Francis Muthaura alikuwa mtumishi wa umma nchini Kenya
................
Mahakama ya kimataifa ya ICC inatupilia mbali kesi ya
uhalifu dhidi ya binadamu iliyokuwa inamkabili aliyekuwa mkuu wa
utumishi wa umma nchini Kenya Francis Muthaura.
Hii ni baada ya shahidi mkuu katika kesi hiyo kusema alitoa ushahidi wa uongo.
Muthaura alihusishwa na ghasia za
baada ya uchaguzi Kenya mwaka 2007 kwa kuwa mmoja wa wale waliopanga na
kufadhili mashambulizi ya uklipza kisasi dhidi ya jamii moja.
Kiongozi wa mashtaka, Fatou Bensouda alisema
anafutilia mbali mashtaka yote dhidi ya Francis Muthaura ambaye
anatuhumiwa kwa uhalifu ikiwemo mauaji na ubakaji baada ya kutokea
dosari katika ushahidi.
Wakati huohuo mawakili wa rais mteule wa Kenya
Uhuru Kenyatta nao wanatarajia baadaye leo kuwashawishi majaji katika
mahakama hiyo kudurusu ushahidi ambao viongozi wa mashtaka walitoa dhidi
ya Kenyatta kwa tuhuma kuwa alihusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa
mwaka 2007
Mawakili wa Kenyatta wanatarajiwa kutoa hoja yao
siku mbili baada ya Kenyatta kushinda uchaguzi wa urais , wa kwanza
kufanyika tangu ghasia za baada ya mwaka 2007.
Mawakili wanasema majaji wanapaswa kudurusu kesi
hiyo hasa baada ya shahidi mmoja kutoa ushahidi wa uongo na hivyo
kuhujumu kesi dhidi ya Uhuru na mshukiwa mwingine Francis Muthaura.
Kenyatta alishinda uchaguzi wa wiki jana licha
ya kesi anayokabiliwa nayo katika mahakama ya ICC kwa kosa la uhalifu
dhidi ya binadamu, ikiwemo mauaji, ubakaji na kuwalazimisha watu kuhama
makwao.
Viongozi wa mashtaka wanamtaja kama mmoja wa wahusika katika ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Kenyatta, ambaye ni mwanawe rais mwanzilishi wa
Kenya, Jomo Kenyatta ni mmoja wa watu matajiri wakubwa zaidi barani
Afrika na anasisitiza kuwa hana hatia.
Kesi dhidi ya Kenyatta itaanza mwezi Julai
Post a Comment