa kampuni kama hizo kutumia fursa
baada ya kuimarika kwa hali ya usalama.
Ndege ya Turkish Airlines ikiwa imekaa
kwenye barabara huko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Ade mjini
Mogadishu. Kampuni ya ndani Afrikan Airlines imeanza safari za ndege
katika maeneo yaliyokombolewa kutoka kwa al-Shabaab. [Na Mohamed
Abdiwahab/AFP]
"Safari za ndani za African Airlines zitawaruhusu watu kufikia maeneo
ambayo yalikuwa shida kuyafikia kupitia ardhini kutokana na ukosefu wa
usalama, barabara mbovu au masafa marefu," alisema Mohamed Jama wa bodi
ya wakurugenzi ya African Airlines.
"Shirika lilianza safari hizi za ndani hapo tarehe 4 Disemba baada ya
kupata vibali zinazotakikana na kukubaliwa na serikali ya Somalia pamoja
na Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia, ambao ndio wenye dhamana
ya usalama wa viwanja vya ndege katika miji iliyokombolewa" aliiambia
Sabahi.
Jama alisema kuwa kampuni ya African Airlines, ambayo mwanzo ilifanya
safari kwenda Somaliland na Puntland tu, sasa inazo safari tatu za ndani
kwa wiki kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Ade kuelkea miji
iliyokombolewa hivi karibuni ya Kismayu, Baidoa na Beledweyne.
"Karibuni, kutakuwa na ratiba ya safari kwenda miji mingine yote ya
Somalia ambayo ina viwanja vya ndege ambako ndege zinaweza kutua,"
alisema.
Mohamud Ahmed wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Somalia alisema kuwa
safari hizo mpya zinaashiria kuwa hali ya usalama nchini inaimarika.
"Hali ya usalama nchini imeimarika sana tangu vikosi vya washirika
kuichukua miji ya kimkakati ambayo ilikuwa katika udhibiti wa wanamgambo
wa al-Shabaab," aliiambia Sabahi. "Biashara imeinuka karibu nchini kote
na idadi ya Wasomali wanaorejea kutoka nje ili kuanzisha miradi ya
uwekezaji imeongezeka kwa sababu ya kurejea kwa utulivu katika sehemu
nyingi za nchi."
Kuinuka kwa uchumi wa ndani
Abdinur Osman, profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Green Hope mjini
Mogadishu, pia alisema kuwa kuanza upya kwa safari za ndani kwenda
maeneo yaliyokombolewa kati na kusini ya Somalia kumeinua uchumi wa
ndani.
"Safari hizi mpya za ndani zinachangia kuimarisha biashara na ukuaji wa
uchumi, pia kunaivutia wawekezaji wa Somalia na wa kigeni kushindana,"
aliiambia Sabahi.
Osman alitoa wito kwa serikali kuendeleza miundombinu ya viwanja vya
ndege vikongwe katika miji iliyokombolewa hivi karibuni, ambapo
isipokuwa uwanja wa ndege wa Mogadishu, viwanja vimechoka ma
havijafanyiwa ukarabati tangu kuanguka kwa serikali kuu," alisema. "Kwa
sababu hii, havikidhi viwango vya usalama vya kimataifa."
"Viwanja vya ndege ni njia [kuelekea duniani] na viwanja vikongwe vya
ndege vinahitaji sana kukarabatiwa na kuimarishwa ili kuhamasisha safari
nyingi zaidi na kuinua shughuli za biashara miongoni mwa mikoa kadhaa
ya Somalia," alisema. "Kuimarisha idadi ya safari za ndani ili kuenea
sehemu zote za Somalia kutasaidia kuunganisha miji ya Somalia na
kuwahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini."
Mfanyabiashara wa Mogadishu Abdifatah Abdullahi alikaribisha uimarikaji huo baada ya kushindwa mfululizo kwa al-Shabaab.
"Wakati wa utawala wa al-Shabaab kwa mikoa ya kusini, ilikuwa ni vigumu
kwa wafanyabiashara, maafisa wa serikali na viongozi wa kanda kufika
katika maeneo ambayo yako mbali na mji mkuu, Mogadishu, au kutembea
baina ya mikoa," aliiambia Sabahi. "Safari kwa kutumia barabara kutoka
Mogadishu hadi Beledweyne ilichukua kiasi cha siku mbili, wakati
kusafiri baina ya Mogadishu na Kismayu kunaweza kuchukua siku tatu hadi
nne kutokana na barabara mbaya na masafa marefu."
"Sasa, kila mtu ataweza kufikia kirahisi maeneo yote," alisema. "Pia
inapunguza muda unaotumiwa na wasafiri, kwa vile sasa wananchi wanaweza
kufungua kinywa wakiwa Mogadishu na kula chakula cha mchana huko
Kismayu, Beledweyne au Baidoa."
Abdullahi alisema kuwa waendesha biashara wa ndani kama vila Daallo
Airlines, Jubba Airways na African Express Airways walikuwa wakifanya
safari za ndani kwenda na kurudi kati na kusini ya Somalia, lakini
safari zilikatishwa kutokana na kudorora kwa hali ya usalama wakati
al-Shabaab ilipoichukua kusini ya Somalia miaka minne iliyopita.
Chanzo: sabahionline.com
Post a Comment