Rais wa Marekani, Barack Obama
Mbali na tahadhari hiyo, ziara hiyo ya
Obama itakuwa na ulinzi mkubwa ambao pengine haujawahi kutokea katika
historia ya viongozi wa nje wanaotembelea Tanzania kwani utahusisha
idadi kubwa ya magari, ndege za kijeshi na meli kubwa ya kivita ambazo
zitakuwa zikifanya doria karibu na pwani ya Tanzania.
Tahadhari za matumizi ya chakula, maji
na nyinginezo zimetolewa katika nchi zote tatu za Afrika ambazo Obama
atatembelea, kila moja kwa jinsi Wamarekani hao wanavyoitathmini.
Rais Obama atatembelea nchi za Tanzania, Senegal na Afrika Kusini.
Ulinzi
Vyombo vya usalama vya Marekani
vimejipanga kuhakikisha ziara ya kiongozi huyo haivurugwi kwa namna
yoyote ile. Tayari ndege za jeshi zilizobeba magari ya akiba 56,
yakiwemo 14 aina ya ‘Cadillac One’ maalumu kwa ajili ya kiongozi huyo,
yamewasili katika nchi hizo tatu za Afrika atakazotembelea.
Kwa mujibu wa gazeti la Washington
Post la Marekani, ndege hizo pia zimebeba malori matatu ambayo
yamesheheni karatasi maalumu za kuzuia risasi kupenya kwenye vioo,
zitakazobandikwa kwenye madirisha ya hoteli ambazo Rais Obama na ujumbe
wake watafikia.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, mamia ya
mashushushu wa Marekani tayari wako katika nchi hizo. Meli maalumu za
kubeba ndege za kivita, maarufu kwa jina la ‘amphibious ship,’ ikiwa na
hospitali maalumu na yenye vifaa vyote itaweka nanga baharini, jirani na
nchi atakayokuwa Rais Obama, tayari kukabiliana na dharura yoyote
itakayotokea. Gazeti hilo liliandika kuwa ndege za kivita za Marekani
zitakuwa zikipeana zamu kufanya doria kwa saa 24, katika anga la nchi
ambayo Rais Obama atakuwepo, iwapo ndege za ‘adui’ zitakaribia eneo
linaloitwa ‘anga ya rais.’ Kwa mujibu wa gazeti hilo, ziara ya Rais
Obama aliyoifanya hivi karibuni katika nchi za Ujerumani na Ireland
Kaskazini, japo kulikuwa nagharama kwa walinzi, lakini safari za nchi za
Afrika zimeelezwa kuwa na gharama kubwa zaidi.
Tahadhari
Kwa mujibu wa taarifa ya maelekezo ya
Ikulu ya Marekani, ambayo Mwananchi imepata nakala yake, watu
watakaokuwa kwenye msafara wa Obama wametakiwa kutotumia kachumbari. Pia
imewataka kutumia maji ya chupa zaidi.
“Kutokana na mfumo wa maji uliopo,
tunashauri watu wetu kutumia maji ya chupa zaidi kwa kunywa na hata kwa
kupiga mswaki,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa kuelewa fika tatizo la ugonjwa wa
malaria nchini, ujumbe wa Obama umeshauriwa kutumia dawa ya mbu ya
kupaka na kupuliza inayoitwa Deet.
Deet ni dawa maarufu huko Marekani na
ikiwa katika aina tofauti ikiwamo ya kupaka na kupuliza na imekuwa
ikitumiwa na jeshi la Marekani kwenye vita mbalimbali tangu miaka ya
1940 kabla ya kuanza kutumiwa na raia mwaka 1957.
ATM nazo noma
Pia watu watakaokuwa kwenye msafara wa
Rais Obama wametakiwa kuhakikisha wanatumia mashine za kutolea fedha
(ATM) zilizoko karibu na hoteli watakazofikia.
“Kuna tatizo la uhalifu kwa hiyo siyo
vizuri kutumia ATM ambazo ziko katika sehemu zisizo salama. Pia katika
kipindi watakachokuwa Tanzania watu wanapaswa kutumia teksi ambazo
zimeidhinishwa na hoteli.
“Pia siyo vizuri kuacha kompyuta ya
fedha kwenye vyumba mtakavyolala. Pia kina mama wanapaswa kuchukua
tahadhari ya mabegi yao watakapokuwa wanapita mitaani,” ilitahadharisha
taarifa hiyo.
Chanzo: mwananchi.co.tz
Post a Comment