Uongozi wa Yanga umesema utapinga uamuzi wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi ya Wachezaji ya TFF ya kumfungia Ngassa.
Dar. Mshambuliaji mpya wa Yanga,
Mrisho Ngassa ameishangaa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi ya
Wachezaji kwa kushindwa kumtendea haki ya kumruhusu kuichezea Yanga moja
kwa moja badala yake wamemfungia mechi sita na kumtaka kuilipa Simba Sh
45 milioni.
Ngassa alisema jana kuwa uamuzi wa kamati hiyo ya
TFF umetokana na ‘fitina’ za soka, lakini yeye anaamini ni mchezaji
halali wa Yanga.
Alisema kuwa hakusaini mkataba na Simba kutokana
na ukweli kuwa alikuwa na timu hiyo kwa mkopo na kama angekuwa amesaini,
kamati hiyo ingemwidhinisha kuchezea Simba ambayo aliitumikia katika
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita.
“Wameniidhinisha kuichezea Yanga, eti mpaka nikae
nje mechi sita na kulipa fidia, hii siyo haki na kwa nini wanipe adhabu
wakati wao walitakiwa kunitetea mimi kwa mujibu wa kazi zao,” alisema
Ngassa.
Alisema kuwa, “Tofauti na majukumu yao,
wameniangamiza kwa staili ya ‘kuuma na kupulizia’ kwa kuogopa kufuata
sheria ambayo wameitumia kuniidhinisha kuichezea Yanga.”
“Mimi napingana nao, si uamuzi wa kunitetea,
‘nitakomaa’ nao na ninaamini viongozi wangu wa Yanga nao watakuwa na
msimamo huohuo,” alisema Ngassa.
Nao uongozi wa Yanga umesema kuwa utapinga uamuzi
wa Kamati hiyo ya TFF wa kumfungia Ngassa kuichezea timu yao kwa mechi
sita sambamba na kuilipa fidia Simba ya Sh45 milioni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah
Bin Kleb alisema kuwa uamuzi wa Kamati hiyo haukulenga hali halisi ya
sakata zima la usajili wa mchezaji huyo na kuhoji kwa nini amelipishwa
faini huku akiidhinishwa kuichezea Yanga?
Bin Kleb alisema kuwa kama kamati imeridhika kuwa
Yanga imefuata taratibu zote za usajili wa mchezaji huyo, haikupaswa
kumchukulia hatua zote hizo.
Alisema kuwa cha ajabu ni kitendo cha kamati hiyo
kushindwa kuiadhibu Simba ambayo inadaiwa ilimsainisha mkataba mwingine
Ngassa huku wakijua kuwa anaitumikia klabu hiyo kwa mkopo na ni kinyume
na utaratibu, siyo hapa Tanzania tu, bali dunia nzima.
“Kingine kamati haikuzingatia mambo aliyofanya
Ngassa akiwa Simba, ameifungia mabao timu hiyo na kuiwezesha kushika
nafasi ya tatu, hii leo unaamuru arejeshe fedha zote zinazodaiwa kulipwa
kwa mchezaji huyo bila kujali ameifanyia nini timu hiyo,” alisema Bin
Kleb.
CHANZO:Mwananchi.
CHANZO:Mwananchi.
