Ninachokiongelea hapo juu kina ukweli zaidi katika maisha ya Salma Msangi ambaye
leo kwa wengi ni mtangazaji wa luninga na radio mwenye tabasamu zito,
wepesi wa kuelewa mazingira na mwenye kuipenda kazi yake na kuwapenda
mashabiki,watazamaji wa vipindi vyake vya kwenye luninga na wasikilizaji
wa vipindi vyake radioni.
Mara ya kwanza nilimuona Salma akiwa binti mdogo tu aliposhiriki
shindano la kumtafuta mrembo wa Wilaya ya Ilala[ Miss Ilala]. Ilikuwa
mwaka 2003. Ukumbi ulikuwa ni Diamond Jubilee. Endapo kungekuwa na
mizani ya kupima nani angefika mbali sio tu katika shindano lile bali
maishani kwa ujumla, bila shaka Salma angekuwemo. Kilichomtofautisha
yeye na wengine si urembo. Ni kujiamini. Bado ninakumbuka jinsi
alivyojibu swali. Jibu lake halikuwa jibu sahihi kupita yote. Lakini
jinsi alivyolijibu, ilitosha kumuweka katika ukurasa mwingine.
Ndivyo safari yake ilivyoanza. Safari ile ikaanzisha safari nyingine na nyingine mpaka kufikia hapa alipo. Leo hii Salma Msangi
ni mtangazaji anayefahamika na mwenye wafuasi wake lukuki ilhali
akiendelea kujifunza mambo mengi zaidi na hivyo kuongeza maarifa kila
kukicha.
Hivi karibuni nilipata bahati ya kufanya naye mahojiano ambayo
utayasoma hivi punde. Endapo uliwahi kutamani kujua amefikaje hapo
alipo,fursa ndio hii. Endapo unataka kujua Salma ana mtizamo gani kuhusu
masuala mbalimbali ya kijamii kama vile wanawake, mitandao ya kijamii,
wasanii nk, fursa ndio hii. Kikubwa zaidi, Salma ana ushauri ambao
naamini kila mtu anapaswa kuusoma hususani vijana.Uuze “sembe” au
ufanyeje? Ungana nami….
BC: Salma, karibu sana ndani ya BC na shukrani nyingi kwa kukubali kufanya nami mahojiano haya. Mambo yanakwendaje?
Salma: Mambo sio mabaya tunashukuru tunasonga. Ahsante sana
Jeff, Kaka hahaa.. kwetu kumoja weweee au sio? Nashukuru kwa kunipa
nafasi hii ya kutaka kufahamu kidogo kuhusu mimi. Mara nyingi huwa
sipendi interview na nimekuwa nazikwepa kweli. Huwa naogopa maswali
lakini nitajaribu.
BC: Naam, kweli kabisa mimi na wewe njia moja.Salma Msangi ni nani? Alianzia wapi mpaka kufikia hapa alipo?
Salma: Salma Msangi ni
msichana aliyezaliwa miaka 29 iliyopita katika wilaya ya Same Mjini mkoa
wa Kilimanjaro. Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Msingi
Masandare hapo hapo Same kabla ya kuhamia jijini Dar Es Salaam kuungana
na mama yake mzazi kwa ajili ya kuendelea na masomo ya sekondari.
Kabla ya hapo Salma alilelewa na Mama yake mkubwa ambaye alikua
ameolewa na Mjerumani. Hii ni baada ya mama yake mkubwa kuamua kumchukua
kwasababu wakati anazaliwa mama yake alikua na umri mdogo kama wa miaka
18 hivi kwa hiyo ndugu na jamaa wakashauriana na kukubaliana kwamba
kutokana na umri huo mdogo asingeweza kumpa mtoto matunzo mazuri au
yanayostahili. Alikuwa bado mdogo na kwa ujumla angehitaji kuendelea
zaidi na jitihada zake katika maisha.
Hivyo nilihamia Dar Es Salaam sehemu ambapo mama yangu alihamia
katika harakati za kutafuta maisha. Nikajiunga na shule ya sekondari
Alharamain Islamic na kumaliza elimu yangu ya sekondari pale mwaka 2001.
Baada ya hapo kilichofuata ni kozi mbali mbali nilizojiunga nazo
ikiwemo masomo ya IT katika chuo cha Issam Computer Networking.
Post a Comment