Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

TUME YA PINDA HAINA JIPYA

HATIMAYE tume ya kuchunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka 2012, iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, imetoa taarifa yake. Tume hiyo imebaini sababu zilizochangia matokeo hayo kuwa mabaya ni upungufu wa walimu na matumizi ya vitabu vilivyopitwa na wakati.
Sababu nyingine ni usimamizi dhaifu katika sekta ya elimu, pamoja na uhaba wa bajeti, sababu ambazo zimezoeleka na zilikuwa zikijulikana kabla ya tume hiyo kuundwa.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Sifuni Mchome, wakati akitoa matokeo ya awali yaliyofanywa na tume hiyo kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam.

Profesa Mchome alisema tume hiyo haitadharau kutumia maoni yalitolewa bungeni na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), kwa ajili ya kunusuru sekta ya elimu.

“Tume imepata maandiko, taarifa na nyaraka mbalimbali kutoka ofisi ikiwamo mikoa na wilaya ambazo tayari zimeshafanya vikao kwa ajili ya suala hili na taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali, ili kusaidia katika utekelezaji wa majukumu ya tume.

“Hadi sasa tumepokea ujumbe mfupi wa maandishi zaidi ya 300, email hazihesabiki, maoni kwenye tovuti zaidi ya 300, simu zaidi ya 1,000 na walimu na wanafunzi zaidi ya 40 katika kila shule, kwa mantiki hiyo ni zaidi ya maelfu ya watu wametoa maoni yao kwa upande wa Dar es Salaam pekee.

“Tulifanya mahojiano na chama cha wamiliki wa shule binafsi, Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSA) Kanda ya Dar es Salaam, Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

“Wengine ni viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kama vile kaimu kamishana wa elimu, wakurugenzi wa idara za elimu ya msingi na elimu ya sekondari.

“Tumefanya mahojiano ya awali na Baraza la Mitihani Tanzania, Taasisi ya Elimu Tanzania, wakuu wa shule, baadhi ya walimu na wanafunzi wa shule za sekondari zilizopo Ilala, Kinondoni na Temeke na wananchi mbalimbali.

“Kutokana na mahojiano hayo ya awali tumebaini kuwa tatizo la uhaba wa walimu, uhaba na uchakavu wa majengo sambamba na nyumba za walimu pia ni chanzo cha kushuka kwa ufaulu.

“Kuhusu mitaala tumechukua sample kwa mamlaka husika na tunaendelea kuzifanyia kazi, huku tukiendelea kusubiri watupatie taarifa tulizowaagiza.

“Pia tumebaini usimamizi duni katika sekta hii pamoja na uhaba wa bajeti ni mojawapo ya chanzo cha kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mtihani huo,” alisema Profesa Mchome.

Alisema kwa sasa wajumbe wa tume yake wamesambaa mikoani kulingana na ratiba ambayo ni Mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Manyara, Arusha, Morogoro, Pwani, Simiyu, Shinyanga na Mbeya.

Alisema maoni yote yanayoendelea kutolewa na watu mbalimbali yanaendelea kufanyiwa kazi, hivyo akawataka wananchi wasisite kuendelea kutoa maoni yao kwa ajili ya kunusuru sekta ya elimu nchini.
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top