|
|
SUALA la nafasi ya meya wa jiji la Arusha limechukua sura mpya,
baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kudai kuwa sio
ajenda yao ya sasa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Kanda ya Kaskazini wa CHADEMA,
Amani Golugwa, alipozungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa
kwamba kwa sasa madiwani wa chama hicho wamejipanga kuweka mikakati
madhubuti ya kupanga na kusimamia miradi ya maendeleo iliyo kwenye
halmashauri hiyo kwa ushirikiano wa karibu na wananchi kwa manufaa ya
taifa.
Alisema pamoja na ukweli kuwa taratibu zilizotumika kumweka Meya
Gaudence Lyimo madakani hazikuwa sahihi, lakini kwa sasa kipaumbele chao
ni kushughulika na maendeleo ya wananchi.
Suala la nafasi ya meya wa jiji hili, lilisababisha maafa makubwa
wakati chama hicho kilipopinga kanuni zilizomweka madarakani.
Katika hatua nyingine, CHADEMA imemtaka Katibu wa Itikadi na Uenezi
wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, kuacha unafiki wa kupinga
kodi ya sh 1,000 kwa kila laini ya simu wakati wabunge wa chama chake
ndiyo walioipitisha.
Golugwa alisema kuwa kodi hiyo ilipitishwa kwa kishindo na wabunge wa
CCM ambao ni wengi wakati wale wa CHADEMA walipokuwa kwenye maombolezo
ya wananchi wanne waliouawa kwa bomu jijini Arusha, hivyo haiwezekani
leo CCM kuikataa.
“Tunamsihi Nape aache unafiki; awe mkweli, haiwezekani wabunge wa
chama chake wapitishe kodi hii inayowaumiza wananchi hasa wa kipato cha
chini halafu yeye akimbilie kwenye vyombo vya habari kuipinga. Kama CCM
ilikuwa haikubaliani na kodi hii isingepitishwa bungeni.
Nape anatakiwa aache usanii wa kujifanya hakujua tozo hii ya laini za
simu wakati ina baraka ya baraza la mawaziri ambalo linaongozwa na
Mwenyekiti wao wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete, na limepitishwa na wabunge
wa chama chake sasa anataka kuwahadaa wananchi kuwa CCM haihusiki,”
alihoji Golugwa.
Alisema kuwa tayari CHADEMA imeshaanza mchakato pamoja na wabunge wake
ili kuona namna suala hilo litakavyoshughulikiwa ikibidi hata kwa
kupeleka hoja binafsi bungeni ili kuhakikisha kodi hiyo inayowaumiza
wananchi walio wengi inaondolewa.
Kauli ya Golugwa imekuja siku chache baada ya Nnauye kutoa msimamo wa
CCM kuipinga kodi hiyo na kuishauri serikali kuiondoa na itafute njia
nyingine ya kuongeza mapato ambapo mamlaka ya mapato nchini (TRA)
imesema kwamba itakuwa inakusanya bilioni 28 kwa mwezi kwa kukata sh
1,000 katika kila laini ya simu. Inasemekana kuwa Watanzania wanaotumia
simu sasa nchi nzima ni zaidi ya mil. 28.
|
|
This post was written by: Author Name
Your description comes here!
Get Free Email Updates to your Inbox!
Filed Under:
Siasa
on Friday, July 19, 2013
Post a Comment