Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe amewashauri watu
walioko mikoani kusitisha safari za kuja Dar es Salaam wakati wa ziara
ya Rais wa Marekani, Barrack Obama kutokana na wingi wa wageni katika
jiji hilo.
Ugeni huo pamoja na ule wa viongozi kumi na moja kutoka nchi mbalimbali
duniani watakaohudhuria mkutano wa kimataifa wa Smart Partnership
utakaofunguliwa kesho na Rais Jakaya Kikwete kwenye Ukumbi wa Mikutano
wa Kimataifa wa Julius Nyerere, umesababisha kuimarishwa kwa ulinzi
katika maeneo mbalimbali hasa katika hoteli za kitalii ambazo zimeanza
utaratibu wa upekuzi kwa wageni wake.
Akizungumza na katika mahojiano na Redio ya Clouds jana, Membe alisema jiji limefurika kwa wingi wa wageni.
“Hoteli na nyumba za wageni zimefurika wageni na magari mengi
yamekodiwa. Kwa ujumla, huduma za kijamii zitakuwa shida,” alisema.
Rais Obama na mkewe Michelle watawasili nchini Jumatatu na tayari
wapambe na maofisa usalama kutokana Marekani wameanza kuwasili. Mbali ya
ujio huo, wake wa marais kutoka nchi 14 za Afrika watakaokutana na
Laura Bush, mke wa Rais wa zamani wa Marekani, George Bush. Pia Michelle
atahudhuria mkutano huo utakaofanyika Jumanne na Jumatano ijayo.
“Jiji la Dar es Salaam litakuwa na mambo mengi kwa hiyo wale wenye kuja
kutaka kustarehe wafute safari zao,” alisema na kuongeza: “Kama kuna
watu ambao hawapo Dar es Salaam na hawana sababu za kuja mjini waache tu
mpaka wageni watakapoondoka kwa sababu jiji la litakuwa limejaa na
baadhi ya barabara zitachukuliwa zitumike na wageni hao.”
Alisema katika kipindi cha siku tano zijazo, baadhi ya barabara za Jiji
la Dar es Salaam zitakuwa na shughuli nyingi na nyingine zitalazimika
kufungwa. Barabara itakayofungwa ni pamoja na ile ya Mwai Kibaki na ile
ya Bagamoyo itakuwa na shughuli nyingi pia wakati Michelle atakapokwenda
Jumba la Makumbusho, Jumanne ijayo.
Wasafiri wa mikoani
Wasafiri wa mikoani wataathirika zaidi Jumanne ijayo wakati Rais Obama
atakapokwenda kutembelea mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Symbion
Ubungo.
Kituo hicho kipo Barabara ya Morogoro, ambayo ndiyo inayotumiwa na magari yanayoingia na kutoka mikoani.
Rais Obama atakwenda katika kituo hicho yapata saa 4.00 asubuhi na kwa
kiasi kikubwa itaathiri magari ya usafirishaji wa mizigo na abiria
yatakayokuwa yanatoka na kuingia Dar es Salaam kabla na wakati huo.
Wengine watakaoathirika ni wakazi wa Kimara, Mbezi, Kibamba hadi
Kiluvya. Athari nyingine ya usafiri itakuwa katikati ya jiji ambako
Obama na msafara watakuwa na shughuli nyingi na hasa ile ya ufunguzi wa
barabara karibu na Ikulu na kukutana na wafanyabiashara kwenye Hoteli ya
Hyatt Regency, Jumatatu ijayo.
Watumiaji wengine wa barabara watakaopata shida ni wale wa Barabara ya
Bagamoyo hasa pale Rais Obama na mkewe watakapokwenda kuweka mashada ya
maua kwenye ubalozi wa zamani wa Marekani uliopuliwa na mabomu mwaka
1998.
Ulinzi hoteli za kitalii
Mashushushu wa ndani na nje ya nchi wamezingira kwenye hoteli kubwa za
Dar es Salaam na walionekana katika baadhi ya hoteli hizo, wakiwatumia
mbwa maalumu kufanya ukaguzi wa chumba hadi chumba.
Tofauti na utaratibu uliozoeleka, baadhi ya hoteli zenye hadhi ya nyota
tano zimeanza kutumia mitambo maalumu ya kompyuta kuwafanyia ukaguzi
wageni wote wanaoingia.
Wamchongea JK
Mtandao wa Kutetea Waandishi wa Habari Duniani (CPJ), umemwandikia barua
Rais Obama ukimtaka kujadiliana kwa kina na mwenyeji wake Rais Kikwete
wakati wa ziara yake nchini kuhusiana na vitendo vya kuuawa na kuteswa
kwa waandishi wa habari wa Tanzania.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu wa CPJ, Joel Simon na
nakala yake kusambazwa kwa viongozi mbalimbali akiwemo Rais Kikwete
mwenyewe, mtandao huo ulitolea mfano wa kuuawa kwa Mwandishi wa Channel
10, Daudi Mwangozi na Issa Ngumba wa Redio Kwizera. Pia kupigwa na
kuteswa kwa Mhariri Mtendaji wa Habari Corporation, Absalom Kibanda.
Marais waja Smart Partnership
Akizungumzia mkutano wa Smart Partnership utakaoanza kesho, Membe
alisema utajadili jinsi ya kutumia sayansi na teknolojia kukuza uchumi.
Viongozi watakaohudhuria mkutano huo ni Waziri Mkuu wa Malayasia, Najib
Razak, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Uhuru Kenyetta (Kenya), Boni
Yayi (Benin), Ali Omar Bongo (Gabon), Ikililou Dhoinine (Comoro), Faure
Gnassingbe (Togo), Ernest Koroma (Sierra Leone), Blaise Compaore
(Burkina Fasso), Mahinda Rajapaska (Sri Lanka) na Mfalme wa Swaziland,
Mswati II, ambaye aliwasili jana.
Chanzo: Mwananchi
Post a Comment