Lema akiongea na wananchi mara ya Kesi hiyo kuahirishwa jana.
Picha na Noise of Silence Blog.
na Happiness Katabazi;
ALIYEKUWA
Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbles Lema, amewasilisha sababu 18,
kuiomba Mahakama ya Rufaa nchini, itengue hukumu ya awali iliyotolewa na
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili mwaka huu ambayo ilifuta ubunge
wake.
Ombi hilo liliwasilishwa mahakamani hapo jana na mawakili
wa Lema, Method Kimomogoro na Tundu Lissu ambao walidai kuwa hukumu hiyo
iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalila haina hadhi ya kuitwa hukumu.
Mbele
ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa linaloongozwa na Jaji
Natharia Salum Massati, wakili Kimomogoro, alieleza mahakama kuwa rufaa
ya mteja wake ina jumla ya sababu 18 za kupinga hukumu iliyotolewa na
Jaji Rwakibalila.
Katika hukumu yake iliyoibua mjadala mkubwa
nchini Aprili mwaka huu, Jaji Rwakibalila alimtia hatiani Lema kwa
makosa ya kutoa lugha za kumkashifu mgombea mwenzie, Dk. Batilda Buriani
(CCM) na kumfungia kutogombea ubunge kwa kipindi cha miaka mitano
mfululizo.
Alidai kuwa, Jaji Rwakibalila alijielekeza vibaya
katika hukumu yake alivyosema kuwa kesi za uchaguzi hazitawaliwi na
kanuni za sheria za Uingereza kwani kuna maamuzi ya kesi mbalimbali
yaliyokwishatolewa na Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu nchini na
kuruhusu kesi za uchaguzi ziamuliwe kwa kutumia kanuni na sheria za
Uingereza.
Katika hoja ya pili, Kimomogoro alidai kuwa Jaji
Rwakibalila alijielekeza vibaya kuruhusu wajibu rufaa, wasitaje maneno
kwenye hati ya madai ambayo walidai ni maneno ya udhalilishaji wa
kijinsia na dini ambayo yanadaiwa kutolewa na Lema, kwenye mikutano ya
kampeni dhidi ya Dk. Burian.
Hoja nyingine ni kwamba hakuna
ushahidi wowote unaoonyesha kwamba wajibu rufaa kama kweli
waliandikishwa kupiga kura katika Jimbo la Arusha Mjini mwaka 2010 au
la.
Kwa mujibu wa wakili huyo, hoja nyingine ni kwamba Jaji
Rwakibalila alikosea kisheria kusema kuwa mtu yeyote akiwemo mpiga kura
ana haki ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo ambalo
yeye ni mpiga kura na kuongeza kuwa, wao wanaomba Mahakama ya Rufaa
itamke kuwa wajibu rufaa (wapiga kura wa Jimbo la Arusha waliofungua
kesi ile), hawana haki kisheria kufungua kesi ile ya kupinga ubunge wa
Lema kwani mwenye haki ya kufanya hivyo ni Dk. Batilda mwenyewe.
Aliongeza kuwa, mpiga kura yeyote hana haki ya kufungua kesi ya kupinga ubunge wa Arusha Mjini kwani haki zao hazikuvunjwa.
Aidha,
katika hoja nyingine alidai kuwa Jaji Rwakibalila hakutumia maamuzi ya
kesi za Mahakama ya Rufaa wala vifungu vya sheria ambavyo mawakili wa
pande zote mbili waliziwasilisha mbele yake katika majumuisho yao ya
mwisho.
Alidai kuwa, maamuzi ya Mahakama ya Rufaa katika kesi
zile yalisisitiza kuwa lazima kesi ithibitishwe bila kuacha mashaka
yoyote, lakini katika hukumu ya Lema, Jaji Rwakibalila imeacha mashaka
mengi, ndiyo maana Lema anadai jaji huyo alikosea.
Baada ya
wakili Kimomogoro kuwasilisha hoja hiyo iliyodai Jaji Rwakibalila
hakutumia maamuzi ya kesi zilizowasilishwa mbele yake na mawakili wa
pande mbili, Jaji Massati alisema si lazima jaji au hakimu atumie kesi
zilizowasilishwa mbele yake na mawakili katika kutoa uamuzi.
Hoja
nyingine ni kwamba, hukumu ya Lema iliegemea katika ushahidi wa mdomo
tu bila kuwepo ushahidi wa kuunga mkono kwani mashahidi wa mjibu rufaa,
waliotoa ushahidi walidai walimsikia Lema katika mikutano ya kampeni
akitoa maneno ya kumdhalilisha na kumkashfu Dk. Batilda, lakini
walishindwa kuleta CD, mikanda ya video kuthibitisha.
“Tulimueleza
Jaji Rwakibalila kuwa mashahidi wa wajibu rufaa hawaaminiki na kwamba
ushahidi wao ulikuwa wa mazingira, lakini jaji katika hukumu yake hakuna
sehemu aliyoonyesha kukubali wala kukataa hoja yetu hii,” alidai wakili
Kimomogoro.
Wakili huyo alidai pia Jaji Rwakibalila alikosea
alivyosema Lema ana bahati kwani hakukamatwa wala kushitakiwa kwa kutoa
lugha za kashfa na udhalilisha katika mikutano ya kampeni za uchaguzi wa
mwaka 2010.
Kutokana na madai hayo, alidai kuwa Lema anaiomba
Mahakama ya Rufaa itamke kuwa Jaji Rwakibalila alitamka neno hilo kwa
bahati mbaya na kutamka kwake neno hilo ndiko kulikomsukuma kufikia
uamuzi wa kumfungia Lema asigombee kwa kipindi cha miaka mitano.
“Kwa
hoja hizo tulizoziwasilisha hapo juu, tunaiomba Mahakama ya Rufani
nchini itengue hukumu ya Jaji Rwakibalila kwani haina vigezo wala hadhi
ya kuifanya iwe hukumu, na pia tunaiomba mahakama iwaamuru wajibu rufaa
walipe gharama za uendeshaji wa kesi hiyo tangu ilipoanza Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha na sasa Mahakama ya Rufaa,” alidai wakili Kimomogoro.
Kwa
upande wake wakili wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa
Uchaguzi Jimbo la Uchaguzi, Timon Vitalis, alidai kuwa sheria ya
uchaguzi haiwaruhusu wapiga kura kufungua kesi ya kupinga ubunge wala
wagombea ubunge, udiwani kwani aliyepaswa kufungua kesi hiyo ni Dk.
Batilda na siyo wajibu rufaa ambao ni wapiga kura wa Jimbo la Arusha
Mjini.
Hata hivyo hoja hizo zilipanguliwa na mawakili wa wajibu
rufaa, Aluthe Mugwai na Modest Akida na Wakili wa Msimamizi wa Uchaguzi
na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Vitalis.
Mugwai na Akida
walitetea kuwa hukumu ile ni sahihi na haistahili kutenguliwa kwani
imekidhi matakwa ya kisheria na kuomba mahakama hiyo itupilie mbali
rufaa ya Lema.
Mugwai alisema mawakili wa Lema wanaipotosha
mahakama kwa kusema hakukuwa na uthibitisho wowote ulioonyesha wajibu
rufaa walikuwa wapiga kura wa Jimbo la Arusha Mjini wakati ukurasa wa 10
katika hukumu inayopingwa, inaonyesha namba za vitambulisho vya wapiga
kura ambavyo ni vya wajibu rufaa na wakati vikitolewa mahakamani,
mawakili hao wa Lema walikuwepo.
Kuhusu hoja ya jaji kwamba
alijielekeza vibaya kusema kuwa sheria za Uingereza hazitakiwi kutumika
kuamua katika kesi za uchaguzi, Mugwai alidai Jaji Rwakibalila yupo
sahihi kwani hata kifungu cha 1(2) cha sheria ya uchaguzi sura ya 343,
kinasema masuala yote ya uchaguzi yatashughulikiwa kwa kutumia sheria ya
uchaguzi na kuongeza kuwa mawakili wa Lema wametumia kesi za Mahakama
ya Rufaa zilizoamriwa kwa sheria ya zamani ya uchaguzi ya mwaka 1985
wakati sheria hiyo ya uchaguzi imeishafanyiwa marekebisho na marekebisho
ya mwisho yalifanyika mwaka 2010 .
“Hata kifungu cha 2 (3) cha
sheria ya Judicuture and Application of Law (JALA), inakataza matumuzi
ya sheria za nje kutumika kuamua kesi za uchaguzi wakati nchi yetu ina
sheria mahususi ya uchaguzi kwa ajili ya kuamua kesi za uchaguzi na
kwamba jaji alikuwa sahihi kusema hilo na pia alikuwa sahihi kusema
wajibu rufaa walikuwa na haki ya kufungua kesi hiyo na kuongeza kuwa
hoja hiyo ni butu,” alidai wakili Mugwai.
Hata hivyo, alipinga
hoja ya mawakili wa Lema iliyodai Jaji Rwakibalila katika hukumu yake
hakutumia kesi walizoziwasilisha mbele yake, ambapo alidai katika hukumu
hiyo alitumia baadhi ya kesi walizoziwasilisha mbele yake na kwamba
jaji ana mamlaka ya kuchuja kesi anazotaka kuzitumia kwenye hukumu.
Akijibu
hoja kwamba hukumu ya Lema iliegemea kwenye ushahidi wa mazingira tu,
wakili Mugwai alikanusha na kusema hakukuwepo ushahidi wa mazingira
kwani mashahidi waliomsikia Lema akitoa maneno ya kashfa kwenye mikutano
ya hadhara, walifika mahakamani hapo na kutoa ushahidi wao ambapo
walisema walimwona na kumsikia akfanya hivyo dhidi ya Batilda.
Hata
hivyo wakati wakili Mugwai akiwasilisha hoja zake, baadhi ya watu
wanaodaiwa ni wafuasi wa CHADEMA ambao walijazana ndani ya chumba cha
mahakama, waliguna na kutoa vicheko hali iliyosababisha wakili huyo
awaombe majaji wawadhibiti watu wenye tabia hiyo kwani mawakili wa Lema
walipokuwa wakiwasilisha hoja zao walitulia.
Rufaa hiyo inayovuta
hisia za wengi ndani na nje ya nchi, ilianza kusikilizwa majira ya saa
tatu asubuhi na kumalizika saa tisa alasiri.
Kesi hiyo imeahirishwa na sasa kinachosubiriwa ni tarehe ya hukumu ili kukata mzizi wa fitina.
Kwa
mujibu wa jopo hilo la majaji wa Mahakama ya Rufaa, tarehe ya kutolewa
uamuzi wa rufaa hiyo itatolewa kwa njia ya maandishi kwa mawakili wa
pande zote mbili.
Tanzania Daima
Post a Comment