Johannesburg: “Happy birthday Mzee Madiba.” Rais wa kwanza na mzalendo
wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, leo anatimiza umri wa miaka 95, pia
anatimiza siku ya 40 tangu alipolazwa katika Hospitali ya Medclinic,
Pretoria kwa ajili ya matibabu.
Raia wa Afrika Kusini akiwa na bango la
kumtakia kheri ya siku ya kuzaliwa kwa Rais Mstaafu wa nchi hiyo, mjini
Polokwane nchini humo. Picha na Mtandao
Nelson Rolihlahla Mandela, alizaliwa Julai 18, 1918 katika Kijiji cha
Mvezo, eneo la Mthatha, Transkei Mkoa wa Eastern Cape na ametumia zaidi
ya asilimia 70 ya maisha yake akipigania haki na usawa wa wananchi wa
Afrika Kusini.
Maadhimisho ya miaka 95 tangu kuzaliwa kwa Mandela yanabeba uzito mkubwa
kuliko maadhimisho mengine yaliyotangulia kwani kwa siku 40, wananchi
wa Afrika Kusini wamekuwa katika wasiwasi mkubwa hasa kutokana na
kuzorota kwa afya ya kiongozi huyo.
Mandela alilazwa katika hospitali hiyo Juni 8, mwaka huu akiugua magonjwa ya figo na afya yake imeelezwa kuwa ni mbaya.
Leo, Rais Jacob Zuma atawaongoza mamilioni ya wananchi wa Afrika Kusini
katika maadhimisho ya nne ya kimataifa ya ‘Siku ya Mandela’ ambayo
yanakwenda sambamba na siku yake hiyo ya kuzaliwa.
Tangu kulazwa kwa Mandela huko Pretoria, Rais Zuma amekuwa akiwahimiza
wananchi wake wajiandae kusherehekea miaka 95 ya Mandela akiwatia moyo
wale waliokuwa na wasiwasi kwamba Madiba asingeweza kuifikia leo
kutokana na matatizo ya kiafya.
Siku ya Mandela huadhimishwa kuenzi kazi za kiongozi huyo alizozifanya
kwa miaka 67 akiutumikia umma wa wananchi wa Afrika Kusini, zikiwamo
vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye kuwa Rais wa kwanza mzalendo
kwa miaka mitano, kisha kustaafu.
Pia ‘Mandela Day’ hutumika kukumbuka kampeni yake dhidi ya ubaguzi wa
rangi na utetezi wa haki za binadamu maarufu kwa jina la “46664”, ambayo
ni namba ya utambulisho aliyoitumia alipokuwa mfungwa katika Gereza la
Visiwa vya Robben.
Dakika 67 za Mandela
Kwa maana ya Siku ya Mandela ambayo pia imeidhinishwa na kutambuliwa na
Umoja wa Mataifa, wananchi wa Afrika Kusini wanatumia dakika 67 kufanya
shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni hatua ya kuenzi kile
wanachokiita ‘kazi za mtu aliyejitoa maisha yake kwa ajili ya kupigania
haki na utu’.
Dakika hizo 67 zinawakilisha idadi kama hiyo ya miaka ambayo Mandela
alitumika, hivyo Waafrika Kusini watakuwa wakitoa msaada na huduma kwa
jamii iwe ni kwa watoto yatima au watu wengine ambao ni wahitaji katika
jamii.
Kituo cha Kumbukumbu ya Mandela kimewataka wananchi kuungana na
kuonyesha ushirikiano wao kwa Mandela kwa kutumia dakika 67 za muda wao
kuzisaidia jamii zao ili kumuenzi kiongozi huyo ambaye ni alama ya
dunia.
Post a Comment