- Waliokufa wafikia 31, JK atembelea majeruhi
Sitta ambaye pia ni Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana, alipotembelea eneo la ajali
kuwapa pole wafiwa waliopoteza ndugu zao, akisema kama sheria na kanuni
za ujenzi zingezingatiwa tukio hilo lisingetokea.
Alisema kinachosikitisha katika nchi hii ni kushuka kwa maadili,
tukio alilodai kuwa limesababishwa na mafisadi wanaotamani faida kubwa
kila kukicha bila ya kujali maisha ya watu wengine.
Sitta alifafanua kuwa ili kudhibiti matukio hayo ni lazima serikali
ihakikishe inasimamia sheria na kanuni za ujenzi ili kuepuka nchi kuwa
na majengo mabovu ambayo matokeo yake yanasababisha majanga.
“Ni dhahiri kanuni katika ujenzi wa jengo hili hazikusimamiwa
ipasvyo, hivyo ni wakati kwa serikali kufanya uchunguzi wake ili
kuwabaini mafisadi wote waliosababisha tukio hili la kusikitisha,”
alisema.
Kwa mujibu wa Sitta, sekta zote nchini zinakabiliwa na mporomoko wa
maadili kwa baadhi ya watendaji kujijengea ujasiri usiofuata sheria
kwa kufanya kazi watakavyo.
Alisema ili kumaliza vitendo hivyo viovu vinavyofanywa na baadhi ya
watu wachache, Watanzania wanahitaji mjadala mpana ili kurudisha
maadili yaliyotoweka katika jamii.
“Siku hizi vitendo vya wizi vimekuwa vya kawaida kwa mfamo hivi sasa
Tanzania ndiyo nchi inayoongoza Afrika Mashariki kwa wizi kwenye ATM,
pia wengine wanaibiwa kwenye daladala mchana kweupe na hakuna
anayejali.
“Tunahitaji mabadiliko ya fikra mpya ili tuweze kumaliza vitendo hivi
vya kushuka maadili katika jamii yetu ya Kitanzania,” alisema Sitta.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik alilitaka Shirika
la Nyumba la Taifa (NHC) kusimamia shughuli zote za mazishi ya watu
waliofariki katika tukio hilo kwa sababu vimesababishwa na mbia wao
Raza Damji.
Pia alilitaka shirika hilo kusimamisha mikataba ya nyumba tatu ambazo
wapangaji wake wametakiwa kuhama ili kupisha uchunguzi wa kuzibaini
kama ziko hatarini kutokana na mtikisiko uliotokana na kuporomoka jengo
jirani.
Alizitaja nyumba hizo kuwa ni zile zilizoko kwenye vitalu Na. 2083/73, 1210/73 na 1960/73.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
alisema hadi sasa watu wanane wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa
ajili ya uchunguzi wa kuporomoka kwa jengo hilo.
Watu hao ni Raza Damji, Ogare Salu, Goodluck Mbaga, Ally Damji, Ibrahim Kisoki na wengine.
Aidha, amesema kuwa majeruhi waliobaki Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni wanne baada ya wengine sita kuruhusiwa.
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete aliwatembelea majeruhi wa
ajali hiyo waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili
kuwafariji.
Mbatia: Dar si salama
Mbunge wa kuteuliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha
NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alibainisha kuwa jengo hilo lililoporomoka
ni miongoni mwa majengo ambayo yanasubiri kuliangamiza Jiji la Dar es
Salaam hasa Kariakoo.
Mbatia ambaye pia ni mtaalamu wa kupambana na majanga, alisema
majengo mengi yaliyopo katikati ya jiji hasa Kariakoo ni janga kubwa
ambalo litapoteza watu wengi kama hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Katika Jiji la Dar es Salaam karibuni majengo yote makubwa yapo
kwenye hatari ya kuleta majanga endapo ikitokea tetemeko kidogo tu, na
itasababisha vilio,” alisema.
Aliitaka serikali kuchukua hatua za kuwaondoa wananchi kwa muda na
kuwahifadhi sehemu maalumu ili uchunguzi wa kina ufanyike kwa majengo
yote kubaini yasiyokidhi viwango.
Mbatia pia alilishukia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa nalo
libanwe kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka ikiwemo kutokagua
vifaa vinavyotumika kwenye majengo mengi.
Alisema kitaaluma TBS inatakiwa kuchunguza bidhaa muhimu ikiwemo
nondo na saruji ambazo nyingi zimekuwa zikitumika bila kukaguliwa na
hata kusababisha majanga ya kujitakia kama hilo.
NA TANZANIA DAIMA
Post a Comment