JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Shirika
la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), limeiomba
radhi Serikali ya Tanzania kufuatia taarifa waliyoitoa kwenye Mkutano wa
64 wa Kamati Tendaji (EXCOM) ya shirika hilo uliofanyika Geneva, Uswisi
tarehe 30 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba, 2013. Katika taarifa yao
kuhusu Afrika, UNHCR ilieleza kuwa Tanzania imewafukuza Wakimbizi wa
Rwanda na Burundi katika operesheni ya kuwaondoa Wahamiaji haramu
inayoendelea nchini.
UNHRC imeiomba radhi Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia barua yake ya tarehe 2
Oktoba, 2013. Barua hiyo imeandikwa na Mkurugenzi wa UNHCR Kanda ya
Afrika Bw. George Okoth-Obbo kwenda kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Mhe. Pereira Ame Silima aliyeongoza ujumbe wa Tanzania katika
Mkutano huo unaofanyika kila mwaka.
Katika
barua hiyo, UNHCR imeeleza kusikitishwa na taarifa hiyo ambayo si ya
kweli na imekiri kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imekuwa ikishirikiana kwa karibu na UNHRC katika ngazi zote kuhakikisha
kwamba hakuna mkimbizi anayerejeshwa kwao katika zoezi la kuwakamata na
kuwarejesha kwao wahamiaji haramu linaloendelea nchini Tanzania.
Aidha, Bw. Okoth Obbo ameeleza kuwa
UNHCR na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla inatambua na kuthamini kwa
dhati mchango mkubwa ambao Tanzania imeutoa na inaendelea kuutoa katika
kuwahifadhi wakimbizi wa mataifa mbalimbali kwa kipindi cha takribani
miaka 40.
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea kauli hiyo na kueleza
kwamba inatarajia na inaamini kwamba UNHCR itaendelea kutoa taarifa
sahihi zenye kutoa picha halisi inayoonesha namna Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inavyotekeleza wajibu wake kuwalinda na
kuwahifadhi Wakimbizi kwa mujibu wa Sheria za nchi na mikataba ya
Kimataifa ambayo nchi imeridhia.
Mwisho.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
06, Oktoba, 2013