Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa
.............
Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, amesema
serikali haitaathirika wala kuyumba katika bajeti yake ya mwaka
2013/2014 kutokana na mabadiliko ya Bunge la bajeti la mwaka huu.
Bunge la bajeti litakaa kwa ajili ya kuidhinisha matumizi ya
serikali Aprili mwaka huu, iwapo wabunge watapitisha mabadiliko hayo ya
ratiba ya vikao vya bajeti baada ya mchakato mzima wa kupitia na
kurekebisha kanuni za Bunge kukamilika.
Kabla ya kauli ya Waziri Mgimwa, baadhi ya watu wamekuwa
wakionyesha wasiwasi kama washirika wa maendeleo ambao huchangia katika
bajeti watakuwa tayari kufanya kuchangia kutokana na mabadiliko hayo.
“Wafadhili wanaochangia bajeti ya serikali hawana tatizo wala
kizuizi na suala la mabadiliko hayo ikiwa wenyewe tutabadili ratiba ya
bunge la bajeti kwa mwaka wa fedha 2013/2014. Lakini kikubwa ambacho
ndio nia ya serikali ni kuhakikisha kwamba bajeti inayopitishwa na Bunge
inaanza kutumika rasmi Julai mosi na si kama ilivyozoeleka huko nyuma
kwamba bajeti huanza kutumika baada ya bunge la bajeti kuhitimishwa
mwezi Agosti,” alisema Dk. Mgimwa.
Alisema nchi wahisani ambao huchangia bajeti ya serikali kila mwaka bado wataendelea kuchangia bajeti hiyo.
Kwa mujibu wa Dk. Mgimwa, serikali imepanga kuondoa uchelewashaji
katika utekelezaji wa matumizi ya bajeti ambayo mara nyingi hushindwa
kuanza kutumika Julai mosi ambao ni mwaka mpya wa fedha wa serikali
kutokana na ratiba ya vikao vya bunge la bajeti kuhitimishwa Agosti.
Kwa kawaida Bunge la bajeti ambalo huidhinisha matumizi mbalimbali
ya serikali huanza vikao vyake Juni na kuhitimishwa Agosti kila mwaka.
“Kwa ujumla wake, hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya bajeti ya
serikali kwa mwaka wa fedha 2013/2014 mpaka hivi sasa ni kwamba
wataalamu kule wizarani wako kwenye hatua ya Consolidation (uunganishaji
wa taarifa ya bajeti) na huenda Bunge likaanza Aprili 9, mwaka huu,”
alisema Dk. Mgimwa.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment