Rais wa Rwanda Paul Kagame 
ameshutumu vikali viongozi wa Burundi kutokana na mauaji yanayoendelea 
nchini humo nakuonya kuwa huenda kukatokea mauaji ya halaiki
Bw Kagame ameshangaa ni vipi viongozi wa taifa hilo jirani "wanaweza kuruhusu wananchi wao kuuwawa kiholela".
Rais
 Kagame alisema hayo Ijumaa, lakini matamshi yake hayakutangazwa hadi 
mwishoni mwa wiki, akionekana sana kumlenga Rais wa Burundi Pierre 
Nkurunziza.
Akizungumza kwa Kinyarwanda Rais Kagame alisema: 
''Tazama nchi jirani kama Burundi, maisha yao yamesimama kabisa. Lakini 
sababu ni ipi? Wana historia inayofanana na yetu.
Ila viongozi wao wapo kwa ajili ya kuua wananchi kuanzia asubuhi hadi jioni."
''Rais akajifungia sehemu isiyojulikana, hakuna 
anayejua sehemu alikojificha, hakuna anayezungumza naye, huyo anaongoza 
watu vipi?" alisema Bw Kagame, akihutubu katika hafla ya kuwatunuku 
Wanyarwanda waliosaidia kuwaficha na kuwaokoa Watutsi wakati wa mauaji 
ya kimbari 1994 pamoja na wanaharakati wanaotetea umoja na maridhiano 
miongoni mwa Wanyarwanda.
''Watu wanakufa kila siku, maiti 
zinabururwa barabarani. La kusikitisha ni kuwa bara la Afrika lina 
ugonjwa wake lenyewe kiasi kwamba hata nitalaumiwa eti nimekosea kuitaja
 nchi nyingine, eti ningecheza diplomasia au siasa. Siyo haki mimi 
nitasema wazi. Viongozi wanashinda wakiua watu, maiti zinatapakaa sehemu
 zote; wakimbizi wanarandaranda sehemu zote watoto, wanawake ....kisha 
unasema ni siasa. Hiyo ni siasa gani?"
Uhusiano kati ya Rwanda na 
Burundi umedorora sana tangu Bw Nkurunziza atangaze kuwa atawania urais 
kwa muhula wa tatu, hatua iliyopingwa na wapinzani.
Mwezi uliopita, 
Burundi ilimfurusha mwanabalozi mmoja kutoka Rwanda ikimtuhumu kwa kuhujumu usalama wa nchi hiyo.
"Utasema
 kuwa ni nani aliyesababisha matatizo ya Burundi? hata kukiwa na mtu 
anayekutakia mabaya atavutiwa na ubaya wako unaotenda...Hata kama ni mtu
 kutoka Rwanda anayesababisha machafuko nchini Burundi, bila shaka 
atavutiwa na maovu ya viongozi wa Burundi wanayotendea wananchi wao. 
Shida ni ya Warundi wenyewe," alisema Bw Kagame.
"Tatizo ni kwamba hawakupata somo kutoka kwetu 
(Rwanda), kutokana na yaliyosibu taifa letu wangepata somo hasa kutokana
 na baadhi ya Warundi wenyewe kuhusika katika yale yaliyolisibu taifa 
letu.
Afrika sijui tunaugua ugonjwa upi?"
Hayo yamejiri siku moja baaya watu 9 kuawa usiku na watu wenye silaha, ndani ya baa moja katika mji mkuu wa Bujumbura.
Askari
 wa usalama wanafanya msako katika kila nyumba, kwenye mitaa 
inayoonekana kuwa ni ngome za upinzani, baada ya muda uliowekwa na 
serikali kwa watu kusalimisha silaha zao kumalizika.
Watu takriban 20 wameuwawa nchini Burundi katika juma lilopita, huku maelfu ya watu wakitoroka makwao.
SOURCE:BBC SWAHILI 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
Post a Comment