Ansaf Tanzania.
Jukwaa Huru la Kilimo nchini (Ansaf), limeshauri
kuwapo kwa kigezo cha walau kufaulu elimu ya kidato cha nne kama moja ya
sifa za kuwa diwani.
Ushauri huo uko kwenye ripoti ya jukwa hilo iliyotolewa juzi
jijini Dar es Salaam kufuatia utafiti lililoendesha kwa miaka mitatu
iliyopita katika wilaya sita nchini.
Utafiti huo ulifanyika katika wilaya za Karagwe, Tandahimba, Singida, Ulanga, Korogwe na Iringa.
Ripoti hiyo ‘Ufuatiliaji wa Uwajibikaji wa kijamii wa Sekta ya
Kilimo,’ inaainisha pamoja na mambo mengine, namna serikali za mitaa
katika ngazi za wilaya zinavyotenga kiasi kidogo cha bajeti kwenye sekta
ya kilimo, bila kuzingatia mchango wake kwenye uchumi.
Akizungumza wakati wa kutoa ripoti hiyo kwa wadau mbalimbali
wakiwamo waliotoka nje ya nchi, Mkurugenzi Mtendaji wa Ansaf, Audax
Rukonge, alisema kitendo hicho kinatokea kutokana na madiwani wengi kuwa
na elimu ya darasa la saba.
“Moja ya mambo yaliyogunduliwa na utafiti ni kilimo kutengewa fedha
kidogo ingawaje ndicho kinachotoa kati ya asilimia 20 hadi 60 ya mapato
ya vyanzo vya ndani ya wilaya, huku madiwani wakishindwa kuhoji,”
alisema.
Rukonge alisema pamoja na bajeti ndogo kutengwa kwenye sekta ya
kilimo na watendaji, ripoti hiyo imegundua pia kuwapo kwa matumizi
mabaya ya fedha za umma, huku madiwani ambao ni moja ya vyombo vya
udhibiti katika ngazi ya wilaya wakishindwa kuhoji.
Rukonge alisema wawakilishi hao wanashindwa kuhoji pale fedha
zinapohamishwa kwenda kwenye miradi isiyokusudiwa kutokana na kutokuwa
na ufahamu wa lugha zinazotumika kwenye bajeti kwa wengi wao wana elimu
ya msingi isiyowapa maarifa ya kuielewa lugha ya kifedha.
“Lakini wakati mwingine wanakosa taarifa za kutosha toka kwa
watendaji ili kuwawezesha kufuatilia matumizi, na kwa kuwa hawana elimu
stahili wanashindwa kuhoji, wakati suala la wao kupatiwa taarifa za
matumizi ni haki yao,” alisema.
Rukonge alisema kutokana na udhaifu huo, watendaji wa halmashauri
hutoa nyaraka za taarifa mbalimbali siku moja au mbili kabla ya kikao
cha madiwani, muda ambao hauwapi madiwani fursa ya kuzisoma na kuwa na
maswali ya kuhoji.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment