Na Esther Wasira

Mabibi na Mabwana,
Mada yangu imegawanyika katika sehemu kuu nne.
(a) Kwanza nitazungumzia kwa nini Tanzania ni nchi ya amani na utulivu.
(b) Pili kama mambo yaliyoipa Tanzania amani bado yanazingatiwa.
(c) Changamoto mpya za amani ya Tanzania.
(d) Mwelekeo wa amani na utulivu wa Taifa letu kwa miaka 50 ijayo.
Kwa nini Tanzania ni nchi ya amani na utulivu?
Mtafiti
mmoja kwa jina Ilana Kessler katika utafiti wake wenye kichwa cha
habari “What Went Right in Tanzania: How Nation Building and Political
Culture have Produced Forty Four Years of Peace, 2006 (Walsh School of
Foreign Service of Georgetown University) katika uk. 2 anasema:
“Pamoja
na kuwepo sababu ambazo zingeweza kudhoofisha amani ya Tanzania kama
vile umaskini, ukosefu wa kazi hasa kwa vijana, uwepo wa makabila mengi
(zaidi ya 120) kuwepo dini kuu mbili (Ukristo na Uislam) na kupakana na
nchi zenye vita, bado Tanzania imebaki kuwa nchi ya amani na utulivu”.
Mtafiti
huyu anajiuliza, Tanzania ilifanya miujiza gani kuweza kujenga taifa
moja lenye amani na utulivu? Kwa hiyo tunakubaliana kuwa amani
tuliyonayo Tanzania si kwamba imekuja tu kimiujiza au si kwamba binadamu
wanaoishi Tanzania ni tofauti na wale wanaoishi Rwanda, Burundi, DRC,
Kenya Uganda, Sudan, Somalia nk. Tanzania tunafanana na nchi nyingine
zilizotuzunguka na hata tuna uhusiano wa damu na mataifa hayo. Hivyo ni
ukweli kuwa kuna kitu waasisi wa Taifa hili walikifanya kuweza kujenga
amani na utulivu.
Wakati
naandaa mada hii, ilinibidi kuisoma katiba na itikadi ya TANU, Azimio
la Arusha, maandiko mbalimbali ya Mwalimu Nyerere pamoja na tafiti
mbalimbali kuhusu amani na utulivu Tanzania pamoja na utamaduni wa
kisiasa Tanzania. “Political Culture”. Baada ya kusoma hayo yote pamoja
na maoni yangu binafsi, sababu zilizojenga amani ya Tanzania ni kama
ifuatavyo:-
Zipo sababu nyingi sana lakini kwa maoni yangu zipo sababu kuu mbili:
(i) Sera safi na itikadi sahihi ya TANU na ASP
(ii) Utekelezaji wa sera na itikadi.
Naomba
nisisitize neno ‘utekelezaji’ maana kama tutakavyoona, sera safi na
itikadi sahihi hazina maana kama hakuna nia wala uwezo wa kutekeleza
sera hizo.
(i) Sera safi na itikadi sahihi ya TANU na ASP
Katiba ya TANU inaeleza wazi kuwa TANU iliamini pamoja na mambo mengine, katika:-
• Binadamu wote ni sawa.
• Kila mtu ana haki ya kuheshimiwa utu wake.
• Kila mtu ana haki ya kumiliki mali asili ya taifa kwa niaba ya vizazi vijavyo.
•
TANU iliamini katika serikali kuzuia mtu mmoja kumnyonya mwingine au
kikundi fulani cha watu kuwanyonya wengine. Hivyo TANU walipania kujenga
jamii yenye usawa na haki.
Malengo ya TANU yalikuwa kama ifuatavyo:-
• Kuzitumia rasilimali za nchi kwa ajili ya kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi.
• Kuhakikisha serikali inaondoa aina zote za unyonyaji, vitisho, ubaguzi, hongo/rushwa na ufisadi.
TANU
pia ilikuwa na miiko ya uongozi. Kikubwa katika miiko ya uongozi ni
kuwakataza viongozi wa umma kutumia nafasi zao kujilimbikizia mali.
Ikumbukwa kuwa Azimio la Arusha lilikuwa ni azimio la kutekeleza sera
safi na itikadi sahihi ya TANU.
Azimio
la Arusha lilikuwa ni azimio lililoleta haki, usawa, utu, uwezo wa
kufanya maamuzi kuhusu rasilimali zetu na lilikuwa ni azimio la ukombozi
kutoka katika makucha ya mabeberu na wanyonyaji.
Kwa
ujumla, sera za TANU zilijenga jamii yenye usawa, haki, umoja na
upendo. Kwa mfano, Watanzania walifanywa kuwa jamii moja na kila mtu
alikula jasho lake. Hakuna aliyeruhusiwa kumnyonya au kumdhulumu
mwenzake.
Kikubwa
zaidi, serikali ilikuwa haina mzaha katika kutekeleza sera na maazimio
iliyopitisha. Kwa mfano, serikali ilikuwa haina mzaha katika kupambana
na rushwa. Rushwa ilionekena kuwa ni adui wa haki na kila mwanachama wa
TANU aliapa kutotoa wala kupokea rushwa. Mwalimu Nyerere katika moja ya
hotuba zake alisema serikali ilikuwa haina utani katika kupambana na
rushwa. Tumesimuliwa na wazee wetu kuwa hata mtu aliyekuwa anakunywa bia
kila siku, kuna watu walikuwa wanahesabu vizibo ili kuangalia kama
idadi ya bia alizokuwa anakunywa inalingana na kipato chake. Nyerere
hakuwa anawapigia magoti wala rushwa kuwaomba waache kujihusisha na
rushwa. Hotuba zenye maneno “wala rushwa tunawafahamu hivyo tunawaomba
waache” hazikuwa kwenye kamusi ya viongozi wa serikali.
Chini
ya uongozi wa Mwalimu, swala kama kuweka fedha kwenye mabenki ya
kigeni, mikataba mibovu, ukwepaji kodi nk. yalikuwa yanashughulikiwa kwa
nguvu zote. Vyombo vya upelelezi na usalama vilikuwa na uzalendo na pia
vyenye dhamira ya kuchunguza na kuwakamata mafisadi na wahujumu uchumi.
Katika
suala la usawa na haki, kila Mtanzania alifanywa kuamini kuwa Tanzania
ni nchi yake. Serikali ilitoa elimu bure na kwa usawa, ilitoa huduma za
afya bure na ilijitahidi kutoa huduma nyingi za jamii bure. Naambiwa
hata watoto wadogo walikuwa wanapewa maziwa bure. Serikali ilikuwa na
dhamira ya kujenga jamii moja hivyo pamoja na rasilimali za nchi kuwa
chache, bado serikali iliweza kutoa huduma kwa haki.
(ii)
Sababu ya pili ni utekelezaji makini wa sera, itakadi na maazimio. Kwa
mfano kwa kuwa serikali ilikuwa haina mzaha kwenye vita dhidi ya rushwa,
tofauti ya kipato kati ya masikini na matajiri ilikuwa ndogo sana.
Kumiliki mali na hasa kama mtu hawezi kueleza amezipataje na kama pia
kipato kilichomuwezesha kupata mali hizo amekilipia kodi, ilikuwa ni
hatari kubwa kwa mtu huyo.
Kwa
hiyo unapokuwa na jamii kama hii inayojali haki za wanyonge, inayopiga
vita unyonyaji, inayopiga vita rushwa, isiyowaogopa mafisadi, isiyokuwa
na matabaka yanayotokana na baadhi ya watu kuwanyonya watu wengine,
inayoongoza kwa maslahi ya wanyonge nk hutegemei kuona fujo au vita
zinazuka baina ya watu hawa. Maana fujo au vita vinasababishwa na
baadhiya watu kujiona wanatengwa katika uongozi wa nchi na pia katika
kufaidi matunda ya uhuru.
Mtafiti
Ilana Kessler katika utangulizi wa kazi yake anasema. “Sera
zilizoanzishwa baada ya Azimio la Arusha zilijenga utamaduni wa kisiasa
ambao ulileta amani. Anasema sera za uchumi zilizingatia usawa,
zilipinga migawanyiko ya kijamii, zilizingati ujenzi wa taifa na
zilijenga utaifa, uzalendo, utambulisho wa kitaifa na ziliwafanya
watanzania wajivunie utaifa wao “national pride”.
Hivyo,
kwa ufupi hayo ndio yametujengea taifa letu, taifa ambalo kila siku kwa
kujua au kutojua tunaimba kuwa ni taifa la amani na utulivu au kisima
cha amani.
Je, mambo yaliyoipa Tanzania amani Tanzania bado yanazingatiwa ?
Kama
nilivyosema hapo juu, Azimio la Arusha lilikuwa Azimio la utu, haki,
usawa, uzalendo na utaifa. Sote tunajua baada ya kuanguka ukuta wa
Berlin, tulilazimika kufuata mfumo mpya wa uchumi. Tunajua kuwa Azimio
la Arusha lilifutwa na serikali ya awamu ya pili na badala yake
wakapitisha Azimio la Zanzibar. Nimejaribu kulitafuta Azimio la Zanzibar
katika maktaba zetu na nakiri sijaliona na wala sijawahi kuliona.
Lakini
watu wenye akili hawawezi tu kusema kuwa Azimio la Arusha halifai au
limepitwa na wakati. Kuna mwanafalsafa mmoja anasema ‘ukitaka kuvunja
uzio, jiulize kwanza ni kwanini uzio huo ulijengwa’.
Baada
ya kulisoma na kulitafakari nakiri katika historia ya Tanzania,
hatutakaa tupate azimio bora kama Azimio la Arusha. Watu wenye akili
wangeweza tu kubadili baadhi ya mambo ili kwenda na wakati ila msingi wa
Azimio ungebaki. Kwa mfano, tungeweza kubadili mfumo wa kumiliki mali
ili watu binafsi wamiliki mashirika ya umma pamoja na migodi kwa
ushirikiano na serikali. Nini kilitushinda kwa mfano kuhakikisha Benki
ya NBC inamilikiwa na serikali au watanzania binafsi kwa asilimia 49% ?.
Kwa kweli Benki ya Taifa ya Biashara, NBC ya zamani ndio ilikuwa nembo
ya kazi alizofanya baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Benki hii ilikuwa na
matawi nchi nzima na kwa wakati huo ilikuwa ni moja ya Benki kubwa
Barani Afrika. Kuambiwa na Benki ya Dunia kuwa ilikuwa kubwa mno na
hivyo igawanywe na iuzwe, ilikuwa ni upuuzi kama alivyowahi kusema
Mwalimu. Mbaya zaidi Benki hii iliuzwa kwa bei ya kutupwa, tunaambiwa
iliuzwa kwa shilingi bilioni 15, bei ambayo haitoshi kulinunua jengo la
makao Makuu ya NBC. Hadi Mwalimu anakumbana na mauti, alikuwa anaililia
NBC na inasemekana alienda kuonana na maafisa wa Benki ya Dunia na IMF
kulalamikia kitendo cha kulazimisha NBC iuzwe. Cha ajabu maofisa wa
Benki ya Dunia walimshangaa Mwalimu kwani walimwambia mapendekezo ya
uuzaji wa Benki hiyo yalitolewa na Serikali ya awamu ya tatu na wala sio
Benki ya Dunia. Hata katika hotuba zake nyingi, Mwalimu alikuwa anapiga
sana kelele kuhusiana na uuzwaji wa NBC.
Mwalimu
huko ulipo tunakuahidi, kizazi hiki cha vijana hakitaacha hata jiwe
moja kufunuliwa na wale waliohusika kuhujumu jitihada za serikali yako
za kuijenga NBC na mashirika mengine ya umma, siku moja wataletwa mbele
ya sheria. Mwalimu tunaahidi pia, wale wote waliouziana nyumba za
serikali kwa bei ya kutupwa wakati nyumba hizo zilikuwa ni jasho lako na
la Watanzania wengine hawataachwa wafaidike kwa hujuma hiyo. Maana
ukweli ni kwamba mashirika ya umma na nyumba za serikali zilijengwa kwa
jasho la wakulima wa pamba, kahawa, tumbaku, korosho nk. Lilikuwa ni
jasho la wafanyakazi wa viwandani, walimu, madaktari nk. Ni kwanini
jasho letu sote wagawane wajanja wachache ? Hiyo haikubaliki hata
kidogo. Naomba nionyeshwe mkulima wa pamba pale Kijiji cha Manyamanyama
Bunda aliyefaidika na uuzaji wa nyumba za serikali na mashirika mengine
ya umma.
Ukiachilia
mbali umiliki wa mali, ni mwendawazimu pekee atakayesema kuwa misingi
ya usawa, haki, uzalendo, utaifa na ujenzi wa taifa zilizojengwa na TANU
hazitufai tena. Baada ya kulipuuza Azimio la Arusha, leo hii kuna mambo
ambayo yanafanyika na ambayo yasipoangaliwa yatatufanya tuharibu amani
yetu.
(i)
Rushwa : Rushwa ya Tanzania inatisha. Rushwa katika taasisi za umma na
katika chaguzi hasa za Chama Tawala si siri tena. Rushwa pamoja na
kwamba ni adui wa haki, inajenga matabaka kwani baadhi ya watu
wanawapora masikini na kujilimbikizia utajiri ambao si wa haki. Kwa
mfano, kama kuna rushwa katika ukusanyaji wa kodi au katika mikataba ya
nchi, ni wazi kwamba hatuwezi kupata fedha za kutosha kuwalipa vizuri
walimu, madaktari, mahakimu, polisi, wanajesh nk. Hatuwezi kutoa elimu
bora, kutoa huduma za jamii, nk. Sijui nani alisema au ametufundisha
kuwa ujasiri na dhamira ya kupambana na rushwa chini ya Azimio la Arusha
haina tena maana.
(ii)
Maadili ya uongozi. Azimio la Arusha lilijenga maadili ya uongozi.
Uongozi ulikuwa ni dhamana na sio njia ya kujitajirisha wewe na familia
yako. Viongozi wengi wa wakati huo walistaafu wakiwa watu wa kawaida.
Mfano mzuri Mwalimu Nyerere alizikwa masikin pamoja na kuongoza nchi hii
kwa zaidi ya miaka 25. Leo mtu akipata uongozi tunasema fulani ameula.
Uongozi si dhamana tena, uongozi si mzigo tena na uongozi si utumishi
tena. Inashangaza viongozi wanakula meza moja na mafisadi. Kiongozi
unakula na kunywa na mafisadi, wewe ni kiongozi wa aina gani ? Fisadi
siku zote anawaza namna ya kuendelea kuwafisidi Watanzania. Sasa kama
kiongozi wa umma ndie mshirika wao, kama kiongozi wa umma ndie
anayechangiwa fedha za kampeni au kutoa misaada kwenye taasisi za dini,
kiongozi huyo pian aye ni fisadi. Kama unatuambia pesa unazotoa misaada
unachangiwa na rafiki zako, tuna haki pia ya kujua hao rafiki zako ni
akina nani na wanachanga kwa nia gani. Sidhani kama marafiki hao
wanachanga kwa vile mhusika ana sura nzuri sana. Nadhani kuna kitu
kinatafutwa na Watanzania tuna kila sababu ya kuambiwa ukweli. Nani
alitudanganya kuwa maadili ya uongozi yaliyojengwa na TANU hayana maana
tena ?
(iii) Haki na Utu
Azimio
la Arusha lilitangaza na kuzisimamia haki za wanyonge na kuheshimu utu.
Je, leo bado tunatetea haki ? Je, tunaweza kuwadhibiti waekezaji ili
walipe fidia ya haki kwa ardhi yetu, walipe mshahara wa haki kwa watu
wetu, wajiepushe kuchafua mazingira yetu au waheshimu utu wetu ?
(iv) Uzalendo na utaifa.
Je, bado tunaona uzalendo na utaifa ni kitu muhimu ? Je kwa taifa linalonuka rushwa, uonevu nk unaweza kujenga uzalendo ?
Kwa
hiyo kwa ufupi, baada ya kulitupa Azimio la Arusha, tumevunja misingi
imara iliyojenga utaifa wetu na amani yetu. Ni sawa na kuvunja nyumba
iliyojengwa na baba yako halafu akaacha kujenga nyumba nyingine.
Changamoto Mpya za Amani ya Tanzania
Mazingira
yaliyokuwepo wakati wa awamu ya kwanza ambayo ndio imejenga amani hii
tunayoiona yamebadilika. Kwa mfano, kwa vile Tanzania ilikuwa ni nchi ya
chama kimoja na serikali moja, ilikuwa na dhamira moja ya kupiga vita
umasikini, maradhi na ujinga. Pia ilikuwa rahisi kuleta umoja wa
makabila yote na dini zote na kulikuwa hakuna sababu ya baadhi ya watu
kutafuta kutugawa kwa msingi ya udini au ukabila.
Leo
hii tuna mfumo wa vyama vingi, uhuru mkubwa wa vyombo vya habari, soko
huria na uhuru wa kutoa mawazo. Katika muelekeo wa amani ya Tanzania kwa
miaka 50 ijayo, nitazungumzia, pamoja na mambo mengine, changamoto
hizi.
Muelekeo wa Amani ya Tanzania kwa Miaka 50 Ijayo.
Nimesema
kuwa amani ya Tanzania imetokana na sera safi na itikadi sahihi ya TANU
na ASP pamoja na dhamira ya utekelezaji wake. Inawezekana kuwa sera na
itikadi ya CCM ya leo haina tofauti sana na ile ya TANU. Lakini
tujiulize,je, bado kuna dhamira na uwezo wa kutekelezasera hizo na
itikadi hiyo? Mimi sidhani kama tatizo la Tanzania ni sera na wala
sikubaliani na wale wanaiomba kila siku kuwa chama chao kina sera nzuri
au wao ndio wameleta amani. Swala lililokubwa ni utekelezaji wa hizo
sera au kuiishi itikadi ya chama. Kama swala ni sera tu, chama chochote
cha siasa kinaweza kuwalipa maprofesa wa vyuo maarufu kama Chuo hiki
Kikuu cha Dar es Salaam, au Haward University au Oxford nk.
wakatengeneza sera nzuri na zinazovutia. Kwa hiyo, kujivunia sera peke
yake bila uwezo au dhamira ya kutekeleza ni sawa na kuwa na gari zuri
ambalo halina engine.
Mtafiti
niliyemtaja Ilana anasema katika uk wa 1 wa kazi yake kuwa, alijaribu
kuwahoji Watanzania wengi. Majibu ya Watanzania wengi ni kuwa Tanzania
ni masikini ; maana hakuna kazi, elimu ni duni, maji na umeme ni shida,
hawawezi hata kumudu milo miwili kwa siku, lakini wanajivunia kuwa
Watanzania maana angalao wana amani. Kwa maana nyingine, kitu pekee
Watanzania wanachojivunia ni amani.
Mtafiti
huyu anasema baada ya kuivunja misingi ya Azimio la Arusha, lazima
Tanzania ijenge utamaduni mpya wa kisiasa ‘political culture’ la sivyo,
nchi hii haina siku nyingi itakuwa sawa na Burundi, Rwanda, DRC nk.
Tutajengaje
utamaduni mpya wa kisiasa ? Kwa maoni yangu, tunapaswa kufanya
yafuatayo ili kujenga utamaduni mpya wa kisiasa na kujenga misingi ya
amani kwa miaka 50.
(a) Lazima Tanzania Tuwe na Serikali Yenye Nguvu
Mwalimu
Nyerere katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Tume ya Kusini ‘South
Commission’ mwaka 1998 kuhusu utawala bora (J.K Nyerere 1998, Good
Governance for Africa) anasema yafuatayo/=
Afrika
lazima iwe na viongozi wenye nguvu ili waweze, pamoja na mambo mengine,
kufanya kazi kwa niaba ya watu wake kutokana na matakwa yao. Anasema
katika soko huria ambalo limetawaliwa na unyonyaji, ufedhuli, ufisadi na
madhila mengine mengi, lazima tuwe na serikali inayoweza kuwatetea
wanyonge.
Anaendelea
kusema hakuna serikali yenye nguvu ambayo haina uungwaji mkono wa raia
walio wengi na haoni itawezekanaje kuwa na serikali yenye nguvu ambayo
haijatokana na uchaguzi huru na haki.
Mwalimu
kwa maana nyingine anasema serikali yenye nguvu si lazima iwe ya
kidikteta na tena anasema udikteta ni udhaifu maana kuwa dikteta maana
yake ni kushindwa kutafuta ridhaa ya watu. Dhana hii inapingana na kauli
za baadhi ya watu wanaosema eti Tanzania tunahitaji rais dikteta. Hi ni
dhana potofu sana. Hatuhitaji Idd Amini, Mabutu au Bokasa wa Tanzania
ili tufanye yafuatayo :-
(i)
Kupambana na rushwa. Watu wanaotutesa kwa rushwa naamini ni chini ya
asilimia kumi (10%). Kama rais unaungwa mkono na zaidi ya asilimia 90%
ya watu katika vita ya rushwa unaopa nini ? Kwa nini uwabembeleze
mafisadi na kuwaomba waache ufisadi au warudishe fedha walizotuibia ili
wasishtakiwe? Hivyo lazima tuchague serikali inayoweza kuwatafuna wala
rushwa bila huruma. Tunataka Watanzania mwaka 2015 mtuchagulie Nyerere
mpya, Sokoine mpya, Kawawa a.k.a Simba wa Vita mpya nk. Tunataka wakati
anaapishwa Nyerere mpya Mwezi November, 2015 kama Rais ambaye nae
atamwapisha Sokoine mpya kama Waziri Mkuu, mafisadi wawe wanahaha
kutafuta tiketi za ndege kuikimbia nchi.
Tunamtaka
Nyerere atakayesaidiwa na Sokoine , ahoji wenye vijisenti kule Uswisi
wamevipaje? Wenye magorofa na fedha zisizoelezeka wamezipataje na kama
wametulipa kodi.
Wataalamu
wa kodi wanajua kuwa kama mtu anajenga ghorofa, anatumia mapato au
amekopa. Lazima tujue amezipataje hizo hela ili tujiridhishe kama
ametulipa kodi. Kama hawezi kutuambia amepataje basi alipe kodi yetu na
kama hawezi basi jengo hilo ni halali yetu.
(ii)
Ulinzi wa rasilimali. Huhitaji kuwa na Bokasa wa Tanzania ili alinde
mbuga zetu, madini yetu, ardhi yetu, misitu yetu nk. Ili kulinda amani
ya nchi lazima rasilimali ziwanufaishe wananchi wote. Tanasikia
malalamiko kila siku kuwa ardhi inachukuliwa bila fidia ya kutosha, watu
na mifugo wanaathiriwa na kemikali, maliasili kama wanyama hai
wanatoroshwa nk. Tunataka serikali inayoweza kumpa mwekezaji masaa 24
awe amefunga mitambo yake na kuondoka baada ya kuwadhuru watu wetu kwa
kemikali. Nyerere anavyosema lazima tuwe na serikali yenye nguvu ana
maanisha tunapaswa kuwa na serikali inayoweza kumuamrisha mwekezaji
aliyechafua maji yetu kwa kemikali atulipe fidia. BP imelipa mabilioni
ya fedha kwa Wamarekeani kama fidia baada ya kuchafua mazingira. BP
walimwaga mafuta baharini na hivyo kuwaathiri wakazi wa maeneo jirani
hasa wavuvi hivyo waliamriwa na serikali yenye nguvu ya Marekani
kuwalipa fidia kubwa waathirika. Tumeambiwa hapa kuna mgodi ulimwaga
kemikali watu watu na wanyama wao pamoja na mazingira viliathirika sana.
Niliona picha ya watu ambao ngozi zao zilibadilika zikawa kama za nyoka
kutokana na kuathirika kwa kemikali lakini sijasikia hatua madhubuti za
kumtetea mnyonge huyu zilizochukuliwa. Sisi tunashindwaje kuwatetea
watu wetu? Kwani mwekezaji ni shangazi au mjomba wetu?
(iii)
Haki za wafanyakazi ; Mabeberu na mabepari wana sifa moja kuu nayo ni
kulinda maslahi yao pekee. Serikali yenye nguvu ambayo Mwalimu
anaizungumzia ni ile inayoweza kumwamuru mwekezaji awalipe watu wetu
mshahara wa kutosha au afunge biashara yake aondoke. Bila kusimamia na
kutetea haki hizi za wanyonge, watu wetu wataendelea kunyonywa.
Nimefanya utafiti kidogo nikagundua kuwa walinzi wa makampuni ya ulinzi
wanalipwa wastani wa shilingi 80,000/= kwa mwezi nk. na wengine
wanafanya kazi kwa masaa 24 mfululizo. Tume wakweli, mlinzi huyu ambaye
ana mke/mume, watoto, ndugu, anapaswa kulipa maji, umeme, kusomesha
watoto, analipa nauli, anakula wakati akiwa kazini nk, kumpa Tsh.
80,000/= ni matusi. Where is the government?
Mwanafalsafa Lenin katika kitabu chake (Lenin, V.I., Imperialism, the Highest Stage of Capitalism, Moscow, pp. 58-59) anasema:-
‘As
long as capitalism remains what it is, surplus capital will be utilized
not for the purpose of raising the standard of living of the masses in a
given country, for this would mean a decline in profit for the
capitalists, but for the purpose of increasing profits by exporting
capital abroad to the backward countries. In these backward countries,
profits are usually high, for capital is scarce, the price of land is
relatively low, and raw materials and labour are cheap’.
Kwa
maneno haya ya Lenin, tusidhani kuwa wawekezaji wanatupenda sana
wanapokuja kuwekeza hapa. Wanakuja ili wachukue ardhi yetu kwa bei chee,
wawalipe watu wetu mshahara mdogo sana, wafanye biashara bila kulipa
kodi, na wanunue mali zetu kwa bei ya kutupwa ili watengeneze faida
kubwa waendelee kuwa matajiri na sisi tuendelee kuwa masikini na
ombaomba. Ni lazima uwe na serikali inayoweza kusimama upande wa
wananchi na kuwa tayari kuwatetea wanyonge. Kuna watu wanacheka eti ni
kwanini TANU iliweka miiko ya uongozi kwa mfano kuwakataza viongozi wa
umma kuwa na nyumba za kupangisha. Busara ya viongozi wa TANU ni kwamba
kwa vile wananchi wengi wakati huo walikuwa masikini, ukimweka kiongozi
mwenye nyumba za kupangisha, hisa kwenye makampuni binafsi nk, atasimama
upande wa wanyonyaji walio wachache dhidi ya wananchi walio wengi. Kwa
mfano, serikali ya awamu ya kwanza ilipitisha sheria inaitwa ‘Rent
Restrictions Act ambayo ilitetea sana na kulinda maslahi ya wapangaji.
Baada ya viongozi wa sasa kumiliki nyumba wamebadilisha sheria sasa
mpangaji hana ulinzi tena maana viongozi wamesimama upande wa wenye
nyumba dhidi ya wananchi masikini. Hebu tujiulize; kama Rais aliye
madarakani anafanya biashara ikulu, anajimegea mashirika ya umma nk, je
atasimama upande wa wawekezaji au wananchi? Ndio maana tunasema lazima
turudishe maadili ya uongozi.
Tunavyozungumzia
amani tunazungumzia haki. Kama hawa watanzania wataendelea kunyonywa na
serikali yao ikaamua kufunga nira na mabeberu basi kuna siku hawa
wananchi wanyonge watakataa.
Lakini
haki za wafanyakazi si za wafanyakazi wa sekta binafsi tu. Hata
wafanyakazi wa sekta ya umma hawatendewi haki. Kima cha chini ni kidogo
sana na kinawafanya wafanyakazi hawa wanakata tama.
Mwalimu
Nyerere katika hotuba niliyonukuu hapo juu anasema mshahara wa kutosha
hauwezi kuwazuia watu wabaya kula rushwa lakini mshahara mdogo na
usiokidhi mahitaji ya mfanyakazi utawachochea hata wale wazuri nao wale
rushwa. Anaendelea kusema unapokuwa na viongozi wa siasa wala rushwa au
wanaohisiwa kuwa ni wala rushwa unaifanya hali ya nchi kuwa mbaya zaidi.
Ili kulinda amani ya Tanzania lazima tuwajali wafanyakazi badala ya
kuwahujumu watetezi wao. Na hapa napenda kuzungumzia tukio la kutekwa na
kufanyiwa unyama kiongozi wa Chama cha Madaktari, Dr Ulimboka.
Pamoja
na kwamba swala hili lipo mahakamani, mazungumzo yangu hayaingilii hata
kidogo uhuru wa mahakama. Watanzania wote tumeshuhudia unyama huo, na
mhusika alijaribu kutaja wale waliohusika kumtesa. Serikali inakanusha
kuhusika lakini haichukui hatua muafaka kuchunguza swala hili ili
kuwaleta mbele ya sheria wale wanaohusika. Serikali ambayo imesimama
upande wa umma haiwezi kukaa kimya pale watu wake wanapoonewa. Kama
serikali haihusiki au imeshindwa kuwajua wanaohusika, ingewaleta
wapelelezi wenye uwezo mkubwa kama ‘Scotland Yard’ ili uchunguzi
ufanyike na wanaohusika wachukuliwe hatua. Serikali kukaa kimya
“inatafsiriwa” kama ni njia ya kuwatisha wale wanaotetea maslahi ya
wanyonge. Hata hivyo, katika historia ya dunia, hakuna kipigo wala
risasi iliyoweza kunyamazisha sauti za wale watetezi wa wanyonge.
(iv)
Amani ya Tanzania ya miaka 50 ijayo itajengwa na haki ya demokrasia.
Tumeruhusu mfumo wa vyama vingi, lazima pia turuhusu vyama hivi vifanye
kazi za siasa. TANU ilihamasisha Watanzania kuunga mkono maazimio na
sera mbalimbali kwa kuitisha maandamano. Tumeambiwa wakati Azimio la
Arusha lilivyotangazwa Mwalimu Nyerere alitembea kwa miguu kutoka
Butiama hadi Musoma kuunga mkono Azimio. Sasa leo kama chama cha siasa
kina sera zake na kinataka ziungwe mkono au kinapinga sera zilizopo
kikaamua kuitisha maandamano kuna tatizo gani? Kuzuia demokrasia ni
kupandikiza mbegu ya vita na machafuko.
Ni
ukweli kuwa siku za hivi karibuni jeshi la polisi limekuwa linatumiwa
na baadhi ya wanasiasa wasiotutakia mema kuharibu amani ya nchi kwa
kuuwa watu bila sababu. Naomba ninukuu muhtasari wa taarifa ya Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa tukio lililopelekea
kifo cha Daudi Mwangosi kilichotokea September, 2, 2012.
Katika
kifungu cha 2, taarifa inasema ‘kutokana na hayo yote, Tume
imejiridhisha kuwa tukio lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi
limegubikwa na uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya
utawala bora.
Kifungu
cha 2.1 kinasema ‘CHADEMA ni chama cha siasa ambacho kina usajili wa
kudumu. Chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa (Cap 258 R.E 2002) vyama vya
siasa vyenye usajili vimeruhusiwa kufanya maandamano na kuitisha
mikutano ya kujitangaza baada ya kutoa taarifa kwa afisa wa polisi
katika eneo husika. Baada ya kutoa taarifa, kazi ya jeshi la polisi ni
kutoa ulinzi.
Hitimisho la taarifa ya Tume ni muhimu sana Watanzania na hasa jeshi la polisi kulizingatia.
Hitimisho lipo katika kifungu cha 4.0.
‘Jukumu
la kulinda amani na utulivu ni wajibu wa kila Mtanzania… Tume inatoa
wito kwa Watanzania wote kuheshimu haki za binadamu na kutekeleza kwa
vitendo misingi ya utawala bora. Kwa kufanya hivi taifa letu litaendelea
kuwa na amani na utulivu. Tume inatoa rai kwa jeshi la polisi
kutekeleza wajibu wake mkuu wa ulinzi na usalama wa raia bila kutumia
juzba. Kuwepo kwa vyama vya siasa ionekane kuwa ni kukua kwa demokrasia
na sio kuwa ni upinzani kwa chama tawala’.
Pia
magazeti hivi karibuni yalimnukuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wakati akihutubia vikao vya Chama huko Dodoma akiwaonya wana
CCM kuacha kulitegemea jeshi la polisi na badala yake wajibu hoja za
wapinzani majukwaani. Hadi Rais ambaye ni Amiri jeshi Mkuu kufikia hatua
ya kusema maneno haya hadharani, inaondoa shaka kuwa vitendo
vinavyofanywa na jeshi la polisi vya kuzuia demokrasia kuchukua mkondo
wake vinachochewa na viongozi wa CCM wanaoogopa hoja na kudhani kuwa
wataokolewa na jeshi la polisi. Hata hivyo, historia inatufundisha kuwa
hakuna jeshi la polisi popote duniani lililoweza kuzuia milele uhuru wa
watu.
Kwa
kumalizia kipengele hiki, ili amani idumu, taasisi za serikali kama
polisi, jeshi, mahakama, ofisi ya msajili wa vyama, Tume ya Uchaguzi na
nyingine lazima ziwe huru na zitende haki kwa Watanzania wote bila
kujali dini, vyama vya siasa au eneo alilotoka mtu. Mfano mdogo tu ni
kwamba kama Kenya katika uchaguzi wa mwaka 2007 ingekuwa na Tume Huru ya
Uchaguzi, mauaji ya raia wasiokuwa na hatia yasingetokea. Mwenyekiti wa
Tume ya Uchaguzi wakati huo alinukuliwa akisema hajui ni nani alishinda
kiti cha urais. Sasa alitangazaje matokeo kama alikuwa hamjui mshindi?
Huku ni kukosa uhuru wa kiutendaji na mawazo.
(v) Ajira kwa Vijana
Serikali
kwa sasa haina njia mbadala. Kuendelea kwa amani ya Tanzania ni ndoto
kama vijana hawatasaidiwa kwa dhati kupata ajira. Vijana wengi wa
Tanzania wamekata tamaa. Wanasiasa hasa wa Chama Tawala wamekuwa wanatoa
majibu mepesi kuwa vijana waende vijijini wakalime. Haya majibu
hayasaidii kutatua tatizo.
Ikumbukwe
kuwa kilimo ni uwekezaji. Kilimo kinahitaji mtaji mkubwa, ardhi, soko
la mazao, utaalam wa kilimo nk. Kijana ambaye hana chochote ni matusi
kumwambia aende kijijini akalime. Cha kushangaza zaidi hawa wanasiasa
wanaosema vijana wakalime wao watoto wao wako kwenye viyoyozi mijini.
Kama kilimo ndio ukombozi kwa vijana, basi watoto wa wanasiasa hawa ndio
wangepaswa kuwa wa kwanza kwenda vijijini.
Tujifunze
kutoka ‘Arab Spring’. Kuna kijana mmoja Mtunisia anaitwa Mohammed
Bouazizi ambaye alisoma hadi chuo kikuu. Kwa vile alikosa kazi na
serikali yao haikuona sababu ya kuwahangaikia vijana wapate ajira,
kijana huyu aliamua kufanya biashara ya kimachinga ya kuuza matunda.
Askari wa Jiji waliamua kumnyanganya matunda yake. Kijana kuona hana
namna nyingine ya maisha aliamua kujimwagia petrol na kujichoma moto.
Kitendo hicho kiliwasikitisha wengi matokeo yake watu waliandamana
wakaiangusha serikali ya Tunisia. Mambo haya yaliendelea yakamtafuna
Gadafi, Mubarak yakaenea Yemen, Bakhrain, Algeria na sasa mnaona
yanayoendelea Syria. Nchi za kibepari zilitambua hilo mapema wakaamua
kuwalipa vijana wao ‘unemployment benefit’ ndio maana mapinduzi ya
kijamaa hayakutokea Ulaya magharibi. Tulizingatie sana hili la vijana
maana pamoja na kwamba nguvu za vijana zinapotelea vijiweni bure, vijana
hawa ni bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote.
(vi)
Lazima turudi kwenye misingi ya Azimio la Arusha kuhakikisha Watanzania
wanapata haki ya elimu, huduma za jamii nk. Kuna wanasiasa wanasema
huko ni kuturudisha kwenye ujamaa. Cha kushangaza, wanasiasa haohao
wanasema Tanzania ni nchi ya ujamaa na kujitegemea. Nani alikuambia
elimu bora na ya bure hasa kwa wasiojiweza ni siasa ya kijamaa? Nani
alikuambia huduma za afya bure ni siasa ya kijamaa? Misingi ya Azimio la
Arusha ni dhahabu, Watanzania tuna dhahabu ila hatujijui. Wenzetu
wamekuwa wanaiga misingi ya Azimio hili na kulitekeleza kwao.
(a)
Rais Bush Jr wa Marekani aliiga Azimio la Arusha akaanzisha kitu
kinaitwa ‘No child shall be left behind’ program. Mpango huu
ulihakikisha kila mtoto wa Mmarekani anapata elimu bora hata kama hana
fedha.
(b)
Rais Obama ame copy msingi wa Azimio la Arusha kwa mpango wake wa bima
ya afya ambao unalenga kumpa kila Mmarekani nafasi ya kupata huduma bora
ya afya hata kama hana fedha.
(c)
Kenya wame copy misingi ya Azimio kwa katiba yao kutamka kuwa elimu
bora ni haki ya kila mtu. Sheria imepitishwa Kenya, the Education Act,
2012 ku-guarantee haki ya kusoma hadi chuo kikuu hata kama mtu hana
fedha.
Tukirudia misingi yetu, tukizingatia haki ya elimu na huduma nyingine za jamii, amani yetu itaendelea kunawiri.
(vii) Tuzuie uchochezi wa dini na ukabila
Hivi
karibuni tumeshuhudia chokochoko za dini hapa Tanzania ambazo
zinatishia amani yetu. Utafiti uliofanywa na REDET mwaka 2000 ulionyesha
kuwa asilimia 78% ya Watanzania wanaamini uhusiano kati ya wakristo na
Waislam wa Tanzania ni mzuri sana. Hivyo tunasema kwa hakika hakuna
ugomvi wala chuki kati ya wakristo na waislamu wa Tanzania.
Tatizo
lipo kwa wanasiasa waliofilisika na wenye udogo wa mawazo wanaodhani
kuwa wanaweza kutumia tiketi ya udini au ukabila/ukanda kuendelea kubaki
madarakani. Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 unadhihirisha hili. Hata
uchaguzi mdogo wa Igunga-Mahakama Kuu imesema wazi kuwa uligubikwa na
udini.
Tufanye nini?
Nilidhani
wazee wetu wastaafu kama akina Mh. Ally Hassan Mwinyi, Salim A.Salim,
John Malecela, Kingunge Ngombale Mwiru, Joseph Warioba, Mzee Joseph
Butiku nk. wangesimama kidete kukemea kwa nguvu zote chuki za kidini,
kikabila na rangi zinazopandikizwa na baadhi ya watu lakini hawajafanya
hivyo. Hata kama wamefanya, si kwa kiwango cha kutosha.
Watanzania mtakumbuka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na 2005 kulitolewa shutuma kuwa CUF ni chama cha kidini.
Mwaka 1995 NCCR-Mageuzi kilisemwa kuwa kilikuwa chama cha Wachaga.
Mwaka 2005 Dr. Salim Ahmed Salim alisakamwa kuwa ni mwarabu hivyo asingefaa kuwa Rais.
Mwaka 2010 Chadema kilisakamwa kuwa ni chama cha kaskazini na ni chama cha wakristo. Haya mambo yanasemwa bila haya majukwaani.
Dr.
Salim anaheshimika sana Tanzania. Ameshawahi kushika nyadhifa nyingi
sana nchi hii. Kusema leo kuwa yeye ni mwarabu eti kwa vile alitaka
kugombea urais ni kosa kubwa na ilipaswa likemewe kwa nguvu zote na
Watanzania wanaopenda amani. Kufumbia macho mambo haya yataendelea kukua
na yatahatarisha amani yetu. Na kweli yanakua maana tumeambiwa kuwa
Rais hawezi kutoka Kaskazini hata kama ni kwa tiketi ya CCM. Kesho
tutaambiwa Rais hawezi kutoka Musoma maana hawa watu wa Musoma kama
akina Esther wana damu ya Unyerere hivyo wakishika nchi watakuwa wakali
kutetea haki za mnyonge kama alivyofanya Mwalimu.
Hatujaambiwa CUF kimeacha kuwa chama cha udini lini wala NCCR kuwa chama cha wachaga lini.
Kwamba
Chadema ni chama cha kaskazini wakati kina wabunge na madiwani nchi
nzima ni kichekesho. Basi hawa wanaopiga kelele watuambie kuwa mikoa ya
Rukwa, Iringa, Katavi, Mbeya, Singida, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dar es
Salaam nk iliyotoa wabunge wa Chadema kwamba siku hizi inaitwa Mikoa ya
Kaskazini.
Kwamba
Chadema ni chama cha kidini ni matusi na kebehi kubwa. Takwimu
zinaonyesha kuwa kati ya viongozi wakuu sita wa juu wa Chadema, wanne ni
waislam. Lakini watu hawa wanaosemasema mambo haya hawatuambii pia kuwa
chama chao ni chama cha familia maana kuna familia moja ambapo baba,
mama na watoto ni wajumbe wa kikao cha juu cha chama hicho.
Napendekeza
itungwe sheria kali ambayo itaunda chombo cha kufuatilia kauli za
wanasiasa na Watanzania wengine. Chombo hiki kipewe mamlaka ya kuwahoji
na kuwashtaki wale wanaohubiri udini, ukanda au rangi. Sheria iweke
adhabu ya kifungo pamoja na faini kubwa ikiambatana na kufungiwa
kujihusisha na siasa kwa miaka mingi au maisha. Chombo hicho pia kipewe
mamlaka ya kumhoji Rais na kumshtaki bungeni ili aondolewe madarakani
kama yeye ndie atakuwa ametoa hotuba ya uchochezi au kujihusisha na
vitendo vya kuwagawa wananchi.
Rwanda waliwavumilia walioleta uchochezi bila kuchukua hatua, madhara yake mmeyaona, Tanzania tusifanye kosa hilo.
(viii)
Mwisho katika kulinda amani kwa muda mrefu tuhimize muungano wa chi
zetu. Matatizo mengi ya amani Afrika yanatokana na umasikini na uhaba wa
rasilimali. Mfano nchi kama Burundi, kutokana na uhaba wa ardhi, watusi
au wahutu wanajaribu kutumia karata ya ukabila ili kuwaondoa wenzao.
Hebu fikiria tungeunda muungano wa Sudan Kusini, Kenya, Uganda,
Tanzania, Rwanda, Burundi na DRC. Tungekuwa na uchumi mkubwa kuliko
India na Brazil. Watu wa nchi hii kubwa na tajiri wangehangaika na
uchumi zaidi kuliko kuangalia ukabila na udini. Tanzania tunaweza
kuongoza tena jitihada za muungano maana awali Kenya ndio walikuwa
wanaogopa muungano wakati Tanzania ilikuwa tayari muda wowote kuungana.
Mwalimu alishawahi kusema, kama Kenyata akikubali leo tuungane, kesho
mimi nipo tayari, tena nakubali yeye awe Rais. Huu utashi wa Muungano
umeenda wapi? Au kuna watu wanadhani ukiwa na muungano itakuwa ngumu wao
kuendelea kujineemesha? Tusiwe waoga maana hata Mwalimu alisema…’africa
bila muungano haina future’. Tuweke maslahi binafsi nyuma, tuwajengee
watoto wetu taifa lenye nguvu ili wawe na nafasi yao duniani. Nina
ndoto, Tanzania tutachukua tena nafasi yetu ya uongozi. Tutahimiza tena
muungano na hata tutakuwa tayari kukubali kiongozi wa juu atoke nchi
nyingine ili mradi tu maslahi ya watu wetu yalindwe.
Mwisho namalizia kwa kunukuu maneno ya mtafiti Ilana Kessler na naomba myatafakari. (uk 103 wa kazi yake).
‘Watanzania
wengi hasa wenye umri mkubwa wanaichagua CCM pamoja na kwamba
hawaziamini tena sera zake na wala hawawaamini tena viongozi wake.
Sababu pekee inayowafanya waichague CCM ni kwa vile wanaamini kuwa CCM
italinda amani. Kama vyama vya upinzani Tanzania vikiweza kuwashawishi
hawa Watanzania kuwa nao wanaamini katika amani na wanalengo hilohilo la
kulinda amani ya Tanzania, basi wataweza kuzipata kwa urahisi kura za
watu hawa na hakika wataiangusha CCM kwa urahisi sana’
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza, Mungu Ibariki Tanzania.
This post was written by: Author Name
Your description comes here!
Get Free Email Updates to your Inbox!
Filed Under:
Jamii
on Monday, December 10, 2012
Post a Comment