Mfanyabiashara maarufu ambaye pia ni
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akitembea
kwenye 'Red Carpet' mara baada ya kuwasili katika hotel ya Hilton
Sandton jijini Johannesburg, Afrika Kusini kwenye hafla ya utoaji tuzo
iliyoandaliwa na jarida maarufu la Forbes na kutunukiwa tuzo ya "Forbes
Africa Person Of the Year 2015".(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).
Na Modewjiblog team
MFANYABIASHARA na mtu mwenye taasisi ya
kusaidia jamii, Mohammed Dewji maarufu kama Mo ametunukiwa tuzo ya
jarida maarufu la Forbes ya "Forbes Africa Person Of the Year 2015"
katika hafla iliyofanyika Novemba 27 mwaka huu jijini Johannesburg,
Afrika Kusini.
Mfanyabiashara huyo pia ni Afisa Mtendaji
Mkuu wa Makampuni ya Mohammed Enterprises T Ltd (MeTL Group) kampuni
iliyoanzishwa na na baba yake katika miaka ya 1970 ambayo sasa imekua na
kujikita katika viwanda vya nguo, usagaji nafaka, utengenezaji wa
vinywaji baridi, usindikaji wa mafuta ya kula, usindikaji wa chai na
kuendesha mashamba ya mkonge ambapo tayari anashea ya asilimia 40 ya
soko.
Mo ametwaa tuzo hiyo kwa kuwashinda watu
watano mashuhuri barani Afrika. Watu hao ni Nkosazana Dlamini Zuma, mke
wa Kwanza wa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. Mama huyo kwa sasa ndiye
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU). Mwingine ni Rais wa sasa wa
Nigeria, Muhammadu Buhari aliyetambuliwa kutokana na kuanzisha vita
dhidi ya rushwa nchini mwake.
Aidha wapo Arumna Otei, mchumi mahiri
raia wa Nigeria ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia. Pia
alikuwemo Mwandishi maarufu wa vitabu wa Nigeria, Chimanda Ngozi
Adichie ambaye moja ya vitabu vyake vinaelezea picha halisi ya Afrika
inavyofikiriwa duniani.
Akitoa neno la shukurani baada ya
kukabidhiwa kwa tuzo hiyo Mo, alisema anatoa tuzo hiyo kwa vijana wa
Kitanzania kwani ndio nguvu kazi inayobeba uchumi wa nchi.
Mo ambaye kampuni yake ya MeTL inaongoza
kwa kutoa ajira nchini, ikiwa imetoa ajira 26,000 kote katika viwanda
vyake 31 vilivyopo nchini na katika mataifa matano ya Afrika, alisema
amefurahishwa na tuzo hiyo ambayo anaitoa kwa vijana kwa kutambua pia
wajibu mkubwa walionao katika kukabiliana na umaskini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya
MeTL Group, Mohammed Dewji akifurahi jambo na baadhi ya wageni waalikwa
nje ya ukumbi wa hafla hiyo ya utoaji tuzo iliyoandaliwa na jarida la
Forbes.
Alisema ajira 26,000 zimegusa watu wengi
nchini na kwamba ana matumaini makubwa ya siku za usoni kutoa ajira
zaidi kutokana na biashara zake kuendelea kukua.
"Heshima yangu kubwa haitokani na
utajiri, maana kama utajiri wako hauna msaada wala kugusa watu masikini
hauna maana yeyote, hivyo basi heshima hii ni kutokana na kwanza bidhaa
zangu kugusa maisha ya watu kila siku kuanzia sukari na majani ya chai
asubuhi pamoja na unga wa ngano, lakini pia chakula cha mchana kwa unga
wa sembe, mafuta ya kupikia na maji ya kunywa, bidhaa zote hizo za
Mohammed Enterprises zinagusa maisha kila nyakati katika siku.
"Nina viwanda 31 ambavyo vimekuwa
vikitengeneza bidhaa za Kitanzania na kuziuza kwa Watanzania kwa bei
yenye unafuu mkubwa, mathalani tunauza maji kwa bei chini ya dola moja
kwa shilingi za Kitanzania 200, hakuna hata Ulaya, nina kiwanda cha
khanga na vitenge ambacho malighafi zake zote ni za Kitanzania, hivyo
kuna kusaidia serikali kwa kulipa kodi ipasavyo, lakini pia kusaidia
moja kwa moja ajira za Watanzania walio wengi ambao tatizo lao kubwa
katika kundi la vijana ni ajira"
Alitumia fursa hiyo kumshukuru na
kumpongeza baba yake kwa kumwita mjasiriamali shujaa ambaye alitoka
kuanzia dereva wa malori baada ya kuhitimu kidato cha nne mwishoni mwa
miaka ya 1960 hadi kufikia ubilionea. Alisema alipata maono ya utajiri
hasa kutoka kwa baba yake huyo aliyekuwa akimshirikisha biashara tangu
akiwa mdogo.
“Mwanaume mwenye ndoto huhitaji mwanamke
mwenye maono. Na nimebarikiwa mwanamke ambaye kwa miaka 15 amekuwa
akinipa sapoti isiyoyumba.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya
MeTL Group, Mohammed Dewji akibadilishana 'Business card' na mmoja wa
wageni waalikwa katika hafla hiyo.
“Saira, nina shukurani nyingi kwako kwa
kuwa nguzo ya familia yetu, mama wa heshima kwa watoto wetu watatu,”
alisema Mo kwenye hafla hiyo.
Kwa utulivu, Mo alisema: “Baba, zawadi
kubwa ambayo ulinipa katika maisha yangu ni muda wako, na kwa hilo
nitakuwa mwenye deni la shukurani kwako siku zote za maisha yangu.”
Mo ambaye moyo wake wa binadamu ulimfanya
awanie uwakilishi Jimbo la Singida Mjini kwa tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na kushinda nafasi hiyo na hivyo kuwawakilisha
wanasingida kuanzia 2005 na 2015 amesema maisha ni changamoto kubwa
inayobadilishwa kwa utumishi wenye nia ya dhati kwa umma.
Alisema alipowania uwakilishi alikuwa na
sababu: “Nilikuwa na umri wa miaka 24, nilikwenda Singida kutoa heshima
kwenye kaburi la marehemu babu yangu. Sikuwa nimefika huko tangu
nilipoondoka nikiwa na umri wa miaka mitatu.
“Nilipokuwa njiani, nilimuona mzee akiwa
na maji yenye rangi ya njano, machafu ambayo aliyatumia kwa kunywa.
Nilishangaa, maana hali ile sikuwahi kufikiri kama ipo vile. Kipindi
hicho nilikuwa nimemaliza Chuo Kikuu cha Georgetown, Marekani.”
Mo anasema kuwa aliingiwa na hisia kutaka
kujua nini hasa alichokuwa anahitajika kufanya, alimfuata yule mzee
aliyekuwa na maji yale, alipozungumza naye, aliwazungukia watu wengine
na kuridhika kuwa ile ndiyo hali halisi, hapo ndipo fikra ya kwa nini
agombee ubunge ilipoanzia.
Anasema kuwa baada ya kujiridhisha hivyo,
alirudi kwa mzee wa kwanza, alizungumza naye na kumuuliza ni kwa nini
shida ile ilikuwa haizungumzwi kwa upana katika mamlaka husika.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji pamoja na ujumbe wake alioambatana nao kutoka Tanzania.
“Nilipojitambulisha yule mzee alisema
anamkumbuka babu yangu, kisha akanishauri nigombee ubunge, alinisisitiza
mno ili nisaidie kuondoa lile tatizo la watu wa Singida kunywa maji
machafu,” alisema Mo.
Anaeleza kuwa alipokuwa njiani kurejea
Dar es Salaam, alilifikiria tatizo hilo kwa mapana zaidi, akalifanyia
utafiti na kubaini kwamba katika kila watu 10, watatu walikuwa
wakipoteza maisha kutokana na maradhi yanayosababishwa na maji machafu.
Anaendelea kusema kuwa aligundua kuwa
Singida kulikuwa na tatizo kali la maji safi na salama. Anasema kuwa
alibaini uwepo wa tatizo la elimu kuhusu matatizo ya maji.
Jambo lingine ambalo anasema aliligundua
ni uwepo wa tatizo la huduma za afya. “Niliwafikiria watoto wangu, jinsi
ninavyowapenda, na namna ambavyo kila mzazi anavyompenda mwanaye.
Nilipingana na hali kuwa watoto wa Uingereza na Marekani wamependelewa
zaidi. Maisha ni sawa bila kujali chochote,” anasema Mo.
Sehemu ya ujumbe kutoka Tanzania
uliombatana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed
Dewji kwenye hafla hiyo.
“Niliona lazima nitimize wajibu wangu.
Kutimiza malengo yangu ya kusaidia jamii, kufanikiwa katika biashara.
Mambo hayo mawili hisani na biashara nimeyaweka pamoja na ndiyo maana
nimefika hapa leo, tunajivunia sana kuitwa METL nembo ya Watu. Katika
miaka yangu 10 kama mbunge, nimefanya mabadiliko mengi. Nilikuwa na
sababu ya kupata mkopo nafuu wa dola milioni 35, ambao ulisababisha
kuwekwa kwa miundombinu ya maji safi na salama Manispaa ya Singida.
“Niliitumia MeTL, tuliweza kudhamini
shughuli nyingi za maendeleo ya kijamii. Kuhusu elimu, nilifanikisha
kujenga shule 15, zikawa 17, kabla ya hapo tulikuwa na shule mbili tu.
“Kuhusu huduma za afya, hapa nimshukuru mke wangu kwa jitihada zake.
Alikuwa Mwenyekiti wa taasisi ya Tumaini la Maisha ambayo imekuwa
ikisaidia watu wengi, hasa watoto dhidi ya maradhi ya saratani.”
Burudani mbalimbali zikiendelea ukumbini hapo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jarida la Forbes
Afrika, Sid Wahi akitoa neno la ukaribisho kwa wageni waalikwa. Kulia
ni Head of Events wa ABN Productions, Alexander Leibner.
Mwanzilishi na mchapishaji wa jarida la
Forbes Afrika, Bw. Rakesh Wahi ( wa pili kushoto) akikamkabidhi
Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania na Afisa Mtendaji Mkuu wa
Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji (wa pili kulia) tuzo ya Heshima
Barani Afrika "2015 Forbes Africa Person of the Year" iliyotolewa na
Jarida la Forbes Afrika kwa kutambua mchango wake katika kusaidia jamii
ikiwemo kutoa ajira kwa zaidi ya watu 26,000 nchini na mambo mengine
yanayoigusa jamii. Wanaoshuhudia tukio hilo ni Mkurugenzi Mtendaji wa
Forbes Afrika, Sid Wahi (kulia) na MEC Panyaza Lesufi kutoka kitengo cha
elimu, Gauteng Province (kushoto).
Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania
na Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akitoa
neno la shukurani baada ya kukabidhiwa kwa tuzo, alisema anatoa tuzo
hiyo kwa vijana wa Kitanzania kwani ndio nguvu kazi inayobeba uchumi wa
nchi.
MO akiteta jambo na Mchumi mahiri raia
wa Nigeria ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Arunma
Oteh (kulia) ambaye walikuwa pamoja kwenye kinyang'anyiro cha kuwania
tuzo hiyo ambapo pia alimpongeza sana.
Pichani juu na chini MO akiendelea kupongezwa na wadau mbalimbali walioalikwa kwenye hafla hiyo.
Pongezi kwa MO zikiendelea kutolewa.
MO katika picha ya pamoja na baadhi ya
wafanyakazi wa kampuni ya Jaguar Land Rover ambao ni miongoni mwa
wadhamini wa sherehe za tuzo hizo.
MO katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Makampuni ya MeTL Group, Vipul Kakad mara baada ya kutwaa tuzo hiyo.
Makamu wa Rais wa MeTL GROUP, Vipul Kakad na Shemane Amin wakipitia moja ya taarifa iliyowavutia kwenye jarida la Forbes Afrika.
Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Jaguar Land Rover ya Afrika Kusini wakipozi kwenye 'Red Carpet'.
Post a Comment