Yanga
licha ya kutia ugumu katika kutotaka mechi zao kurushwa 'live' na Azam
TV, kituo hicho kipya cha televisheni nchini kitaendelea kurusha mechi
zote za ugenini za mabingwa hao wa soka wa Tanzania Bara.(hd)
Ofisa
Habari wa shirikisho la soka (TFF), Boniface Wambura aliiambia NIPASHE
jana Azam TV itaendelea kuonyesha mechi za Yanga za ugenini kwa sababu
haziko katika mamlaka yao.
Yanga
walikataa mechi zao kurushwa na Azam TV walionunua haki za matangazo ya
televisheni kwa Sh. bilioni 5.6 wakitaka wapewe fungu kubwa kuzidi klabu
nyingine kwa madai wana mashabiki wengi zaidi nchini.
Hata
hivyo, baada ya kuonekana kwamba Yanga hawana mamlaka na mechi za
ugenini, miamba hao wa soka nchini wako tayari mechi hizo zionyeshwe
lakini wakibaki na msimamo kwamba za nyumbani hazitaonyeshwa.
Wikiendi
iliyopita, hata hivyo, mechi ya Yanga ya nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar
ambayo Wanajangwani walishinda 2-0 Jumapili, ilirushwa moja kwa moja na
Azam TV kupitia kituo cha televisheni cha TBC.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema walishangazwa na kitendo hicho.
"Sisi
(Yanga) tulishangaa baada ya kubaini kuwa mechi yetu dhidi ya Mtibwa
ilikuwa inarushwa 'live' na Azam TV kinyume cha makubaliano yetu na TFF.
Waulizeni TFF kwanini mechi hiyo ilirushwa wakati Yanga haikuwa 'away'
(ugenini).
Hata
hivyo, mkataba uliosainiwa baina ya Azam Media na TFF ulijumuisha
kurusha mechi za timu zote bila ya kujali kama ni Yanga ama timu gani.
Wakati
huo huo, timu ya soka ya Azam FC leo itakuwa na fursa ya kuishusha Yanga
katika nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wakati
itakapoikaribisha Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo
Chamazi, Dar es Salaam.
Ushindi
dhidi ya timu hiyo ya Tanga ambayo imepoteza mechi mbili mfululizo za
nyumbani zilizopita, utaifanya Azam ifikishe pointi 14, mbili zaidi ya
Yanga ambayo itakuwa na mechi moja mkononi.
Mgambo
Shooting yenye pointi tano, ikiwa nafasi ya pili kutoka mwisho imeshinda
mechi moja tu dhidi ya Ashanti United huku ikipoteza mbili nyumbani
dhidi ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons. Kocha Mohamed Kampira ana kibarua
cha kuhakikisha anapata pointi mbele ya Azam.
Mechi
nyingine za ligi hiyo leo ni Rhino Rangers itakayoivaa timu iliyo kwenye
kiwango ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora
wakati JKT Ruvu watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa
Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utazikutanisha
Oljoro JKT na Ruvu Shooting ya Pwani inayofundishwa na Charles Boniface
Mkwasa.
CHANZO: NIPASHE