TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri Mkuu wa Denmark, Mhe. Helle
Thorning-Schmidt anatarajiwa kuwasili nchini tarehe 05 Machi, 2013 kwa ziara ya
kitaifa ya siku nne. Ziara hiyo ya Mhe. Thorning-Schmidt
inafuatia mwaliko wa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Mhe. Thorning-Schmidt ambaye anatarajiwa
kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 05 Machi,
2013 saa 12:45 jioni atapokelewa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania,
Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.
Akiwa
hapa nchini, Mhe. Thorning-Schmidt atafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Rais
Kikwete tarehe 06 Machi 2013 na baadaye kwa pamoja na Mhe. Rais Kikwete
watakutana na Waandishi wa Habari, Ikulu, Dar
es Salaam.
Aidha,
siku hiyo hiyo ya tarehe 06 Machi 2013, Mhe. Thorning-Schmidt atatembelea Meli
ya Kijeshi ya Denmark
ya Iver Huitfeldt ambayo imetia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam tarehe 1 Machi, 2013 na kuzungumza na
Mabaharia katika meli hiyo.
Mhe.
Thorning-Schmidt pia anatarajiwa kutoa Mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam siku hiyo ya tarehe 6 Machi, 2013 kuhusu Elimu na Maendeleo kabla ya
kushiriki Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu, Dar es Salaam.
Mhe.
Thorning-Schmidt ataondoka Dar es Salaam tarehe 7 Machi, 2013 kuelekea Arusha
ambako ataendelea na ziara yake kwa kutembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni
pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Kijiji
cha Wamaasai cha Lepurko na kukutana na Waandishi wa Habari.
Akiendelea
na ziara yake Mkoani Arusha tarehe 8 Machi, 2013 Mhe. Thorning-Schmidt
atatembelea Shamba la Kahawa linalomilikiwa na Bw. Christian Jespen lililoko
pembezoni mwa Bonde la Ngorongoro na baadaye anatarajiwa kutembelea Hospitali
ya Wilaya ya Mbulu.
Aidha
siku hiyo hiyo, Mhe. Thorning-Schmidt anatarajiwa kutembelea Makao Makuu ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo atakuwa na mazungumzo na Katibu Mkuu
wa Jumuiya hiyo, Dkt. Richard Sezibera. Mhe. Thorning-Schmidt pia atatembelea
Kituo cha Mafunzo kinachofadhiliwa na Serikali ya Denmark
cha Mellemfolkeligt Samvirkes, MS-TCDC
kilichopo Usa River.
Mhe. Thorning-Schmidt anatarajiwa kuondoka hapa nchini
tarehe 08 Machi 2013 kupitia Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kurejea nchini kwake Denmark.
IMETOLEWA
NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.
04
MACHI, 2013
Post a Comment