Mwenyekiti wa CHADEMA,Mh.Freeman Mbowe akihutubia mjini Karatu jana.
Picha na CHADEMA Blog
HATIMAYE Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Freeman Mbowe amevunja ukimya na kuweka bayana kuwa
hatagombea urais katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Kwa kauli hiyo, Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upunzani
Bungeni, amefuta rasmi minong’ono ya muda mrefu kwamba anakusudia
kuwania tena urais baada ya kufanya hivyo mwaka 2005.
Akizungumza na wananchi wa Karatu kwenye Uwanja wa mpira wa Karatu
baada ya kumaliza kikao chake na viongozi wa Karatu, Mbowe alisema kwa
sasa amejielekeza kupanga na kutekeleza mikakati kuhakikisha CHADEMA
inaingia Ikulu mwaka 2015 na kuhakikisha anasimamia kupata viongozi bora
wa kupeperusha bendera ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Mbali na kusimamia upatikanaji wa mgombea bora wa urais, Mbowe alisema
pia kazi yake kubwa itakuwa kuhakikisha anasimamia upatikanaji wa
wagombea bora wa nafasi zote za uongozi kuanzia ngazi ya serikali za
vijiji, vitongoji, madiwani, wabunge na urais.
“Kuna taarifa za upotoshaji zinaenezwa kuwa mimi na Dk. Slaa tuna
ugomvi wa kuwania urais. Jambo hili sio kweli hata kidogo, mimi
sitawania urais mwaka 2015 na Dk. Slaa nafanya naye kazi kwa
kuheshimiana na maelewano ya hali ya juu kwani tumekuwa wote kwa muda
mrefu sasa,” alisema Mbowe.
Alitamba kuwa CHADEMA itaingia Ikulu mwaka 2015 na itachukua majimbo
mengi ya uchaguzi na kutolea mfano wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini kwamba
kati ya majimbo 22 yaliyopo, chama hicho kina uhakika wa kushinda 15.
Kuhusu mgogoro wa Karatu uliokipasua chama hicho katika makundi, Mbowe
alisema umemalizika baada ya kikao chake na viongozi hao kwa siku
mbili.
Katika kuonesha kwamba viongozi hao wamemaliza tofauti zao, Mbowe
aliwapandisha jukwaani viongozi wote na kushikana mikono kama ishara ya
kutakiana amani.
Mwaka 2000, Mbowe alikuwa Mbunge wa Hai, lakini ilipofika mwaka 2005,
chama kilimwomba kuwania urais, hivyo aliacha kuwania ubunge licha ya
wananchi wa Hai kumtaka asiache.
Hata hivyo alishindwa na Rais Jakaya Kikwete. Ilipofika mwaka 2010,
Mbowe aliwania ubunge wakati Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa akijitosa
kuwania urais, akichuana na Rais Kikwete.
Dk. Slaa alitoa upinzani mkali kwa Rais Kikwete na kusababisha aibuke na ushindi mdogo wa asilimia 60.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2010, Mbowe amekuwa akitajwa
na duru za siasa nje na ndani ya CHADEMA kwamba anakusudia kuwania tena
urais mwaka 2015.
Mbowe amekuwa akitajwa sambamba na Dk. Slaa na Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe kwamba wanasuguana kutaka urais kupitia CHADEMA.
Wapo waliokwenda mbali wakihusisha migogoro ya chini kwa chini
inayoendelea ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani, kwamba inatokana
na makundi ya vigogo hao watatu kuutaka urais kwa udi na uvumba.
Hata hivyo, Zitto pekee ndiye ambaye tayari ameshaelezea nia yake ya
kutaka kuwania urais kama chama chake kitampa ridhaa, na amekuwa balozi
mzuri wa kupigia debe katiba ibadilishwe ili umri wa kuwania urais
upungue kutoka miaka 45 ya sasa hadi 30.
NA TANZANIA DAIMA
Post a Comment