JESHI
la Polisi nchini limekwama kumfikisha mahakamani Mkurugenzi wa Ulinzi
na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred
Lwakatare kwa madai ya kuendelea na uchunguzi.
Kukwama kwa jeshi
hilo ambalo jana lilitangaza kumfikisha Lwakatare katika Mahakama ya
Kisutu, kumezua tafrani kutoka kwa mawakili wake wakidai kuwa hatua hiyo
ni kinyume na sheria, ni unyanyasaji na ukandamizaji wa haki za
binadamu.
Mmoja wa mawakili wake, Nyaronyo Kicheere alisema
pamoja na polisi kumshikilia Lwakatare, wamemuweka katika mahabusu
isiyokidhi hali ya afya ya kiongozi huyo, ambaye anasumbuliwa na ugonjwa
wa kisukari.
“Hali ya Lwakatare ni mbaya, anaumwa kisukari,
anahitaji chakula kila baada ya saa nne, na kupata huduma ya haja ndogo
mara kwa mara, lakini amewekwa katika chumba ambacho hakina huduma ya
choo ingawa vinapatikana pale polisi.
“Ni kinyume cha sheria
kumweka mtu polisi saa zote hizo, na wanafanya vile utadhani huyu
wameshampata na hatia. Hatuwezi kuhamishia familia yake pale ili
wampatie chakula kila mara,” alisema.
Aliongeza kuwa juzi
alipotolewa kutoka katika chumba alipohifadhiwa alikuwa na hali mbaya
kiasi cha kushindwa kuongea au kusimama kwa kuwa alikuwa hajala kwa muda
mrefu kulingana na hali ya ugonjwa wake.
“Mtu wa aina hii sio wa
kuwekwa mahabusu muda mrefu, kwanza Lwakatare sio mtu wa kutoroka,
ukiachilia mbali suala la kisheria linalowalazimisha polisi kumpeleka
mahakamani ndani ya saa 24,” alisema Kicheere.
Akizungumza kwa
niaba ya mawakili wanaomtetea Lwakatare nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, kiongozi wa jopo hilo, Tundu Lissu alisema kitendo cha polisi
kutomfikisha mkurugenzi huyo mahakamani kama ilivyopangwa mapema jana ni
ukatili.
“Kama wanaendelea na upelelezi wangemfungulia mashtaka
hata ya kuokoteza tu ili apate dhamana ya mahakama kuliko kumtesa hivi,”
alisema Lissu.
Aliongeza kuwa polisi wameendelea kujichanganya
na kutupiana mpira kuhusiana na sakata hilo, jambo linalowafanya
wajiulize kulikoni.
Alifafanua kuwa alipoongea na mtu aliyeambiwa
ndiye anayekaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Hezron
Kigondo, alikana kutohusika na jambo hilo.
“Mimi nilipomuuliza
alisema ahusiki kabisa na suala la kumshikilia Lwakatare isipokuwa
anasimamia upelelezi wa suala lake tu, hivyo nimuulize Isaya Mungulu,”
alisema Lissu.
Kwamba alipozungumza na Mungulu naye alisema yuko
Mtwara, na kwamba hajui kabisa jambo hilo, akaomba ampigie tena baada ya
nusu saa.
Lissu anasema alipompigia tena Mungulu alisema “Jeshi
la Polisi litamshikilia Lwakatare hadi siku ya Jumatatu ndio
watamfikisha mahakamani” kauli iliyozusha zogo kubwa kwa mawakili hao.
Mawakili hao walisema majibu ya maofisa hao wa polisi yanadhihirisha namna walivyoshindwa kubaini kosa linalomkabili Lwakatare.
Walisema
huo ni ushahidi mwingine kuwa Jeshi la Polisi linajifanya liko juu ya
sheria na kwamba lina uwezo wa kunyanyasa watu kadiri linavyotaka.
Lissu
alisema ikifika Jumatatu polisi hawajamfikisha Lwakatare mahakamani,
basi wataongea na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, na
baada ya hapo watapeleka ujumbe kwa wananchi kuwa Jeshi la Polisi
halifuati sheria.
Mbali na Lissu na Nyaronyo, wakili mwingine
Professa Abdallah Safari alimtaka IGP Mwema aache kujiaibisha, kwani na
yeye ni mwanasheria, ni wakili kama wao, hivyo anajua kuwa ni kinyume na
sheria kumshikilia mtuhumiwa kwa muda unaozidi saa 24.
Lwakatare
anatetewa na jopo la mawakili wanne; Lissu, Prof. Abdallah Safari,
Kicheere na Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Peter
Kibatala.
Wabunge waliofika mahakamani jana kumwekea dhamana
Lwakatare ni Israel Natse (Karatu), Suzan Kiwanga na Naomi Kaihula (viti
maalumu), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa mjini) na Ezekiah Wenje
(Nyamagana).
Utata wa video
Katika hatua
nyingine, wakili Kicheere amezungumzia kile alichokiita utata wa video
iliyokamatwa na Jeshi la Polisi akisema ina walakini mwingi.
Kicheere
alisema video hiyo ambayo mteja wake alioneshwa ina kasoro nyingi na
tofauti na ile iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii.
“Mkanda
uliopo polisi kuna sehemu sauti inaongea, lakini picha imefunga mdomo,
na kuna sehemu midomo inafunguliwa hakuna sauti inayosikika. Huo mkanda
ni wa kutengeneza kabisa,” alisema.
Alidai kushangazwa na habari
zilizotolewa na gazeti moja la kila siku zikidai kuwa Lwakatare katika
video hiyo amemtaja mhariri mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis
Msaky, jambo alilosema ni uzushi.
“Katika mkanda huo, ulioko
polisi hakuna sehemu hata moja alipotajwa Msaky, sasa kama sio kuandaa
mazingira ya kuhalalisha ajenda zao ni nini?
“Sisi tunawasubiri wamlete Lwakatare mahakamani ili tujue waliohusika kuutengeneza mkanda huo,” alisema.
Kupekuliwa Bukoba
Msemaji wa Polisi, Advera
Senso alipohojiwa ikiwa hawaoni kama wanavunja sheria kwa kutomfikisha
Lwakatare mahakamani alisema; “sisi bado tunaendelea na utaratibu wa
upepelezi, hatujavunja sheria, tukikamilisha upelelezi tutamfikisha
mahakamani haraka, siwezi kuzungumza mengi maana nitakuwa navujisha
upelelezi.”
Kurekodi sauti bandia
Kwa
mujibu wa tafiti mbalimbali za wanasayansi, kuna uwezekano wa kurekodi
sauti bandia, huku video za mara kwa mara zilizorekodi sauti za viongozi
kadhaa maarufu duniani, akiwemo Osama bin Laden zikitolewa mfano.
Wanasema
sauti isiyokuwa na ubora pamoja na kuwepo kwa mabadiliko mbalimbali ya
sauti zisizohitajika ni dhahiri kuwa kanda za aina hiyo ni feki.
“Nchi
mbalimbali duniani zimekuwa zikigundua teknolojia ambazo zinaweza
kubadilisha sauti kwa haraka sana,” anasema mwanasaikolojia Jan van
Santen.
Mwanasaikolojia huyo anasema kutokana na sababu kuwa
teknolojia ya kubadilisha sauti imekuwa ikiongezeka na kukua kwa kasi
sana, ni vigumu kugundua kama sauti zinazorekodiwa ni halisi ama ni
bandia.
Anaeleza kuwa njia mojawapo inayotumika kwa sasa kuweza
kugundua uhalisi wa sauti hiyo ni kwa kuangalia alama maalumu zilizopo
kwenye vyombo vya kurekodia ambazo nazo pia hutegemea ni njia gani ya
ubadilishwaji wa sauti imetumika.
Dk. Alexander Kain ambaye ni
miongoni mwa watafiti kutoka katika shule ya OGI, kituo
kinachoshughulikia uelewa wa lugha ya matamshi, amegundua Mimics kuwa ni
njia mojawapo inayoweza kuiga sauti halisi kwa kutumia kigezo cha sifa
pekee iliyoko kwenye koromeo, njia ya matamshi pamoja na muziki maalumu
na ‘biti’ yake.
Anaeleza kuwa wanasayansi wengi wamegundua njia
mbalimbali za kubadilisha sauti ambazo ni rahisi sana kutumia na
vinapatikana kirahisi kwa kila mmoja kupitia vitabu pamoja na mtandao wa
Internet.
Ili kutumia na kufanikisha Mimic ni lazima sauti
halisi iliyorekodiwa ya mtu husika itambuliwe kwanza na baadaye atafutwe
mtu wa tofauti mwenye sauti sawa na mtu wa kwanza ambaye atasoma ama
kusema maneno yaleyale aliyosema mtu huyo bila kukosea.
Anasema
kuwa ni lazima mtu huyo afanye kazi hiyo kwa uhakika kiasi kwamba ni
vigumu kwa mtu yeyote kutambua ama kutofautisha kama sauti hiyo ni ya
watu wawili tofauti.
Chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment