MAKUNDI maarufu ya muziki wa bongo fleva, TMK Wanaume Family na
TMK Wanaume Halisi yanatarajiwa kuchuana katika mpambano uliobatizwa kwa
jina la ‘NANI MKALI’ unaotarajiwa kufanyika Machi 31 kwenye ukumbi wa
Dar Live uliopo Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mratibu wa mpambano huo
Abdallah Mrisho alisema kwamba lengo ni kumtafuta mkali kati ya makundi
hayo yenye historia ndefu, si kwa Wilaya ya Temeke tu bali Tanzania
nzima kwa ujumla.
Alisema kwa muda mrefu makundi hayo yamekuwa katika ushindani mkubwa
wa kisanii, hivyo kupitia mpambano huo mashabiki watakaojitokeza
watapata kushuhudia wenyewe kazi zao jukwaani, kabla ya kuamua nani
mkali.
Alisema kundi la TMK Wanaume Family linaloongozwa na Said Fella
linaundwa na wasanii kama Chegge, Dogo Aslay, Mh. Temba, Bibi Cheka na
wengineo, huku Wanaume Halisi lililopo chini ya Abdallah Mashoto
linaundwa na Juma Nature, Inspector Haroun, JB, Dollo na wengineo.
Naye kiongozi wa TMK Wanaume Family, Fella akizungumzia mpambano huo
alisema kwamba ni nafasi nzuri kwa mashabiki wa muziki wa bongo fleva
kuona kundi lipi ni bora kati ya hayo.
“Tunafurahi kuwepo kwa mpambano huu ambao utatoa picha halisi ya nani
ni nani baada ya mabishano ya muda mrefu kwa kila upande kudai ni bora
zaidi,” alisema.
Kwa upande wa TMK Wanaume Halisi, kiongozi wake Mashoto pamoja na
kushukuru kwa kuwepo kwa mpambano huo, alisema pia itadhihirisha kwamba
makundi hayo hayana uhasama kama inavyoaminiwa na wengi.
Alisema wasanii wake kwa sasa wapo katika maandalizi ya mpambano huo,
hivyo amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kuweza
kupata jibu la nani ni mkali.
Aidha, mpambano huo ambao utasindikizwa na wasanii nguli nchini
wakiwamo malkia wa taarabu, Khadija Kopa na mkali wa Hip Hop Profesa J,
kiingilio ni sh 10,000.
NA TANZANIA DAIMA
Post a Comment