Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

WANANCHI WAUA TENA POLISI WAWILI


Mkuu wa majeshi Tanzania, IGP Said Mwema.
...........
Askari wawili wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, wameuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira na  gari lao kuchomwa moto, wakidhaniwa kuwa ni majambazi.
Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Kasheshemisha, Kata ya Rugu Wilaya hiyo juzi saa 2:30 usiku.

Akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Karagwe chini ya Mkuu wa Wilaya  hiyo,  Darry Ibrahim Rwegasira na ya Mkoa iliyoongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo,  Phillipo Kalangi na viongozi wengine wa serikali wilayani humo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasheshemisha, Sadick Mohammed, alisema walipata taarifa kutoka Kijiji cha Rugu kuwa kuna majambazi  walifika majira ya saa 12:00 jioni na wakati wakijaribu kuondoka, wanakijiji waliweka kizuizi barabarani na kuwaamuru wasimame.

Mihamed alisema watu hao hawakutii amri na kupita kwa nguvu katika eneo hilo ndipo walipoamua kupiga simu kwa mwenyekiti huyo ambaye naye alitoa taarifa  kwa wananchi wake na kuziba barabara kwa mawe.

Alisema  gari lao lilipofika Kijiji cha Kasheshemisha, lilikuta mawe barabarani na kushindwa kupita ndipo wananchi waliwaamuru  wajisalimishe, lakini walikaidi na kuanza kufyatua risari hewani huku wakitafuta njia ya kuwawezesha kutoroka.

Alisema walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili na kutokana na hasira ya kurushiwa risasi, waliwapiga hadi kuwaua kisha walipopekua ndani ya gari walikuta meno saba ya tembo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, hasira za wananchi zilipanda zaidi walipogundua mwenzao amejeruhiwa na risasi na kuamua kuyatoa meno hayo ya tembo saba na kulitekeleza gari  hilo lenye namba za usajili T.654 BNB.

Mohamed alisema mwanakijiji huyo, Jovinary Joseph aliyejeruhiwa na risasi kwenye kiganja, alikimbizwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Karagwe ya Nyakahanga kwa matibabu.

KAULI YA KAMANDA

Kamanda Kalangi aliwashukuru wakazi  wa Kijiji cha Kasheshemisha kwa ushirikiano waliounyesha katika kukabiliana na watuhumiwa hao.

Pia alitumia nafasi hiyo kuwaeleza  kuwa kila raia ana haki ya kuishi kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo aliwaasa na kusema si vema kujichukulia sheria mkononi kama walivyofanya.

Alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kufanyika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

DC AZUNGUMZA

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Darny Ibrahimu Rwegasira, aliwapongeza wakazi wa Kijiji cha Kasheshemisha na kuwataka kuimarisha zaidi kamati za ulinzi na usalama katika ngazi za kata, vijiji,vitongoji na mitaa.

Aidha, aliwaasa kutii amri halali mahali popote inapotolewa na kusema kuwa iwapo watuhumiwa hao wangetii amri walipotakiwa kusimama, huenda wasingefikwa na mauti hayo.
Askari waliokufa wametambuliwa kwa majina ya Sajenti Thomas Migiro na Koplo Damas Kashala kutoka Benako wilayani Ngara.
Askari mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Braiton, anadaiwa kujisalimisha katika kituo kidogo cha polisi.

MGANGA HOSPITALI YA WILAYA

Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo,  Dk.  Andrew Cesari, amethibitisha kupokea miili ya marehemu wawili ambao majina yao

hayakutambulika na kwamba uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa chanzo cha mauti hayo ni  majeraha.

Desemba 15, mwaka jana katika Kijiji cha Mugoma wilayani Ngara  ,  polisi wawili waliuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya  kufanya mauaji ya raia, Said Mkonikoni, hali iliyosababisha hasara kubwa ikiwani pamoja na kuteketezwa kwa moto kituo kidogo cha Polisi cha Mugoma.

Kadhalika, baadhi ya polisi wa mkoa wa kagera wameripotiwa kukamatwa jana wilayani Serengeti Mkoa wa Mara wakisafirisha meno ya tembo kinyume cha sheria.
Jeshi hilo limedai linaendelea na uchunguzi na kwamba itakapothibitika wahusika watafikishwa mahakamani wakati wowote.


KITUO CHANUSURIKA KUCHOMWA MOTO

Kituo Kidogo cha Polisi cha Kibirizi kilichopo mkoani Kigoma kimeponea chupuchupu kuchomwa moto na wanananchi wenye hasira kali baada ya askari wake kumuokoa Mary Ally (18) ambaye anatuhumiwa kumuua Mhitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Buronge iliyopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji,  Daniel Charles Sadamu kwa uchawi.

Shuhuda wa tukio hilo,  Athumani Mpeka  (40), mkazi wa Kibirizi, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 9 jioni eneo la Kibirizi baada ya Sadamu kufariki dunia ndipo wakachukua maiti na kuipeleka nyumbani kwa mtuhumiwa huyo na familia yote.

Mpeka alisema baada ya kufikisha maiti nyumbani kwa mtuhumiwa huyo, vurugu zilianza ndipo polisi walifika katika eneo la tukio na kuchukua mtuhumiwa huyo,  mama yake mzazi  na familia yote na kuwapeleka katika kituoni hapo kisha Kituo cha Polisi Mkoa wa Kigoma.

Alisema baada ya kuchukua familia hiyo, wananchi wenye hasira  na familia ya marehemu walivamia kituo hicho na kuanza kupiga mawe na kumjeruhi askari mmoja kwa kumpiga jiwe kichwani.

Alisema kana kwamba haitoshi, waliwasha moto ili wachome kituo  hicho kwa kuwahifadhi watuhumiwa hao kwa madai kuwa wamezidi kuua wanafunzi wengi katika eneo hilo kwa uchawi.

Alisema baada ya vurugu hizo, polisi walifyatua mabomu ya machozi hewani ndipo wananchi hao walitawanyika na kwenda kubomoa milango ya nyumba ya watuhumiwa kisha kuichoma moto na kuteketea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusisitiza wanafanya uchunguzi wa tuhuma hizo.

Kashai aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mary Ally (18), Joyce Elias (41), Benadeta Elias (15), Ally Willison (5), Elena Willison (8) na Elias Willison (10). Imeandikwa na Rama Maselle, Karagwe; Daniel Limbe, Chato; na Renatus masuguliko, Geita na Joctan Ngelly, Kigoma.

 
CHANZO: NIPASHE
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top