“Wengine wanasema si mapambano ya dini ya Kikristu na Waislamu ila ni
wahuni wachache wanajichukulia madaraka, lakini lolote liwavyo Serikali
haiwezi kukwepa majukumu yake, hatuwezi kutegemea nchi itawaliwe na
wahuni kama vile Serikali haipo.”
Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo amelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kile
alichosema kwamba limeshindwa kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani na
mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Kadhalika kiongozi huyo alihoji ulipofikia upepelezi wa mauaji ya Padri
Evarist Mushi wa Zanzibar aliyepigwa risasi mwezi uliopita huku akisema,
“Siwezi kusema naridhika au siridhiki lakini tulitegema kwamba polisi
wangetegua kitendawili cha wauaji wa padri huyo.”
Kardinali Pengo alisema Serikali haipaswi kusema wanaovuruga amani ni
wahuni wakati hilo ni jukumu lake kuhakikisha inadumisha amani. Pengo
alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam
wakati akitoa salamu za Pasaka.
“Watu wanaharibiwa mali zao, watu wanapoteza uhai wao, Serikali haiwezi
kukaa pembeni na kufikiri ni kauli za viongozi wa dini peke yao,
viongozi wa dini hawana jeshi au hawawezi kukamata watu, Serikali ndiyo
wana jukumu hilo kuhakikisha wanaingilia kati,” alisema Pengo na
kuongeza:
“Wengine wanasema si mapambano ya dini ya Kikristu na Waislamu ila ni
wahuni wachache wanajichukulia madaraka, lakini lolote liwavyo Serikali
haiwezi kukwepa majukumu yake, hatuwezi kutegemea nchi itawaliwe na
wahuni kama vile Serikali haipo.”
Kuhusu Padri Mushi aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kwenda kwenye misa huko Zanzibar, Pengo alisema:
“Watanzania tungeambiwa zimechukuliwa hatua zipi na aliyehusika na mauaji hayo ni nani, lakini hali inayoonekana sasa hatujui.”
Aliongeza: “Siyo mimi wala Askofu wa Zanzibar (Augostino Shao) au askofu
yeyote anaweza kukwambia kuwa kuna mtu amekamatwa, ila inaonekana kama
mambo yanataka kuisha kimyakimya na kufanya hivyo haiwezi kuwa chimbuko
la amani.”
Kardinali Pengo alisema vyombo vya kulinda amani vinapokuwa chimbuko la
kuharibu amani kwa vyovyote nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea.
Alisema kunahitajika kukutanishwa kwa pande zote mbili za Wakristu na
Waislamu, lakini akatoa angalizo kwa kubainisha mambo mawili ambayo
yanahitajika kuzingatiwa ili kufikia mwafaka.
Alisema pande zote mbili watu wakitaka kujadiliana ni lazima kila upande
uwe tayari kujadiliana na kupokea ukweli sambamba na kusema ukweli na
siyo kupotosha ukweli kwa masilahi binafsi.
“Pili kila upande uwe na mawazo kwamba upande wa pili una nia njema,
lazima watu wawe tayari kuwasiliana kuwa upande wa pili una nia njema,
lakini kinyume na hapo itakuwa bure na kudanganyana na mambo yataendelea
kuwa mabaya zaidi,” alisema Kardinali Pengo.
Kuhusu kuwapo kwa taarifa kwamba katika mkesha wa Pasaka kuna watu
watafanya vurugu, alisema haogopi kwani vyombo vya usalama vina jukumu
la kuhakikisha raia wanakuwa salama.
“Mimi kazi yangu si kujiandaa kushika bunduki kwani Serikali wana jukumu la kulinda amani iwe kanisani au msikitini.
“Wanatakiwa kuchukulia mazungumzo hayo ‘serious’ (makini) kwani baada ya
Padri Ambrose kujeruhiwa kwa risasi walisema wataendelea na kweli
ikatokea Padri Mushi akauawa. Mimi sitaacha kwenda kanisani hata kama
nitaambiwa nitauawa na kama kufa nife katika kanisa langu,” alisema.
Polisi wanena
Msemaji Mkuu wa Polisi, Advera Senso alisema upelelezi wa tukio la kifo
cha Padri Mushi unaedelea na kuwaomba wananchi kusubiri kujua
kinachoendelea.
“Kunapotokea tukio la aina yoyote lile polisi ndiyo jukumu lao kujua
chanzo na hatua za kuchukua. Tunaomba watu tuwaachie wanaohusika ili
kuweza kufanya kazi hiyo vizuri na tutawaeleza kinachoendelea upelelezi
utakapokamilika,” alisema Senso.
Kuhusu uvumi wa matukio ya uhalifu wakati wa Pasaka, Senso alisema wanafuatilia taarifa hizo.
“Tunawaomba wananchi ambao wanajua ni kina nani wanaeneza taarifa hizo,
watupe ushirikiano ili tuwachukulie hatua kutokana na kutoa taarifa za
kuhatarisha usalama wa wananchi,” alisema Senso.
Pia Novemba mwaka jana, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhili Soraga
alimwagiwa Tindikali na watu wasiojulika wakati akifanya mazoezi kwenye
Viwanja vya Mwanakwerekwe.
Mapema mwezi ulipita, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of
God (TAG) mkoani Geita, Mathayo Kachila aliuawa katika ugomvi wa
kugombea kuchinja, katika tukio ambalo watu sita walijeruhiwa vibaya kwa
mapanga.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
Post a Comment