Wananchi
wakivuka kwa taabu sehemu ambako daraja la bonde la Mbutu wilayani
Igunga linajengwa na kuondoa kabisa tatizo hilo mwaka huu ambapo ujenzi
huo unaofanywa na muungano wa makandarasi wa Tanzania unatarajiwa
kukamilika. Mpaka sasa asilimia 45 ya ujenzi wa daraja hili lenye
thamani ya sh bilioni 11.28 umekamilika na inakadiriwa kuwa litakuwa
tayari ifikapo Novemba mwaka huu.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo ya jinsi mashimo yatayosimikwa nguzo za daraja hilo yanavyochimbwa
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na mawaziri, wabunge na maofisa waandamizi
wa wizara na wakala wa ujenzi (TANRODS) pamoja na viongozi wa bodi ya
wakandarasi akikata utepe kuzindua rasmi ujenzi wa daraja hilo
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wengine wakipozi na umoja wa
wakandarasi wazalendo kutoka makampuni mbalimbali waliopewa kandarasi ya
kujenga daraja hilo.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa Serikali yake inakaribia kukamilisha ujenzi wa madaraja
yote 10 yaliyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na
ambayo yanagharimu mabilioni ya fedha.
Rais Kikwete amesema kuwa kati ya
madaraja hayo ambayo thamani yake inakaribia sh. bilioni 415, madaraja
mawili tayari ujenzi wake umekamilika. Madaraja hayo ni lile la Ruhekei
lililoko Wilaya ya Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma na Daraja la Mwatisi
katika Mkoa wa Morogoro.
Rais Kikwete amesema kuwa madaraja
mengine saba yanaendelea kujengwa, ikiwa ni pamoja na Daraja la
Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam linalogharimu sh bilioni 214.6, Daraja
la Kikwete katika Mto Malagarasi, Mkoa wa Kigoma unaogharimu sh bilioni
90.185, Daraja la Kilombero, Mkoa wa Morogoro linalogharimu sh bilioni
53.214 na Daraja la Rusumo, Mkoa wa Kagera linalogharimu sh bilioni
31.7.
Madaraja mengine yanayoendelea
kujengwa ni Daraja la Sibiti, Singida, linalogharimu sh bilioni 17.5,
Daraja la Nangoo, Mkoa wa Mtwara linalogharimu sh bilioni 4.29 na Daraja
la Maligisu, Mwanza, linalogharimu sh bilioni 2.51.
Amesema Rais Kikwete: “Madaraja
niliyotaja ujenzi wake ukikamilika, tutakuwa tumetimiza ahadi yetu ya
kujenga madaraja yote yaliyotajwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010
isipokuwa Daraja la Ruhuhu ambalo maandalizi yake ya ujenzi
yanaendelea.”
Rais Kikwete alikuwa anazungumza
wakati anaweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mbutu,
Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora katika sherehe ya kufanya iliyofanyika
Jumatatu, Januari 7, 2013.
Rais Kikwete amesema kuwa baadhi
ya madaraja yanayojengwa sasa na Serikali yalipangwa kujengwa katika
Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo mwaka 1968 lakini kwa bahati mabaya
hayakuweza kujengwa. Madaraja hayo ni Daraja la Kigamboni, Daraja la
Kirumi kwenye Mto Mara, Daraja la Rufiji, Daraja la Kilombero, Mkoa wa
Morogoro na Daraja la Kikwete kwenye Mto Malagarasi.
Awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi
yetu ilijenga Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara, Awamu na pili ikafanya
maandalizi na Awamu ya tatu ikajenga Daraja la Rufiji na Awamu ya sasa
inajega madaraja matatu yaliyobakia – Kilombero, Kigamboni na Kikwete.”
Daraja la Mbutu lina urefu wa
kilomita tatu, na linajengwa katika Bonde la Mbutu na litaunganisha
mikoa ya Tabora, Singida, Simiyu na Shinyanga.
Daraja hilo litakuwa na daraja
moja kubwa la mita 60 na madaraja mengine madogo saba na hivyo kufanya
urefu wa daraja lote kuwa na mita 165. Mpaka sasa asilimia 45 ya ujenzi
wa daraja hili lenye thamani ya sh bilioni 11.28 umekamilika na
inakadiriwa kuwa litakuwa tayari ifikapo Novemba mwaka huu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
7 Januari, 2013
Post a Comment