Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

Polisi Washuhudia Majambazi Yakitwangana Risasi, Zakamatwa Shehena za Silaha na Vifaa vya Uhalifu

WATU watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wa kutumia silaha, ambao wamehusika kufanya matukio mbalimbali ya kihalifu katika mkoa wa Dar es Salaam, wameuawa na majambazi wenzao katika eneo la Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Licha ya kuuawa kwa majambazi hao, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limefanikiwa kuwakamatwa watu zaidi ya saba, wanaosadikiwa kuhusika na tukio la majibizano ya risasi na polisi, lililotokeo Vikindu lililosababisha kifo cha askari mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Sirro alisema kabla ya kuuawa watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti ya Mbagala, Keko na Kawe jijini humo.

Alisema watu hao walikamatwa kufuatia tukio la ujambazi, lililotokea Agosti 29, mwaka huu katika Jengo la Sophia House maeneo ya Veta Changombe, ambapo majambazi hao walidaiwa kupora Sh milioni 35 na kutoweka kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah lenye namba bandia T 549 BPK.

Aliongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo, uliendelea kufanyika na Septemba 3, timu ya upelelezi kutoka Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, iliweka mtego na kufanikiwa kuwakamata majambazi hao watatu na walipohojiwa walikiri kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi wa kutumia silaha na kuweza kutaja silaha mbalimbali walizonazo.

Kamanda Sirro alisema majambazi hao, waliwapeleka askari eneo la Mbezi Chini katika nyumba waliyokuwa wamekodi na askari walifanya upekuzi na walifanikiwa kupata silaha mbalimbali, zikiwemo bunduki 23 na risasi zaidi ya 800 na vitu vinginevyo.

Alitaja silaha hizo kuwa ni bunduki za kijeshi tatu aina ya SMG zikiwa na magazini nane na risasi 120, bastola 16, magazini tatu za bastola na risasi moja, Shot gun pump action tatu na risasi 130, bastola 16 magazini na risasi 548 na bunduki tatu aina ya Shot gun na risasi zake 130.

Aidha alisema walikuta redio za mawasiliano 12 na chaja zake tatu, darubini za kuonea mbali tatu, pingu za plastiki 45, majaketi ya kuzuia risasi matatu, mkasi mmoja wa kukatia vyuma, mtarimbo mmoja, risasi baridi za kutishia 37, boksi moja la kusafishia silaha, nyundo kubwa moja, pingu za chuma tatu, mashine moja ya kuhifadhia kumbukumbu na magari mawili.

Alisema uchunguzi wao ulibaini kuwa majambazi hao Septemba 6, mwaka huu walipora bunduki aina ya Shot gun yenye namba 006091830, ikiwa na risasi moja katika barabara ya Mbozi Chang’ombe.

Sambamaba na hayo, majambazi hao walikiri kuhusika na wizi wa mamilioni ya fedha katika Benki ya Habib African ya Kariakoo mwaka 2014 na Benki ya Stanbic mwaka 2014, wakitumia gari aina ya Toyota Noah.

Kamanda Sirro alisema baada ya mahojiano zaidi, majambazi hao walisema wanazo silaha nyingine ambazo wamezificha Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Ndipo askari walifuatana na watuhumiwa hao hadi kwenye msitu wa Vikindu.

Alisema askari walipofika eneo hilo, walilodai ni karibu na zilipo silaha hizo, walishuka kwenye gari na kuingia porini wakiwa wamewatanguliza watuhumiwa mbele majira ya usiku.

Aliongeza kuwa wakiwa msituni humo na askari wakiwa wenye tahadhari kubwa, ghafla walisikia milio ya risasi ikitokea mbele, ambapo askari walilala chini na baadaye zikisikika sauti zikisema ‘mmetuua sisi’.

Alisema baada ya risasi za mfululizo kutulia, askari walishuhudia majambazi hao ambao walichelewa kulala chini wakati risasi zikipigwa wakiwa wamejeruhiwa sehemu za kifuani na tumboni huku wakivuja damu nyingi.

Alisema askari walipiga risasi kuelekeza eneo zilikotokea risasi na walipoendelea kusonga mbele, walikuta silaha aina ya SMG ikiwa imetelekezwa na haikuwa na risasi ndani ya magazine, hivyo kufanya idadi ya silaha za SMG kufikia nne.

Aidha alisema askari waliwabeba majambazi hao na kuwapeleka kwenye gari kuelekea hospitalini, lakini wote walifariki dunia wakiwa njiani kutokana na kutoka damu nyingi.

Akizungumzia tukio la Vikindu, Sirro alisema wamefanikiwa kuwakamata watu hao wanaosadikiwa kuhusika na tukio ambalo lilisababisha kifo cha askari mmoja.

“Majambazi hao walikuwa ni kundi la kama watu 14 na tayari tumewakamata zaidi ya saba ambao mpaka sasa tunawashikilia kwa mahojiano zaidi ili kufanikisha upelelezi,” alisema Kamanda Sirro.

Pia alisema kumekuwa na taarifa mbalimbali, zikisambazwa katika vyombo vya habari zikidai kuwa katika tukio la Vikindu, kuna askari anahusika na tukio hilo na kudai taarifa hizo si za kweli na hakuna askari aliyehusika katika tukio hilo.

Katika tukio lingine, jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kwa makosa ya wizi wa magari manane, likiwemo gari moja la kibalozi.

Kamanda Sirro alisema magari hayo yaliibwa jijini Dar es Salaam na kuuzwa kwa watu mbalimbali jijini hapo na mikoani na watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na mara upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Sirro alisema katika tukio lingine jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita wanaodaiwa kuhusika na kuvunja nyumba usiku na kuiba.

Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na mara upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

KUELEKEA SEPTEMBA MOSI POLISI WAENDELEA NA MAZOEZI HUKO MOSHI

Moshi. Mazoezi ya Polisi mkoani Kilimajaro yaliyodumu kwa takriban saa nne yaliyofanywa na vikosi vya askari wa kutuliza ghasia na magari ya washawasha, yametikisa mji wa Moshi na kuzua hofu kwa  wananchi.
Baadhi ya wananchi walishangazwa na kitendo hicho cha polisi  kuzunguka wakiwa na mabomu ya machozi na gari la maji ya washawasha.

Mkazi mmoja, Peter Lyimo alisema ameshtushwa kuona magari ya polisi yakizunguka, huku milio ya milipuko ya mabomu ikisikika.

Naye Mary Kavishe alisema: “Tumezoea kuona polisi wakifanya mazoezi kambini kwao, siyo kuzunguka katikati ya mji.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbrod Mutafungwa  alisema wanafanya mazoezi ya kawaida ya kujihami na wahalifu  na kulinda wananchi na mali zao.

“Ni mazoezi ya kawaida na yanafanyika mkoa mzima kwa ajili ya kuimarisha askari wetu,  ili kujihami na matukio mbalimbali ya kihalifu,” alisema.

Mke wa Trafiki Kinyogori Adaiwa Kukiri Kumuua Mumewe

MKE wa askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki), Sajenti Ally Salum (Kinyogori) aliyeuawa hivi karibuni, inadaiwa amekiri kuhusika kwenye mauaji hayo, akidai ilitokana na mumewe kumuacha na kuoa mke mwingine.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa mauaji hayo yaliyofanyika nyumbani kwa Kinyogori, Mkuranga mkoani Pwani.

Wakati huo huo, Kamanda Sirro amezungumzia pia mauaji ya Anathe Msuya yaliyofanyika hivi karibuni Kigamboni na kusema polisi inaendelea kumtafuta msichana wa kazi za nyumbani aliyetoroka siku moja kabla ya kifo cha mwanamke huyo.

Anayetuhumiwa kuua mumewe
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu yaliyojitokeza jijini Dar es Salaam, Sirro alisema katika mahojiano ya awali mke wa Kinyogori amekiri kuhusika.

Kwa mujibu wa kamanda, mwanamke huyo ambaye hata hivyo hakutaja jina lake kwa sababu za kipelelezi, aliamua kumtuma mtu kutekeleza mauaji hayo baada ya mumewe kumwacha na kuoa mke mwingine.

“Ni jambo la kusikitisha kuona mtu anatoa uhai wa mtu sababu ya kuachwa. Tunawasihi wananchi kuepuka kujihusisha na matukio kama haya, eti sababu tu ya kuachwa wanawake wapo wengi na wanaume wapo wengi unaweza kuachwa na ukaolewa na ukaoa kuliko kuondoa uhai wa mtu,” alisisitiza Sirro.

Hata hivyo, Sirro alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili waweze kuwataja watu wengine walioshirikiana nao kutekeleza tukio hilo baada ya kuonekana kuwepo kwa wahusika wengine.

‘Hausigeli’ asakwa
Kuhusu mauaji ya Anathe aliyechinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, Kamanda Sirro alisema wanaendelea na jitihada za kumtafuta msichana huyo ahojiwe kuhusu tukio hilo.

Aidha alisema mtu mmoja anashikiliwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo huku polisi ikiwa imeandaa timu ya upelelezi itakayoshughulikia tukio hilo kufanikisha kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.

Sirro alisema msichana huyo aliondoka siku moja kabla ya tukio hilo la mauaji hivyo kupatikana kwake, kunaweza kusaidia polisi kujua kama kuondoka kwake kulikuwa salama au kuna kitu kimejificha.

“Msichana huyu tunaendelea kumsaka tujue kama aliondoka salama na kumhoji zaidi juu ya kuondoka kwake siku moja tu, tukio linatokea nina imani tutafanikiwa kumpata na wote waliohusika na kukomesha matukio haya,” alisema Sirro.

Mamia wajitokeza msibani
Vilio na simanzi jana vilitawala wakati mamia ya wakazi wa Kibada Kigamboni na Salasala walipokuwa wakiuaga mwili wa marehemu Anathe Msuya (30), aliyeuawa Mei 25 nyumbani kwake kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.

Mwili ulichukuliwa jana asubuhi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na kupelekwa nyumbani kwake Kibada, kwa ajili ya kuagwa na majirani zake kabla ya kusafirishwa kwenda kuzikwa mkoani Arusha leo.

Akizungumza baada ya mamia kumuaga nyumbani kwa marehemu, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyakwale Kibada, Said Pazi alisema kuwa wao kama majirani waliomba familia wapate fursa ya kumuaga jirani yao ambaye tangu ahamie ana muda wa miezi sita.

“Baada ya kuambiwa msiba upo Salasala tuliomba kama majirani na sisi tupatiwe fursa ya kuuaga mwili wa ndugu yetu ambaye alihamia mwaka jana… kwa kweli msiba wake umetusikitisha sana” alisema.

Akizungumzia tukio hilo alisema kuwa mtoto wa marehemu huyo, Allan Kimario (4) aliwataarifu majirani kuwa mama yake haamki na ndipo walipofika wakakuta ameuawa.

Mwenyekiti huyo alitoa pole na kusema atahakikisha wanaimarisha ulinzi na kuhimiza wenye viwanja ambavyo havijajengwa, wavifanyie usafi ili kuondoa vichaka ambavyo ni hatari kwa usalama.

Upotevu wa Makontena 349 Bandarini: Watu 12 Watiwa Mbaroni na Jeshi la Polisi

Kufuatia agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa la kuwataka watuhumiwa wa wizi wa makontena 329 katika bandari ya Dar es salaam kuchukuliwa hatua na Jeshi la Polisi, tayari Jeshi hilo limewashikilia watuhumiwa kumi na mbili wanaohusika na wizi huo.

Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam,  Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CP) Diwani Athumani amesema kuwa, uchunguzi unaofanywa na wataalamu waliobobea katika makosa ya uhalifu wa kifedha umeweza kuwabaini watu kumi na mbili  ambao wamehusika na wizi huo.

“Kati ya watuhumiwa hao kumi na mbili, watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na saba bado wapo katika upepelezi na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Athumani.

Wanaoshikiliwa kutokana na tuhuma mbalimbali ni Kamishna wa Idara ya Forodha na Ushuru TRA Bw. Tiagi Masamaki, Meneja Kitengo cha Huduma za Ushuru  na Bi.  Habib Mponezia, Msimamizi Mkuu wa Kitengo cha Ushuru wa Forodha.

Watuhumiwa wengine ni pamoja na Bi. Eliaichi Mrema, Msimamizi Kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta  Bw. Haroun  Mpande na Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara Bw. Hamis Omary.

Aidha Kamanda Athumani amewaomba wananchi wenye taarifa za ubadhilifu wa mali za Umma kuendelea kulisaidia Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu yake.
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top