MWAKA 1951 nchi ya kwanza Afrika 
ilipata uhuru na kufikia mwaka 1966, nchi karibu zote zilipata uhuru 
isipokuwa sita tu. Kwa maana hiyo, si vibaya kusema Bara la Afrika kwa 
wastani liko kwenye miaka ya 50 ya uhuru wake kutoka kwa wakoloni.
Kipindi hiki cha miaka 50 ya uhuru Afrika kinakwenda sambamba na miaka 
50 ya watu wa rangi hasa weusi nchini Marekani, kuwa na haki kamili za 
kiraia (civil rights) baada ya kupitishwa sheria ya haki za kiraia 
(civil rights act), mwaka 1964 na ile ya haki ya kupiga kura (voting 
rights act) mwaka 1965.
Sheria hizi mbili ziliondosha kabisa sheria za kibaguzi zilizojulikana 
kama Jim Crow; sheria zilizokuwa zikitenganisha wazungu na jamii 
nyingine hasa weusi, kwa kila nyanja za maisha yao mfano shule za weupe 
na weusi, sehemu za kukaa kwenye mabasi (weusi walitakiwa kukaa nyuma na
 kukaa mbele ilikuwa kosa kisheria) na pia katika makazi.
Sheria za kibaguzi za Jim Crow ndiyo zilizopingwa na Martin Luther King,
 hadi kuawa kwake mwaka 1968, King alitaka watu wote bila kujali rangi 
wawe na haki sawa nchini Marekani, lakini Marcus Garvey na Malcom X 
walikuwa na maoni tofauti.
Ingawa Malcom X alikuwa akibadili mtazamo kulingana na mwenendo wa 
wakati, yeye na Marcus Garvey kwa nyakati tofauti walitaka weusi wawe na
 nchi yao, kwa maana taifa la weusi iwe kurudishwa Afrika au kupewa 
sehemu ya Marekani waanzishe taifa la weusi.
Madhumuni ya Marcus Garvey na Malcom X kutaka sheria za kibaguzi ni 
kuonyesha kwamba watu weusi wanavipawa au akili kama Wazungu.  
Waliamini kabisa kwamba weusi wakiwa na taifa lao, wataweza kuwa na 
misingi mizuri ya kidemokrasia, kujitawala, kufanya biashara na mambo 
mengine mengi tu yanayohusu maisha ya mwanadamu.
Marcus Garey alizaliwa mwaka 1887 nchini Jamaica na kufariki mwaka 1940 
jijini London, Uingereza. Aliendeleza harakati za kudai haki za weusi 
kutoka kwa weusi waliomtangulia kama Prince Hall, Martin Delany na 
Edward W. Blyden kwa kujikita zaidi kwenye falsafa ya Pan-Africanism 
(umajumui wa Afrika); itikadi na vuguvugu kuhimiza umoja wa watu weusi 
duniani.
Aliongoza harakati zake za ukombozi wa weusi kwa kutia hamasa ya weusi popote duniani kurudi barani Afrika liliko chimbuko lao.
Pia alihimiza uwezeshaji wa weusi kiuchumi kwa vitendo, baada ya 
kuhimiza weusi kuanzisha kampuni ya meli ya weusi iliyoitwa Black Star 
Line na gazeti la kila wiki lililojulikana kama Negro World lililopigwa 
marufuku na wakoloni kuingizwa katika makoloni yao Afrika.
Ni katika gazeti hilo la kila wiki la Negro World, Marcus Garvey aliweza
 kuandika na kuchapisha makala kuhimiza juu ya umoja wa watu weusi 
popote pale duniani.
Moja ya makala aliyoandika kwenye Negro World juu ya umoja wa weusi ni 
ile iliyokuwa na kichwa cha habari “African Fundamentalism”, moja ya 
nukuu kutoka kwenye makala hiyo ni “Our union must know no clime, 
boundary, or nationality; let us hold together under all climes and in 
every country…”, kwa tafsiri isiyo rasmi; “Umoja wetu usiangalie pande 
gani ya dunia, mipaka au utaifa bali tufungamane kutoka pande zote za 
dunia na katika kila nchi.”
Makala nyingine alizoandika ni kama “Society and The Selfish Exploiter”,
 hii ni makala iliyohusu unyonyaji na kuwaita watu wanaodhulumu wanyonge
 kuwa wahalifu zaidi ya wauaji.
Vilevile katika harakati za kupinga ukoloni uliokuwa ukiendelea Afrika, 
Marcus Garvey alitoa hotuba ya kusisimua kwa weusi waliojumuika kwenye 
ukumbi wa Liberty (Liberty hall), New York mwaka 1921 na kuipa kichwa; 
“Africa For The Africans”, nitatoa baadhi ya nukuu kutoka kwenye hotuba 
hiyo sambamba na tafsiri isiyo rasmi:
“Say! Africa for the Africans, 
Like America for the Americans:
This the rallying cry for a nation, 
Be it in peace or revolution.
Blacks are men, no longer cringing fools; 
They demand a place, not like weak tools;
But among the world of nations great
They demand a free self-governing state”.
“Sema! Afrika kwa Waafrika.
Kama Marekani kwa Wamarekani:
Hiki ni kilio cha kudai taifa,
Iwe ni kwa amani au kwa mapinduzi.
Weusi ni binadamu, sio tena wajinga;
Wanadai sehemu, wao sio dhana dhaifu;
Bali kati ya mojawapo ya mataifa duniani,
Wanadai taifa huru linalojitawala”
Ndugu zangu, hayo ni maneno ya Marcus Garvey miaka 30 kabla nchi ya 
kwanza Afrika ipate uhuru na miaka 45 kabla karibu kila nchi Afrika 
ipate uhuru, isipokuwa nchi sita tu.
Miaka 11 baada ya kifo chake nchi ya kwanza Afrika ilipata uhuru na 
miaka 26 baada ya kifo chake, nchi karibu zote zilipata uhuru. Hivyo 
harakati zake japo za kutaka weusi kuachiwa Afrika zilikamilika akiwa 
tayari ameiaga dunia, kwa bahati mbaya pia alikuwa amefariki kabla ya 
kukanyaga ardhi ya Afrika.
Kwa upande wa Malcom X, yeye mpaka kuawa kwake mwaka 1965, karibu nchi nyingi za Afrika zilikuwa zimepata uhuru.
Aliuawa takribani miezi sita kabla ya Wamarekani weusi kuwa na haki sawa
 za kiraia kwa kupitisha sheria ya mwisho ya haki ya kupiga kura (voting
 rights act). Kama nilivyosema mwanzoni, Malcom X alikuwa akibadilika 
kiasi kwenye mitizamo yake kadiri muda ulivyokuwa unakwenda lakini bado 
msimamo wake ulikuwa wa kuhimiza utengano wa weusi na wazungu, kwa maana
 na weusi kuwa na taifa lao.
Aliendelea kudai kwamba kwa muda wa zaidi ya miaka 400 ya mateso ya 
weusi nchini Marekani, basi Marekani igharimie usafiri wa watu weusi 
kurudi Afrika au wapewe ardhi sehemu ya Marekani waanzishe taifa la 
weusi na waweze kuonyesha uwezo wao kwamba ni binadamu kama wengine, 
wanaweza kujitawala, kufanya biashara na mambo mengine.
Pia aliendelea kupinga juu ya Marekani kuingilia mambo ya nchi za Afrika
 na hii inajionyesha pale baada ya kuawa Rais Kennedy, wa Marekani 
wakati huo siku iliyofuata kiongozi wake mkuu wa kundi la Kiislam la 
Nation of Islam, alimsihi kutozungumzia kabisa mambo yanayohusu Rais 
Kennedy kesho yako kwenye mkutano.
Lakini alipoulizwa swali na mwandishi kuhusu kuawa kwa Rais Kennedy, 
baada ya kumaliza hotuba yake, Malcom hakuonyesha kushangaa kwani 
alisema hayo ni malipo juu ya machafuko yanayosababishwa na Marekani 
duniani kote, na mnukuu hapa “Being an old farm boy myself, chickens 
coming home to roost never did make me sad, they have always made me 
glad.” Aliendelea kudai kwamba Rais Kennedy ndiye aliagiza kuuawa kwa 
Waziri Mkuu wa Congo, Patrick Lumumba. Malcom X alisimamishwa kufanya 
kazi za kundi hilo la Nation of Islam kwa siku 90, lakini hakurudi tena 
na alianzisha kundi lake na kuuawa mwaka mmoja baadaye.
Wote Marcus Garvey na Malcom X walikuwa na shauku ya kuona Waafrika 
wakijitawala na kuonyesha dunia kwamba weusi wanauwezo mkubwa wa 
kujitawala na ni binadamu kama binadamu wengine.
Kwa sasa ni miaka zaidi ya 50 tangu Bara la Afrika lianze kujitawala na 
naweza kusema itikadi za hawa magwiji kutaka Waafrika wajitawale 
zimejaribiwa ila swali je, tumeweza kujitawala kwa misingi bora ya 
demokrasia, utawala bora, kuondoa baa la njaa kila mara na kuacha 
utegemezi?
Ni nchi gani Afrika ambayo sio tegemezi? Hata zile zenye rasilimali 
zaidi ya nchi ya Italia, kama Tanzania bado zinategemea misaada kutoka 
kwa wakoloni (siku hizi mnawaita wafadhili).
Swali ambalo wengi tutakuwa tunajihuliza ni; je, kweli juhudi zote 
zilizofanywa na kundi hili la wapigania haki za watu weusi wakiwa na 
lengo la kuhahakikisha Mwafrika anapoachiwa ajitawale ataonyesha uwezo 
wake, zimefanikiwa?
Malengo yao ya kutaka mtu mweusi awe na taifa lake huru aonyeshe vipawa 
vyake vyote alivyopewa na Mwenyezi Mungu, yametimia? Bara la Afrika 
linatawaliwa na weusi kwa zaidi ya miaka 50, hivi kweli tumeweza 
kuonyesha uwezo wa mweusi kuudhihirishia Ulimwengu wa wazungu kwamba 
ndiyo tumeweza? Au ni kauli mbiu tu za kila mara kwamba tumedhubutu, 
tumeweza, tunasonga mbele?
Je, leo Marcus Garvey na Malcom X wakifufuka, wataweza kuwabeza wazungu 
kwamba si mnaona tuliwaambia mkiacha tujitawale tutaonyesha kwamba sisi 
ni binadamu kama nyie na uwezo tunao, na tangu mtuache weusi tuwe na 
nchi zetu huru haya ndiyo maendeleo tuliyonayo.
Au wazungu ndiyo watakaowabeza akina Garvey na Malcom kwamba tulijua 
weusi hawawezi kujitawala, kwa miaka zaidi ya hamsini tuwape Bara lenu 
bado mnatutegemea kwa kila kitu, mmeshindwa kuwalisha watu wenu, 
mnagombana wenyewe kwa wenyewe.
Nikifikiria Bara la Afrika lilipo kwa sasa, ni kwamba ndoto zote za hao 
magwiji wa haki za weusi hazijatimia kwa maana ya kuonyesha uwezo na 
kuweka heshima kwa mweusi katika nchi huru anayoitawala.
Bara la Afrika halijaweza kuonyesha thamani halisi ya Mwafrika na kuonyesha uwezo wa Mwafrika, huo ndiyo ukweli.
Haya ndiyo yaliyokuwa malengo ya akina Garvey na Malcom na weusi wengine
 waliokuwa utumwani, kujenga heshima ya mtu mweusi kwa kuonyesha uwezo 
katika nchi huru anayoitawala. Mwonekano uko wazi, bado taifa ni 
tegemezi.
Swala hili si kwa Marcus Garvey na Malcom X au jamii ya Wamarekani weusi
 tu waliokuwa na mtizamo kama wao bali ni kwa Waafrika ndani ya Bara la 
Afrika, waliokuwa na mitizamo kama hiyo, mfano, Kwame Nkrumah wa Ghana, 
Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Thomas Sankara wa Burkina Faso na 
Samora Machel wa Msumbiji, mlolongo ni mrefu wa Waafrika wenzetu 
waliojitoa kwa ajili ya Bara letu lakini hawako nasi kuona mwelekeo wa 
Bara hili na kuzidi kupotea kwa heshima ya mtu mweusi waliyokuwa 
wakiipigania na kuijenga, enzi zao.
Tunabaki tu na maswali kama wakifufuka iwe kwa wale waliopata uhuru kwa 
amani au mapinduzi pengine wakapewa nafasi ya mdahalo kama waliokuwa nao
 kipindi wakidai uhuru kutoka kwa wakoloni ni hoja hizi zipi wataingia 
nazo kutetea uhuru wa Mwafrika baada ya miaka 50? Je ni hoja kwamba 
binadamu wote ni sawa?
Ndio, inawezekana tuko sawa, watasema tuliwapa nchi zenu mzitawale, na 
je, uwezo wa kujitawala kwa ufanisi tumeuonyesha au bado ni mtindo ule 
ule wa kuwalaumu wazungu?
Kila mwaka tarehe ya kuadhimishwa uhuru inapofika kwa kila nchi Afrika, mbwembwe ni nyingi, sambamba na sherehe za gharama.
Sina hakika kama viongozi wetu huwashirikisha wananchi kutafakari 
madhumuni ya wapigania huru wetu na hadhi ya Mwaafrika ulimwenguni. Au 
ni mtindo ule wa kunywa mvinyo na kuthamini kuwapo kwao madarakani, 
kufurahia fursa za kukutana na marais au mawaziri wa nchi za kizungu na 
kupigiwa mizinga na kuandaliwa tafrija ughaibuni katika Ikulu za 
wenzetu. Je, hayo ndiyo yaliyokuwa madhumuni ya kudai uhuru?
Kwamba mtu mweusi anapigiwa mizinga ya urais Marekani na Uingereza, 
inawezekana rais huyo kutoka Afrika akaona hiyo ndiyo heshima na 
ukombozi kwa Mwafrika.
Ni hapo rais kutoka Afrika anapoulizwa kwa nini nchi yako ni masikini 
anajibu kwamba hata yeye haelewi ni kwa nini. Sasa kama rais haelewi na 
anakaa madarakani kwa miaka 10, inawezekana katika miaka 50 ya uhuru 
basi toa miaka 10, jibu utapata miaka 40 ya uhuru, na kama mtangulizi 
wake alikuwa haelewi basi toa tena miaka 10 unapata miaka 30 ya uhuru.
Kwa mtindo huu, kama watawala wetu hawaelewi kwa nini Bara letu bado ni 
masikini, ukitoa miaka yao katika miaka 50 ya uhuru wa Afrika 
inawezekana Bara letu likawa bado haliko huru; linaitaji wakombozi wapya
 wanaotambua kwa nini hili Bara ni masikini mbali na kujaaliwa 
rasilimali lukuki, wakombozi watakaoweza kutimiza malengo ya wapigania 
uhuru na haki za mtu mweusi popote pale dunia.
Ninatambua kwamba wako watu weusi wengi walioonyesha uwezo katika 
masuala mbalimbali kama uongozi, michezo, taaluma, lakini wachache hao 
hawawezi kuchukuliwa kama mfano kuonyesha kwamba weusi tumethubutu na 
tumeweza.
Heshima ya Mwafrika iko kwenye kuliendeleza Bara la Afrika, kukomesha 
majanga ya njaa ya kila mara na vita ya wenyewe, pia kuonyesha ukomavu 
wa demokrasia.
Hata hao wachache kwenye medani ya michezo wameonyesha uwezo wao nje ya 
Bara la Afrika na hii inaonyesha kwamba kama Bara tumeshindwa kuwa na 
mipango madhubuti kujiendeleza kimichezo, na hili si michezo tu hata 
kwenye taaluma.
Kwa upande wa uongozi wale waliothubutu kuonyesha uwezo wa kiuongozi 
kama Thomas Sankara wa Burkina Faso waliishia kuawa na Waafrika wenzao.
Je, kweli tumeweza kuonyesha kwamba Afrika huru imefikia au inaelekea 
kufikia malengo ya kutaka kujitawala kwa miaka hamsini ya uhuru wake na 
kuweka heshima ya mtu mweusi popote pale duniani?
Mwandishi wa makala haya, 
Mshobozi Kamugisha, ni msomaji wa Raia Mwema aliyeko North Carolina, 
Marekani. Anapatikana kwa namba ya simu; +19195368526 na baruapepe; 
klmu9@yahoo.com             
Post a Comment