Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

KIBANDA AUMIZA VICHWA MADAKTARI


Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda
*Wabaini alivyovunjwa mfupa wa pua
*Wahaha kuokoa jicho,watu wazuiwa kumuona

JOPO la madaktari wanaomtibu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda katika Hospitali Mill Park, Afrika Kusini, wamebaini mfupa unaounganisha pua na mdomo kuwa umevunjika.

Habari zilizopatikana jana kutoka Afrika Kusini zinasema tangu juzi usiku, baada ya Kibanda kuwafikishwa hospitalini, jopo la madaktari lilianza kazi kuibaini matatizo yanayomsumbua zaidi.

“Tunashukuru mpaka leo (jana asubuhi),madakatari wamebaini tatizo jingine la kuvunjika mfupa unaounganisha mdomo na pua… tunaamini hii inaweza kuwa ilitokea wakati wa purukushani za kung’olewa meno baada ya kuvamiwa nyumbani kwake,”alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe.

Alisema baada ya kubaini tatizo hilo,madaktari hao wanahaha na vipimo kwa ajili ya kuangalia namna ya kuokoa jicho la kushoto la Kibanda ambalo linaonekana kuumia zaidi.

“Pia nimejulishwa na waangalizi wetu pale hasa mke wake Angela Semaya na Erick Kabendera, kwamba madaktari walikuwa wanahaha kuchukua vipimo vya jicho kuona ni namna gani wanaweza kuliokoa… kwa vile vipimo vimechukuliwa naomba tuendelee kumuombea,”alisema Bashe.

Alisema katika uchunguzi huo, jopo hilo jana lilitumia zaidi ya saa mbili, huku Watanzania au watu wa karibu wakizuiwa kuingia wodini kumjulia hali Kibanda.

Alisema hadi jana, Kibanda alikuwa na tatizo kubwa la kula chakula kutokana na maumivu aliyonayo kwenye koromeo.

“Nimeelezwa tatizo jingine ambalo linamkabili hivi sasa ni namna ya kula chakula. Inaonekana baada ya kuvunjika mfupa unaounganisha mdomo na pua mawasiliano ya kupokea chakula au maji yamekuwa tatizo…lakini aliweza kunywa juisi,”alisema Bashe.

Akizungumza na wafanyakazi wa kampuni hiyo jana, Bashe alisema aliwatoa hofu kwa kuwaeleza kuwa Kibanda ameanza kupatiwa matibabu, ikiwamo kufanyiwa uchunguzi wa kina kuhusiana na majeraha aliyopata.

“Kinachotia moyo zaidi ni kwamba nimezungumza na Kibanda mwenyewe na hata sauti yake inaonyesha kuwa ile hofu na mshtuko alioupata juzi imeanza kupungua,”alisema Bashe.

Alisema kingine kinachotia moyo ni jinsi madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili walivyotueleza kwamba majeraha aliyopata hayakupasua fuvu,jambo ambalo lingehatarisha zaidi uhai wake.

“Ni jambo la kushukuru,nilivyojaribu kudodosa madakatri pale hospitali walisema majeraha aliyopata hayakuweza kufika mbali au kupasua fuvu. Jeraha kubwa ambalo walikuwa na wasiwasi nalo ni lile la jicho.

“Na wenyewe juzi walifikia hatua ya kutaka jicho lile liondolewe ndiyo nikadodosa zaidi kitaaluma ili liondolewe ni lazima lichukue muda gani, walisema inawezekana kwa saa 72,” alisema.

Habari zaidi jana zilisema Mwenyekiti wa Taasisi ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi Afrika, Mzirikae aliyemtembelea Kibanda hospitalini jana, alisema chama hicho kitatuma timu ya waandishi kuja kuchunguza tukio hilo.

Alisema chama hicho kimepokea kwa mshutuko mkubwa tukio hilo na kinaamini uchunguzi wao utaisaidia waandishi kutoandamwa na matukio hayo.

Kibanda alivamiwa juzi nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam saa 6.00 usiku na watu wasiojulikana na kumpiga na kumjeruhi vibaya kwa kitu kinachosadikiwa kuwa na ncha kali.

Watu hao walimtoboa jicho, kumng’oa meno mawili ya mbele na kumjeruhiwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kelele zilizopigwa na mlinzi wake zilisaidia majirani kuamka na kuweza kumuokoa baada ya kumkuta akiwa ameburutwa zaidi ya mita 30 kutoka nyumbani kwake.

Juzi Mkuu wa Jeshi la Polisi,IGP Said Mwema alisema jeshi hilo limeunda timu ya watu wanne kutoka makao makuu ya polisi kitengo cha upelelezi kuungana na wapelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa ajili ya upepelezi wa tukio hilo la kinyama dhidi ya Kibanda.

Vilevile, taasisi na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Bilal, Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), walilani tukio hilo na kutaka wahusika wasakwe haraka na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

CHANZO:MTANZANIA
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top