alahly4

Wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano makubwa ya vilabu barani Afrika (CAF Champions League), Yanga wametolewa katika mashindano hayo baada ya kupokea kichapo cha goli 2-1 kutoka kwa Al Ahly ya Misri.
Katika mchezo huo ambao ulionekana timu zote kukamiana ulianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu na hadi mapumziko hakuna timu iliyokuwa imefanikiwa kuona lango la mwenzake.
Kipindi cha pili Al Ahly ilifanikiwa kupata goli kupitia mchezaji wake Hossam Ghaly katika dakika ya 51 ya mchezo huo na dakika 15 mbele yaani dakika ya 66 Yanga ilisawazisha goli hilo kupitia Donald Ngoma.
Mchezo huo uliendelea kwa timu zote kushambuliana kwa zamu na katika dakika ya 90+5 ya mchezo huo, Al Ahly kupitia Abdallah El-Said ilipata goli la pili nala ushindi ambalo limewawezesha kuingia nafasi inayofuatia.
Baada ya matokeo hayo, Yanga imetolewa katika mashindano hayo na kuungana na wenzao Azam ambao nao walitolewa jana ambao wote walikuwa wakishiriki mashindano ya vilabu Afrika ambayo yanaandaliwa na Chama cha Soka Afrika (CAF).