Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani akionesha Kifaa cha
‘Lead Board’ kwa viongozi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma (hawapo
pichani) hivi karibuni. Dk Kalemani alikutana na viongozi hao wakati wa
ziara yake wilayani humo kukagua miradi ya umeme inayotekelezwa na
Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma
Kaskazini, Peter Serukamba.
Fundi
Umeme, akifunga umeme wa REA kama alivyokutwa na Msafara wa Naibu Waziri
wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, eneo la Buselesele mkoani
Geita hivi karibuni. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua
miradi ya umeme vijijini.
Na Veronica Simba - Kakonko
Serikali
imesema, wananchi wa kipato cha chini, hususan wa vijijini, wenye
nyumba zenye kuanzia Chumba kimoja hadi Vinne, wataunganishiwa umeme
pasipo kutandaza nyaya za umeme (wiring) kwenye nyumba zao.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, aliyasema hayo hivi
karibuni Wilayani Kakonko, mkoani Kigoma, akiwa katika ziara ya kazi
mkoani humo, kukagua miradi inayotekelezwa chini ya wizara yake, hususan
ya umeme vijijini, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Dk
Kalemani alisema, badala ya kutandaza nyaya za umeme katika nyumba zao,
wananchi hao watafungiwa kifaa maalum kijulikanacho kitaalam kama ‘Lead
Board’, kitakachowawezesha kutumia umeme kama kawaida.
Alisema,
utumiaji wa kifaa hicho ni teknolojia mpya itakayowasaidia wananchi wa
kipato cha chini kuondokana na gharama kubwa za kutandaza nyaya ndani ya
nyumba, ambazo mara nyingi husababisha wengi wao kushindwa kumudu
gharama hizo na hivyo kukosa huduma muhimu ya umeme.
Hata
hivyo, Dk Kalemani aliweka bayana kuwa, watakaonufaika na huduma hiyo ni
wale tu wenye kipato cha chini, wanaomiliki nyumba ndogo za kuanzia
chumba kimoja hadi vinne. “Wenye nyumba kubwa wataendelea na utaratibu
wa kawaida wa kutandaza nyaya.”
Alisema,
Serikali imefikia uamuzi huo, baada ya kuona wananchi wengi wa
vijijini, ambao kipato chao ni duni, wanashindwa kunufaika na huduma ya
umeme, licha ya Serikali kuwapelekea huduma hiyo kwa gharama nafuu sana
kupitia Mradi wa Umeme Vijijini unaotekelezwa na REA.
"Kama
Serikali, tumedhamiria kuhakikisha asilimia 75 ya Watanzania wanatumia
nishati ya umeme ifikapo mwaka 2025. Ili kufikia malengo hayo, ni lazima
tuhakikishe tunawapatia huduma hiyo muhimu Watanzania wengi zaidi, na
tuhakikishe wanawezeshwa kuitumia, hususani walioko vijijini, ambao
wengi wao wana kipato cha chini,” alisisitiza Naibu Waziri.
Akifafanua
zaidi kuhusu faida za kutumia kifaa hicho, Naibu Waziri alisema,
wananchi watakaofungiwa ‘Lead Board’, watatumia shilingi 27,000 hadi
30,000 tu. Gharama hiyo inahusisha uwekaji wa nguzo, kuunganishiwa umeme
nyumbani pamoja na kifaa husika.
Alibainisha
kuwa, kimsingi, umeme wa REA ni bure, isipokuwa mwananchi analazimika
kulipia shilingi 27,000 tu kama tozo ya kodi ya Serikali (VAT). “Tofauti
na kulipia VAT, hakuna malipo hata Thumni kwani Serikali imegharamia
umeme huo.”
Aliongeza
kuwa, Serikali inaangalia utaratibu wa kuondoa hata shilingi 6,000
inayotumika kulipia fomu kwa ajili ya maombi ya umeme kama njia ya
kumwezesha mwananchi wa kipato cha chini kutumia huduma hiyo.
Akizungumzia
gharama za matumizi ya umeme, Dk Kalemani alisema, watumiaji wote wa
umeme, ambao matumizi yao ni chini ya uniti 75, wanapaswa kulipia
shilingi 100 tu za kitanzania kwa kila uniti moja. Alisema, gharama hiyo
ni nafuu sana, hivyo hakuna sababu ya wananchi wa kipato cha chini
kushindwa kutumia umeme kwani wako katika kundi hilo linalotumia umeme
kidogo.
Dk
Kalemani alifafanua kuwa, wapo baadhi ya wananchi wanaotumia umeme chini
ya uniti 75, lakini kwa bahati mbaya, wamewekwa katika kundi la
watumiaji wakubwa wa umeme, hivyo wanapaswa kupeleka malalamiko katika
Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika maeneo yao ili
wabadilishwe na kurudishwa katika kundi wanalostahili kuwa.
Vilevile,
aliwataka viongozi katika ngazi mbalimbali, kuanzia Kijiji hadi Mkoa,
kuelimisha wananchi juu ya matumizi bora ya umeme, kwani wengi wanatumia
umeme vibaya na hivyo kulazimika kulipia bili kubwa.
Akizungumzia
suala la kukatika-katika kwa umeme, Dk Kalemani alisema, Wizara yake
imewaagiza Mameneja wa Tanesco wa Wilaya, Mkoa na Kanda nchi nzima,
kuhakikisha wanarekebisha miundombinu mibovu ya umeme kama vile nguzo na
transfoma ili kutatua tatizo hilo.
“Kwa
hiyo, kukatika-katika kwa umeme kunakotokana na masuala ya kibinadamu,
hakutarajiwi kuendelea baada ya Machi 31, mwaka huu.”
Aidha,
aliwataka viongozi katika ngazi za Vijiji, Tarafa, Wilaya na hata Mkoa,
kuhakikisha wanawasilisha majina ya vijiji ambavyo havikupangwa
kupelekewa huduma ya umeme katika Mradi wa REA Awamu ya II, unaotarajia
kukamilika ifikapo mwezi Juni mwaka huu, ili viingizwe katika Mradi wa
REA Awamu ya III, unaotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.
Alisisitiza
kutokusahau maeneo muhimu kama Vituo vya Afya, Shule, Masoko, Magereza,
Jeshi na mengine ya aina hiyo, ambavyo havikupangwa kwenye REA Awamu ya
II, ili viingie katika REA Awamu ya III.
Post a Comment