TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeibua mtafaruku mkubwa wa 
kisiasa mjini Arusha, baada ya kutangaza kata nne kufanya uchaguzi mdogo
 na kuiacha Kata ya Sombetini ambayo aliyekuwa diwani wake, Alphonce 
Mawazo (CCM) alihamia CHADEMA.
  Ratiba hiyo iliyotangazwa juzi na Mkurugenzi wa NEC, Julius Mallaba 
inaonesha kuwa uchaguzi huo mdogo utafanyika katika kata 26 kwenye 
halmashauri 21 zikiwemo nne za Arusha Mjini za Kimandolu, Elerai, 
Kaloleni na Themi.
  Madiwani wa kata hizo nne walivuliwa uanachama na chama chao cha 
CHADEMA baada ya kukiuka taratibu na katiba huku Kata ya Sombetini ikiwa
 wazi baada ya Mawazo kujiondoa CCM.
  Hata hivyo, taarifa ya NEC kutoiingiza Kata ya Sombetini katika ratiba
 ya uchaguzi mdogo, imeibua hisia mbaya za kisiasa huku CHADEMA wakidai 
ni mkakati wa kuilinda CCM ili isiipoteze kata hiyo.
  Kumekuwa na madai kuwa Mawazo hakuwahi kuandika barua ya kuitaarifu 
NEC kuwa alijiuzulu udiwani na kuhama CHADEMA, jambo ambalo 
alilikanusha.
  Akizungumza na gazeti hili jana kwa simu, Mawazo alisema amesikitika 
kuona tume hiyo haitangazi uchaguzi katika kata hiyo wakati alishahama 
CCM kwa kuandika barua kwa viongozi wa Manispaa ya Arusha.
  Alipotafutwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema 
wao wanafuata utaratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na 
Serikali za Mitaa (Tamisemi).
  Hata hivyo alisema kuwa watawasiliana na Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia ili aweze kulitolea ufafanuzi suala hilo.
  Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema aliliambia gazeti hili jana kuwa
 NEC inafanya kazi kwa maelekezo ya CCM, jambo ambalo linaashiria kuwa 
hakuna utawala bora nchini.
  “Tume inashirikiana na CCM kupanga ni uchaguzi upi ufanyike lini na 
upi usifanyike kwa maslahi ya kuilinda CCM, na mimi kama mbunge 
ninahitaji uwakilishi wananchi wa Sombetini, tume isifanye siasa,” 
alisema.
  Kata zingine na halmashauri zake kwenye mabano ni Stesheni 
(Nachingwea), Nyampu Lukano na Lugata (Sengerema), Genge Tingeni 
(Muheza), Ibugule (Bahi), Langiro (Mbinga) na Manchila (Serengeti).
  Nyingine ni Iyela (Mbeya), Mbalamaziwa (Mufindi), Ruzewe Mashariki 
(Bukombe), Mianzini (Temeke), Dalai (Kondoa), Minepa (Ulanga), Makuyuni 
(Monduli), Bashnet (Babati), Iseke (Singida), Dongobesh (Mbulu), 
Ng’ang’ang’e (Kilolo), Ifakara (Kilombero), Msanze (Kilosa) na Mnima 
(Mtwara).
  Mbali na uchaguzi huo wa madiwani, pia tarehe hiyo, Juni 16 mwaka huu,
 NEC imetangaza uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Chambani-Pemba 
kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Salum Hemed Hamisi aliyefariki 
Machi 28, mwaka huu.
NA TANZANIA DAIMA 
      
Post a Comment