Wananchi waliojeruhiwa wakiwa wanavuja damu
kufuatia vurugu kubwa iliyozuka kati ya wananchi hao na Polisi katika
viwanja vya Mashujaa mjini Mtwara jana.
Malalamiko hayo walikuwa wayakabidhi kwa
wabunge wa mkoa huo ambao ni Asnein Murji wa Chama cha Mapindunzi (CCM)
na Said Baruani kutoka Chama cha Wananchi (CUF). Hata hivyo, hadi
tunakwenda mitammboni Murji alikuwa hajafika eneo hilo la mkutano kwa
madai kuwa alikuwa amekwama baada ya gari lake kuharibika.
Aidha, maandamano hayo pia yalikuwa
yakielekea ofisi za Shirika la Umeme (Tanesco) mkoani hapa, kupinga
kukatika kwa umeme uliokwamisha mkutano wao uliokuwa unafanyika katika
Uwanja wa Mashujaa.
Waliojeruhiwa katika vurugu hizo wametajwa kuwa ni wakazi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Rashid Mohamed na Mustafa Hasan.
Vurugu hizo zilianza baada ya wananchi hao
waliokuwa wakitokea Uwanja wa Mashujaa kwa kuwafuata wafanyabiashara wa
maduka, hoteli na baa ambao hawakutii amri ya kufunga biashara zao na
kujumuika katika maandamano hayo.
Maandamano hayo yalisababisha polisi wa
kikosi cha kutuliza ghasia, kuingilia kati na kurusha kufyatua mabomu
hayo ili kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiwabugudhi wafanyabiashara.
Wananchi hao walisikika wakitoa amri kwa
wafanyabiashara ya kuwataka wafunge biashara zao kwa muda na kisha
kujumuika kwenye maandamano hayo.
“Funga duka lako…funga baa yako, funga
lounge yako…sisi wananchi wa Mtwara twendeni tukatetee gesi yetu… na
gesi kwanza uhai baadae…mpaka kieleweke…,” walisikika wananchi hao
wakiamrisha wafanyabiashara hao.
Wakazi waliojeruhiwa walisema kuwa
walikuwa wakikimbilia gari la aliyewahi kuwa mgombea wa ubunge jimbo la
Tandahimba kwa tiketi ya CUF, Katani Ahmed Katani, kwa ushabiki wa
kumfurahia kiongozi huyo ambae kwa madai yao ni mwanamapinduzi wa
kutetea rasilimali gesi .
“Sisi tulikuwa tukilifuata gari la Katani
huku tukimfurahia Katani…na sio kama tulikuwa tukifanya fujo ila cha
kushangaza jeshi la polisi liliamua kutufyatulia mabomu miguuni na
angalia jinsi tulivyoumia…,” alisema mmoja wa majeruhi hao.
Majeruhi hao walikimbizwa katika hospitali ya Mkoa wa Ligula na hali zao zinaendelea vizuri.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mtwara, Maria
Nzuki, alipoulizwa kwa njia ya simu ya mkononi kuhusu watu hao
kujeruhiwa, alikana kuwepo kwa tukio hilo na kukata simu yake.
DC, VIONGOZI WA CCM (W) YA NACHINGWEA WAZOMEWA.
Wakazi wa mji mdogo wa Nachingwea, mkoani
Lindi, wamewazomea viongozi watatu wa wilaya hiyo, akiwemo mmoja wa
Serikali na wawili wa kisiasa kwa madai ya kutoridhishwa na ushawishi
wao wa kuwataka wasiwaunge mkono wananchi wa mkoa wa Mtwara, wanaopinga
mpango wa Serikali wa kuisafirisha gesi kwenda Dar es salaam.
Viongozi waliokumbwa na zomeazomea hiyo ni
mkuu wa wilaya hiyo, Reginal Chonjo, Mwenyekiti wa CCM, Albert Mnali na
mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya Chama hicho, Fadhili Liwaka.
Tukio hilo limetokea mwanzoni mwa wiki
hii, kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na viongozi hao uliofanyika
viwanja vya kituo cha mabasi cha mji mdogo wa Nachingwea.
Wakiwa wanahutubia umati mkubwa wa watu
katika eneo hilo, kwa nyakati tofauti viongozi hao, waliwataka wananchi
wa wilaya hiyo, kutowaunga mkono mgogoro wa gesi unaoendelea mkoani
humo, kwa madai kwamba hauna maslahi kwa wakazi hao.
Zomeazomea hiyo, ilikuja muda mfupi, baada
ya Mkuu wa wilaya hiyo kusimamana kuanza kuhutubia huku akiwataka
kutojiingiza kwenye maandamano yanayoandaliwa hivi karibuni katika miji
ya Mtwara na Lindi, kuishinikiza Serikali kutoihamisha gesi
iliyogundulika mkoani Mtwara.
Katika mkutano huo Chonjo alisema wakazi
wa wilaya ya Nachingwea hawana sababu ya kushiriki migogoro hiyo, kwa
madai kwamba tangu awali wananchi hao wamekuwa wanatumia raslimali
zilizo nje ya wilaya na mkoa wao wa Mtwara.
Mkuu huyo wa wilaya ya Nachingwea,
alizitaja baadhi ya raslimali ambazo wana Mtwara wanazitumia kutoka nje
ya maeneo yao kuwa ni pamoja na umeme na barabara ya Kibiti hadi Lindi,
ambao ujenzi wake umetokana na raslimali alizodai ni za nchi nzima.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment