Imeandikwa Alex Nicholaus Mushi katika ukurasa wake wa Facebook akipinga Waraka wa Nape alioutoa dhidi ya Mgomo wa Madaktari soma zaidi Alivyoandika....
TUJISAHIHISHE!
(waraka wa Nape dhidi ya mgomo wa Madaktari)
Haya hatukukuzwa nayo.,wala si taratibu katika mila zetu kama watanzania. Katika utawala wowote lazima ziwepo changamoto ambazo serikali inalazimika kuzishughulikia, miongoni mwake ni migomo katika waajiriwa wa serikali, taasisi binafs na hata makundi ya watu yasiyo rasmi. Lakini kila mgomo una athari zake na namna ya kuumaliza.
Jamii ya watanzania imekuzwa katika Utaifa na Uzalendo. Kwa maana Taifa ni msingi wa mapambano ya mtu binafsi kisha yanafuata masuala binafsi. Huu ndio msingi tulioachiwa na waasisi wa Taifa hili. Kuachwa na kudharauliwa kwa misingi hii kunabadilisha namna ya maisha yetu, hatuhurumiani tena, hatusaidiani na wala hatupendani.
Wanalolifanya madaktari lina sura hii ya kubadilika kwa namna ya maisha yetu kwa sasa. Ni kweli maslahi ya kila mmoja wetu ni muhimu hasa katika kazi aliyoitolea jasho. Na hata nyongeza na mazingira mazuri ya kazi ni kitu cha msingi katika utendaji wa yeyote katika sisi,lakini sidhani kuwa kudai nyongeza kwetu na mazingira bora kunalazima kuacha fulani afe ukimtazama akiwa anakufa kwa kuwa si ndugu yako, wala si mtu unayemfahamu kwa ukaribu ama rafiki kwa kuona maslahi yako ni bora kuliko maisha ya mwingine, na bahati mbaya mwingine huyo hana uhusika wa namna yeyote katika kuzuilia ama kutozuilia maslahi hayo, hili si la kuungwa mkono kwa namna yeyote. TUNAPOTOKA kama jamii itaunga mkono hili na lazima wawepo watu miongoni mwetu wakukosoa ili TUJISAHIHISHE...!
......................@@@@@@@@@>>>>>>>>>@@@@@@@@@..........................
NITOFAUTIANE NA NAPE KATIKA BAADHI YA HOJA ZAKE.
Namuunga mkono kabisa Nape Nnauye katika hoja kuwa, nanukuu "Jamii ya watanzania imekuzwa katika Utaifa na Uzalendo. Kwa maana Taifa ni msingi wa mapambano ya mtu binafsi kisha yanafuata masuala binafsi. Huu ndio msingi tulioachiwa na waasisi wa Taifa hili. Kuachwa na kudharauliwa kwa misingi hii kunabadilisha namna ya maisha yetu, hatuhurumiani tena, hatusaidiani na wala hatupendani"
Sasa nianze kwa kuonesha kwa jinsi gani anachokisemea kinavyokosa nguvu, yeye anaona madaktari wanafanya mambo yanayokiuka tamaduni na mila zetu akisahau mabaya na ukiukwaji wa mila na tamaduni hizo hizo unaofanywa na chama chake (CCM). Mambo ambayo hayahitaji miwani kuyaona. Mambo yanayosadifu vilivyo ukiukwaji wa misingi ya mila na utamaduni wetu tuliochiwa na wasisi wetu wa taifa.
Pengine Nape anaweza akawa haifahamu vizuri historia yetu kama taifa kwa sababu ni kijana kama mimi hatujaishi sana kama wazee wetu, lakini namhamasisha akashike vitabu na asome vizuri historia yetu. Tunu za ushikamano, umoja, udugu na upendo ni zao la misingi iliyoasisi taifa letu la Tanzania. Lakini chama cha CCM, chama tawala kimekuja kupoteza tunu hizo kwa kuanza kuwalea viongozi wabinafsi, walafi, waliojali familia zao, wasio na upendo na kuwasahau watanzania wengi waliowapa dhamana ya kuwaongoza.
CCM ya sasa haijahishia hapo bali kupitia serikali yake watu wameiba pesa za nchi mabilioni kwa mabilioni ya shilingi ambayo wameyaficha kwenye maakauti nje ya nchi. Viongozi hao wameliingizia taifa hasara ya mabilioni ya shilingi. Pia wameliingiza taifa katika mikataba isiyo na tija kwa mf. mikataba mibovu ya madini, mikataba mibovu ya utalii, mikataba mibovu ya ujenzi na kadhalika. Ubinafsi huu ni dhahiri Uzalendo na Utaifa ambao wazee wetu walituachi kama alivyosema Nape imetupiliwa mbali.
Na suala hili la viongozi wa CCM kujinufaisha na kusahau wananchi wanaokufa vijijini bila kupata dawa ambazo zingeweza kununuliwa na fedha hizo zinazokwapuliwa si la jana bali ni la muda mrefu lakini viongozi wa serikali na chama wamenyamaza kimya bila ya kuwachukulia hatua yoyote na muda mwingine kuwakingia kifua.
Sasa najiuliza inakuwaje nape anakuja kuona kuwa madaktari wamepoteza misingi tuliyokuziwa na wazee wetu ili hali anaona kinachofanywa na chama chake kupitia serikali? Nape unawezaje kuona kutokuwa na uzalendo na utaifa kwa madaktari na kuacha kuyaona hayo hayo ndani ya chama chako (CCM)? Nape waraka wako unamaanisha kweli?
Nibainishe wazi kuwa anaesababisha watanzania wengi kufa ni serikali kwasababu wanawachekea wezi wanaolihujumu taifa kwa kukwapua mabilioni ya pesa, kwa kuliingiza taifa katika mikataba ya ovyo isiyo na tija kwa taifa, kuuza mali za taifa kwa bei ya kutupwa, na kutoa misamaha ya kodi ya karibu bilioni 1400.
Pesa zote hizo zinazopotea ni wazi ndizo pesa za madaktari wanazogoma kuzihitaji ili kuboresha utoaji wa huduma, pesa hizo hizo ndizo zinazochochea walimu kutangaza mgomo nchi nzima, pia ndio pesa ambazo zingeweza kuokoa maelfu ya watanzani wanakufa kutokana na kukosekana kwa hospitali katika maeneo yao na madawa katika hospitali zao.
Kaka yangu NAPE alieacha watanzania wafe ni CCM kupitia serikali yake kabla ya madaktari, tena wao (serikali) wameacha watanzania wengi sana wafe kuliko madaktari. CCM na serikali yake inafanya hivi kutokana na ukweli kuwa ule UPENDO,UZALENDO na UTAIFA tulioachiwa na waasisi wa taifa hili ambao tulikuziwa umewatoka na kuingiwa roho chafu ya UBINAFSI, ULAFI, UNYAMA na UKATILI ambao kwa miaka mingi tulizoea kuusikia katika nchi zinazoongozwa na serikali za KIDIKTETA.
NAPE ni dhahiri Madaktari huenda wanafanya hivyo kwa sababu baba (serikali) yao ambaye anatakiwa kuwa mfano anafanya hivyo. Na hii si Ajabu hata kidogo kwa sababu mtoto wa nyoka ni nyoka.
"....toa BORITI kwenye jicho lako ili uone KIBANZI kwenye jicho la mwenzio........."
Na Alex Nicholaus Mushi.
Post a Comment