WAKATI Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) likitangaza
kutoingiliwa kiutendaji na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, siri
zaidi za kuzama kwake zimefichuka.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Tanzania Daima Jumamosi, umebaini
TANESCO imekuwa ikiangushwa kutokana na uamuzi mbaya wa kisiasa
unaodaiwa kutolewa na viongozi wa juu wa wizara hiyo.
Jumatano wiki hii gazeti hili liliandika kuwa hali ya TANESCO ni mbaya
na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu
wa Wizara hiyo, Eliakimu Maswi, wanatajwa kuwa chanzo cha kudhohofika
kiuchumi shirika hilo kwa madai ya kuingilia shughuli za kiutendaji kwa
maslahi ya kisiasa.
Hata hivyo, siku moja baada ya habari hiyo, TANESCO inayoendeshwa kwa
hasara ya sh bilioni 90 kwa mwezi, ilitangaza katika vyombo vya habari
kuwa habari hiyo haina ukweli wowote wala mashiko, na kueleza umma kuwa
hakuna msuguano wala kukinzana kati ya menejimenti ya TANESCO na wizara.
Lakini nyaraka za mawasiliano baina ya shirika hilo na Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) zimebainisha namna
TANESCO ilivyolalamika kuingiliwa kiutendaji na wakubwa hao wa wizara.
Katika nyaraka hizo, TANESCO walisema bayana kutopenda kabisa uamuzi wa
wizara ambao unafanywa kisiasa, bila kuzingatia utaalamu wakati wa
sakata la kutaka kupandisha bei ya umeme.
Ushauri wa kitaalamu ambao ulizingatia sababu za TANESCO kutopendezwa na
uamuzi wa kisiasa ulifikishwa kwa maandishi kwa Mkurugenzi Mkuu wa
Ewura, Haruna Masebu Jan, 16, mwaka huu.
TANESCO katika mawasiliano yake na Ewura iliweka wazi namna
“isivyopendezwa hata kidogo na uamuzi wa serikali, na inaona hakuna
uwezekano wa kusikilizwa kila inapopeleka suala hili na kuelezea madhara
yatakayopatikana baada ya kuondoa maombi ya dharura ya kupandisha
ushuru”.
TANESCO katika maelezo yake, ilitoa sababu nne; kwanza ikisema kiwango
cha ruzuku kinachopangwa na Ewura kilionesha kuwa hakutakuwa na
mabadiliko ya kupanda na kushuka kwa thamani ya fedha, kwa mantiki hiyo
hata kama ushuru huo ungetumika usingeisaidia TANESCO.
“Hali ya hewa pia siyo nzuri, kuna upungufu wa mvua unaosababisha
upungufu wa maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme, hivyo zitahitajika
pesa nyingi sana ili kuwezesha ununuzi mafuta au umeme katika mwaka
2013.
“Mtiririko wa fedha kutoka serikalini haupo sanjari na mahitaji ya
uendeshaji wa TANESCO, na mara nyingi serikali huchelewa kutoa pesa,”
ilisema sehemu ya mawasiliano baina ya pande hizo mbili.
Shirika hilo liliongeza kuwa, mkopo kutoka Benki ya Dunia utatumika
kulipa madeni tu wala sio kuisadia TANESCO, hivyo kwa mtazamo huo,
utaratibu wa serikali wa kutoa ruzuku inayotosheleza mwaka mzima,
unaweza kufanyika bila kupandisha bei ya umeme, lakini ubuniwe utaratibu
mwingine utakaofanya TANESCO iendelee kuonekana kwa macho ya watu kama
vile bei imepandishwa, lakini bila kuondoa maombi ya kutopandisha ambako
kutazidisha shaka kwa wadau wengine mfano wawekezaji na wabia wa
maendeleo.
Wiki hii gazeti hili lilimnukuu Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Felchesmi Mramba,
akisema kuwa hakuna mgawo wa umeme kwa sasa, na kwamba ikitokea
serikali itatangaza.
Hata hivyo, kukatika kwa umeme kwa siku nzima katika baadhi ya sehemu kunadhihirisha uwepo wa mgawo wa siri unaoendelea.
Pamoja na kukanusha kuwepo kwa mgawo, Mramba alikiri kuwa hali ya umeme
haijarejea katika uhalisia wake wa kawaida kiasi cha kuondoka katika
hali ya dharura.
“Bado mitambo ya dharura tuliyokodi kupambana na hali ya umeme
inaendelea kuhitajika, lakini pia mabwawa hayana maji ya kutosha kukidhi
mahitaji ya umeme bila kuhitaji mitambo ya matufa,” alisema.
Mramba alibainisha kuwa tangu Julai mwaka 2012 hadi Februari 2013,
serikali imetumia jumla ya sh bilioni 231.2 kama ruzuku kwa TANESCO kwa
ajili ya kununua mafuta ya mitambo.
“TANESCO kutoka kwenye mapato yake imetumia jumla ya sh bilioni 423.3
katika kipindi hicho kununulia mafuta, hivyo fedha yote iliyotumika
kununulia mafuta ndani ya kipindi hicho ni sh bilioni 654.5,” alisema
Mramba.
Kauli ya Mramba inaonesha kuwa hata kama TANESCO ingeamua isilipe
mishahara wala isifanye matengenezo ya mitambo, isinunue vifaa vya
kuunganishia wateja, au isiingie gharama nyingine zozote, bado ingepata
hasara ya karibu sh bilioni 90 kila mwezi.
Chanzo chetu kutoka Ewura kimesema kuwa walishangazwa na uamuzi wa
TANESCO wa kujitoa katika mazungumzo ya kupanda kwa bei ya umeme kwa
kiasi kidogo na kwenye upungufu ruzuku ya serikali iweze kufidia, kwa
madai ya kutekeleza maelekezo kutoka wizarani.
Chanzo hicho, kimekiri wazi kuwa kuna mgawo wa umeme ingawa haujatangazwa rasmi.
“Mgawo upo ingawa haupo katika ratiba, ila tukiwauliza TANESCO ambao
ndio wasemaji wanadai ni tatizo la miundombinu, au maji hayatoshi na
kweli kwa sasa maji hayatoshi Mtera na kama hali ikiendelea hivi hivi
Mtera itafungwa.
“Kwa sababu mvua za Januari hadi Machi zinazotegemewa hazikunyesha
vizuri, na bado maji machache tunayopata toka Mto Ruaha Mkuu na Ruaha
Mdogo tunagawana na wakulima wa mpunga walio katika bonde la Usangi,
hapo ndiyo tunajiuliza tutoe maji kwa ajili ya mpunga au kwa ajili ya
umeme?” kilisema chanzo chetu.
Chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment