Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,
amemteua Balozi Mhandisi John William Kijazi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi
tarehe 6 Machi 2016, akichukua nafasi ya Balozi Ombeni Sefue.
Kabla ya uteuzi huo, Balozi Mhandisi Kijazi alikuwa mwakilishi wa
Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal mwenye
makazi yake jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007 na hivyo kumfanya
kuwa Mkuu wa Mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi.
Vilevile, hadi uteuzi wake, Balozi Kijazi amekuwa Mkuu wa Mabalozi
wa Afrika nchini India ambaye amekuwa mtetezi mkuu wa wanafunzi wenye
asili ya Kiafrika nchini India.
Kabla ya kuwa balozi, Mhandisi Kijazi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya
Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002
hadi 2006, baada ya kuteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New
Delhi, India. Kati ya mwaka 1996 hadi 2002.
Mhandisi Kijazi alikuwa Mhandisi Mwandamizi wa Ujenzi wa Barabara
ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi
wa Barabara za Mikoa ndani ya Wizara hiyo hiyo.
Balozi Mhandisi Kijazi alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa
Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na baadaye Shahada
ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha
Birmingham, Uingereza mwaka 1992.
Balozi Mhandisi John Kijazi amemuoa Fransiscar Kijazi na pamoja wamejaliwa watoto watatu, David, Emmanuel na Richard Kijazi.
Balozi Mhandisi John Kijazi ataapishwa leo tarehe 7 Machi 2016 na
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Ikulu jijini Dar es salaam.
Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa
Umma,Wizara ya Mambo ya Nje,Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Kikanda na
Kimataifa,07 Machi 2016.
Post a Comment