Waziri
wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya mji
wa Kyela kupiga marufuku uoshaji magari katikati ya mji.
Dk. Mwakyembe alitoa agizo hilo jana baada
ya kufanya ziara mjini hapa na kukuta vijana wakiosha magari pembeni
mwa barabara karibu na Hospitali ya Wilaya.
Alichukua hatua hiyo baada ya kuhudhuria
kikao cha madiwani wa Kamati ya Fedha na Uchumi ambacho pamoja na mambo
mengine madiwani walijadili suala la tabia ya vijana kuosha magari
katikati ya mji hali ambayo imekuwa ikisababisha uchafu wa mazingira.
Katika kikao hicho, Mtendaji wa Mamlaka ya
Mji wa Kyela, Raphael Samwel, alisema vijana walikwisha elezwa
wasitishe uoshaji magari katikati ya mji lakini hata hivyo bado
wamekaidi agizo hilo hali ambayo imekuwa ikileta usumbufu kwa wananchi
wengine.
Samwel alisema kutokana na hali hiyo
wananchi ambao nyumba zao zipo karibu na maeneo kunapooshwa magari
wamekuwa wakilalamika kutokana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na
waosha magari hao.
Kufuatia hali hiyo, Dk. Mwakyembe alisema kuanzia sasa Mamlaka ya Mji wa Kyela ipige marufuku uoshaji wa magari katikati ya mji.
Alisema magari yote yawe yanaoshwa eneo la
Bwawani na kuagiza viongozi wa Mamlaka ya Mji wa Kyela kupeleka huduma
ya maji katika eneo hilo.
Alisema kwa upande atahakikisha
anatengeneza banda kwa ajili kupumzika watu watakaokuwa wanasubiri
wakati magari yao yanaoshwa.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment