MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Kazi, imemtaka Mwenyekiti wa Klabu ya
Yanga na Katibu Mkuu wake, Lawrence Mwalusako, wafike mahakamani hapo
leo kueleza kwa nini wasihukumiwe kifungo jela kutokana na kukaidi
hukumu ya kesi namba 203 ya mwaka 2011.
Katika hukumu hiyo, Yanga waliamriwa kuwalipa walalamikaji katika kesi
hiyo, kipa wake wa zamani, Stephen Marashi na beki raia wa Malawi,
Wisdom Ndlovu sh 106,000,000.
Marashi na mwenzake, wameiomba mahakama kumfunga jela mwenyekiti huyo
na katibu wake, baada ya timu hiyo kushindwa kutekeleza amri ya mahakama
iliyotolewa Februari 4, mwaka huu, ikiamuru kiasi hicho kulipwa.
Kwa mujibu wa barua ya wito iliyosainiwa na Msajili wa Mahakama hiyo,
Mohamed R. Gwae, Machi 21, kutokana na hayo, Manji na Mwalusako
wanatakiwa kufika mahakamani Machi 27, 2013 saa tatu asubuhi, kujieleza
kwa nini wasifungwe kwa kushindwa kutekeleza amri hiyo.
Yanga iliingia kwenye mgogoro na wachezaji hao, baada ya kuvunja nao
mikataba mwaka 2010 kutokana na sheria mpya ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), kuzitaka klabu kuwa na nyota watano tu kutoka nje, hivyo
kuwaacha Ndlovu, Mkenya John Njoroge na Mtanzania Marashi.
Katika hukumu hiyo ya Februari 4, mwaka huu, baada ya wachezaji hao
kufungua kesi ya kushinikiza kulipwa haki zao, Yanga ilitakiwa kuwalipa
ndani ya wiki mbili kuanzia tarehe ya hukumu.
Walalamikaji hao, mara ya kwanza waliishtaki Yanga Kamisheni ya
Usuluhishi na Upatanishi, ambako iliamriwa kulipwa fedha hizo, kabla ya
Yanga kutaka marejeo ambako walishindwa.
Njoroge kwa upande wake, suala lake liliamuliwa na Shirikisho la Soka
la Kimataifa (Fifa), lililoitaka Yanga kumlipa Njoroge sh milioni 17.
Tanzania Daima Jumatano, ilimtafuta Mwalusako kwa simu kuhusiana na wito huo wa mahakama, ambaye alidai hawajaupata.
NA TANZANIA DAIMA
Post a Comment